Maximilian John Ngube a.k.a.  'Max' 
Na Muhidin Issa Michuzi
Mkiwa katika kazi na kukuta kule kusukumana na hata kupigana makumbo na makelele hakujaanza, basi ujue hajafika bado.
Ila mara tu yeye akishatia mguu wake kwenye sehemu ya tukio ambayo wanahabari wapigapicha mmejipanga baada ya  kukubaliana wapi pa kusimama, lazima zogo liumuke. 
Maana yeye ile  akifika tu hapo mahali (aghalabu alichelewa kufika kutokana na daima kuwa na kazi nyingi sehemu zingine kwa wakati mmoja) aidha alipiga watu vipepsi na kuchukua nafasi kibabe, ama bila kujali aliamua kukaa mbele yenu hadi mlazimike kumpisha na kumpa nafasi muafaka inayomfaa.
Baada ya  hapo ndipo anapogeuka na kuwasalimia;  “Jamani hamjambo lakini?” Nanyi, Badala ya kukasirika na kumsemea mbovu, wote mnajikuta mnacheka na kukubaliana kwamba naam! Max keshawasili na sasa kazi inaanza rasmi… 
Na uzuri wake akishasimama mahali anapoona panamfaa kuchukua picha vizuri, alikuwa hana tena bughudha na mtu.
Hakika ni wanahabari wachache waliojaaliwa kuwa na moyo wa kuthubutu na kupenda kazi (daring and passionate)  kama yeye. Bahati mbaya tunamaizi haya wakati akiwa hayupo nasi tena hapa duniani. Tutaku-mmiss vibaya sana!
Huyo si mwingine bali Mpigapicha mkongwe wa Luninga, Maximilian John Ngube ama 'Max'  kama ambavyo  kila mtu alizoea kumwita tokea akiwa mchezaji wa Yanga miaka hiyo ya nyuma, tokea akiwa mfanyakazi wa Star TV na tokea akiwa  Mlimani TV alikohitimisha majukumu yake akiwa nyota wa mchezo.
Yaani hadi sasa siamini kwamba rafiki yangu mpendwa na mkorofi,  mfanyakazi mwenzangu,  mpiganaji huyu aliyetutoka ghafla siku ya   Ijumaa Mei 23, 2014, Max, jijijini Dar es salaam hatunaye tena.
Jamani, ni nani tena atakayekuwa anatupiga vipepsi ama kukaa mbele yetu na kutukera na baadaye kutuchekesha wakati wa kuchapa kazi? Ni nani atakayekuwa anafanya tutabasamu, badala ya kukasirika, afikapo sehemu ya tukio, akiwa kachelewa kutokana na kuchapa kazi sehemu mbalimbali kwa siku moja?
Hakika Mlimani TV,  pamoja na tasnia nzima ya habari, tumepoteza Jembe lisilo la kawaida! Max alikuwa na atadumu kuwa mfano wa kuigwa katika tasnia hii adhimu.
Mara ya mwisho mie kuchapa naye kazi bega kwa bega ilikuwa ni siku ya Mei Mosi pale uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam, wakati aliponichana mbavu kwa kung’ang’ania kumpiga picha mwanamama mmoja tu kwa muda mrefu kama kwamba ni yeye pekee alikuwa katika maandamano makubwa ya wafanyakazi siku hiyo.
 “Yule ni mke wangu!” aliniambia baada ya kumyanyulia ukope mmoja kwa namna ya kumuuliza kulikoni tena mwenzetu??.
Sina uhakika, lakini  huenda hiyo ilikuwa ni siku ya kwanza - na ya mwisho – kwa Max  kumrekodi mpendwa mke wake kwa ajili ya taarifa ya habari katika kituo cha Mlimani TV alikokuwa akifanyia kazi. Kumbuka, hiyo ni nafasi nadra mno kupatikana kwa wanahabari. Na yeye aliitumia vyema mno. Samahani Mhariri wa Mlimani TV kwa kutoboa siri hii… 
Habari za umauti wake nilizipata mapema asubuhi ya siku hiyo kutoka kwa rafiki yetu Iddi  Janguo. “Aisee rafiki yako amefariki leo alfajiri. Je,  una habari?”, aliniambia kwa simu milango ya  saa moja hivi za asubuhi. Bahati mbaya sikuwa Dar es salaam Nilikuwa Pretoria, Afrika ya Kusini, kikazi. Nami hapo hapo nikaamsha vijana wangu na kuwaomba wafuatilie taarifa hizo na kuzirusha mara tu baada ya kupata uhakika, kama ilivyo kawaida yetu Globu ya Jamii. 
Si rahisi rafiki na mfanyakazi mwenzio ama mtu uliyemzoea maishani mwako kumwita marehemu, kama ninavyojikuta mie katika hali ngumu leo kumtaja Max kama marehemu. Yeye atakuwa marehemu kwa wote lakini sio sisi tuliokuwa naye karibu kikazi. Kwetu atabakia kuwa Max tu. Max mtu wa fujo.  Max mpenda kazi.  Max ambaye atafanya lolote mradi atimize wajibu wake.
Buriani Max…
Tutakuwa nawe katika mioyo yetu Daima.
Mola na aipumzishe roho yako mahali pema Peponi
AMINA...







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. Robin UlikayeMay 27, 2014

    Robin frm Mby...Nikiwa Mhariri wa Picha Mlimani TV wakati huo 2010,2011 mara kadhaa aliniambia "Mwanangu weka picha hii" akiamini ilikuwa picha nzuri zaidi, lakini ukweli utasalia kwamba alikuwa shooter mahiri miongoni mwa wapiga picha wa Televisheni hapa nchini...Zaidi aliipenda sana kazi yake...Nakumbuka waandishi walipenda sana kuambatana na mpigapicha Max kwani alifanya kazi iliyomakinika...Go Max behind you us!

    ReplyDelete
  2. AnonymousMay 27, 2014

    JAMANI NAOMBA KUULIZA KUHUSU HUYU KAKA. SURA YAKE NAIKUMBUKA PALE KINONDONI KWENYE MIAKA YA THEMANINI MWISHONI LAKINI KUMBUKUMBU YANGU NI ALIKUWA MTU KUTOKA ZAIRE AU SIJUI NIMEMCHANGANYA NA MTU MWENGINE. NAOMBA MNIJUZE MNAOMFAHAMU.

    ReplyDelete
  3. RIP Max Ngube, Ndugu Said ni kweli Max alikuwa akiishi maeneo ya Kinondoni kwa muda mrefu hasa katika Mtaa wa Ufipa.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...