![]() |
Maximilian John Ngube a.k.a. 'Max' |
Na Muhidin Issa Michuzi
Mkiwa katika kazi na kukuta
kule kusukumana na hata kupigana makumbo na makelele hakujaanza, basi ujue
hajafika bado.
Ila mara tu yeye akishatia
mguu wake kwenye sehemu ya tukio ambayo wanahabari wapigapicha mmejipanga baada
ya kukubaliana wapi pa kusimama, lazima
zogo liumuke.
Maana yeye ile akifika tu hapo
mahali (aghalabu alichelewa kufika kutokana na daima kuwa na kazi nyingi sehemu
zingine kwa wakati mmoja) aidha alipiga watu vipepsi na kuchukua nafasi kibabe,
ama bila kujali aliamua kukaa mbele yenu hadi mlazimike kumpisha na kumpa
nafasi muafaka inayomfaa.
Baada ya hapo ndipo anapogeuka na kuwasalimia; “Jamani hamjambo lakini?” Nanyi, Badala ya
kukasirika na kumsemea mbovu, wote mnajikuta mnacheka na kukubaliana kwamba
naam! Max keshawasili na sasa kazi inaanza rasmi…
Na uzuri wake akishasimama
mahali anapoona panamfaa kuchukua picha vizuri, alikuwa hana tena bughudha na
mtu.
Hakika ni wanahabari
wachache waliojaaliwa kuwa na moyo wa kuthubutu na kupenda kazi (daring and
passionate) kama yeye. Bahati mbaya
tunamaizi haya wakati akiwa hayupo nasi tena hapa duniani. Tutaku-mmiss vibaya
sana!
Huyo si mwingine bali Mpigapicha
mkongwe wa Luninga, Maximilian John Ngube ama 'Max' kama ambavyo kila mtu alizoea kumwita tokea
akiwa mchezaji wa Yanga miaka hiyo ya nyuma, tokea akiwa mfanyakazi wa Star TV
na tokea akiwa Mlimani TV alikohitimisha majukumu yake akiwa nyota wa mchezo.
Yaani hadi sasa siamini kwamba rafiki yangu mpendwa na mkorofi, mfanyakazi mwenzangu, mpiganaji huyu aliyetutoka ghafla siku ya Ijumaa
Mei 23, 2014, Max, jijijini Dar es salaam hatunaye tena.
Jamani, ni nani tena atakayekuwa anatupiga vipepsi ama kukaa mbele yetu na
kutukera na baadaye kutuchekesha wakati wa kuchapa kazi? Ni nani atakayekuwa
anafanya tutabasamu, badala ya kukasirika, afikapo sehemu ya tukio, akiwa
kachelewa kutokana na kuchapa kazi sehemu mbalimbali kwa siku moja?
Hakika Mlimani TV, pamoja na
tasnia nzima ya habari, tumepoteza Jembe lisilo la kawaida! Max alikuwa na
atadumu kuwa mfano wa kuigwa katika tasnia hii adhimu.
Mara ya mwisho mie kuchapa naye kazi bega kwa bega ilikuwa
ni siku ya Mei Mosi pale uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam, wakati
aliponichana mbavu kwa kung’ang’ania kumpiga picha mwanamama mmoja tu kwa muda
mrefu kama kwamba ni yeye pekee alikuwa katika maandamano makubwa ya
wafanyakazi siku hiyo.
Sina uhakika, lakini huenda hiyo ilikuwa ni siku ya kwanza - na ya
mwisho – kwa Max kumrekodi mpendwa mke
wake kwa ajili ya taarifa ya habari katika kituo cha Mlimani TV alikokuwa akifanyia
kazi. Kumbuka, hiyo ni nafasi nadra mno kupatikana kwa wanahabari. Na yeye
aliitumia vyema mno. Samahani Mhariri wa Mlimani TV kwa kutoboa siri hii…
Habari za umauti wake nilizipata mapema asubuhi ya
siku hiyo kutoka kwa rafiki yetu Iddi Janguo. “Aisee rafiki yako amefariki leo
alfajiri. Je, una habari?”, aliniambia kwa
simu milango ya saa moja hivi za asubuhi.
Bahati mbaya sikuwa Dar es salaam Nilikuwa Pretoria, Afrika ya Kusini, kikazi.
Nami hapo hapo nikaamsha vijana wangu na kuwaomba wafuatilie taarifa hizo na
kuzirusha mara tu baada ya kupata uhakika, kama ilivyo kawaida yetu Globu ya
Jamii.
Si rahisi rafiki na mfanyakazi mwenzio ama mtu
uliyemzoea maishani mwako kumwita marehemu, kama ninavyojikuta mie katika hali
ngumu leo kumtaja Max kama marehemu. Yeye atakuwa marehemu kwa wote lakini sio
sisi tuliokuwa naye karibu kikazi. Kwetu atabakia kuwa Max tu. Max mtu wa fujo.
Max mpenda kazi. Max ambaye atafanya lolote mradi atimize
wajibu wake.
Buriani Max…
Tutakuwa nawe katika mioyo yetu Daima.
Mola na aipumzishe roho yako mahali pema Peponi
AMINA...
Robin frm Mby...Nikiwa Mhariri wa Picha Mlimani TV wakati huo 2010,2011 mara kadhaa aliniambia "Mwanangu weka picha hii" akiamini ilikuwa picha nzuri zaidi, lakini ukweli utasalia kwamba alikuwa shooter mahiri miongoni mwa wapiga picha wa Televisheni hapa nchini...Zaidi aliipenda sana kazi yake...Nakumbuka waandishi walipenda sana kuambatana na mpigapicha Max kwani alifanya kazi iliyomakinika...Go Max behind you us!
ReplyDeleteJAMANI NAOMBA KUULIZA KUHUSU HUYU KAKA. SURA YAKE NAIKUMBUKA PALE KINONDONI KWENYE MIAKA YA THEMANINI MWISHONI LAKINI KUMBUKUMBU YANGU NI ALIKUWA MTU KUTOKA ZAIRE AU SIJUI NIMEMCHANGANYA NA MTU MWENGINE. NAOMBA MNIJUZE MNAOMFAHAMU.
ReplyDeleteRIP Max Ngube, Ndugu Said ni kweli Max alikuwa akiishi maeneo ya Kinondoni kwa muda mrefu hasa katika Mtaa wa Ufipa.
ReplyDelete