Hatimae Bingwa wa Mashindano ya Kombe ya Muungano yaliyoanza kutimua vumbi tarehe 23 April Mwaka huu na kushirikisha Timu za Soka zipatazo Kumi na Moja za Jimbo la Kiembe Samaki Wilaya ya Magharibi amepatikana na kufikia hatma yake kwenye uwanja wa michezo wa Kiembe Samaki.

Chukwani United ilitawadhwa kuwa bingwa wa kombe hilo baada ya kuikung’uta New Generation ya Kiembe samaki kwa Magoli mawili kwa bila kwenye pambano la fainali ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akijumuika na mamia ya wapenzi wa mchezo wa soka walioshuhudia pambano hilo kali na la kuvutia.

Magoli yote mawili ya Timu ya Soka ya Chukwani United yaliwekwa kimiani katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo ambapo Goli la kwanza lilifungwa na mchezaji Khatib Abdulla lile la pili likafungwa na Mfaume Abdulla.

Akizungumza mara baada ya pambano hilo mgeni rasmi wa fainali hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewapongeza vijana hao pamoja na Uongozi wa Jimbo la Kiembe Samaki kwa uamuzi wao wa kuandaa na kushiriki kwenye mashindano hayo kwa njia ya amani na salama.

Balozi Seif alisema mchezo wa soka hivi sasa umekuwa ukitoa ajira kubwa Kitaifa na Kimataifa. Hivyo aliwaasa Vijana hao kuendelea kufanya bidii katika kudumisha mchezo huo ili hapo baadaye mchezo huo usaidie fursa nzuri ya kuwaendeshea maisha yao. Katika Fainali hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikabidhi zawadi mbali mbali kwa washindi wa mashindano ya kombe hilo la Muungano zilizotolewa na Mwakilishi wa Jimbo la Kiembe Samaki sambamba na yeye binafsi kuongeza zawadi ya mipira miwili kwa kila Timu iliyoshiriki mashindano hayo kati ya timu 11.

Mapema Mwakilishi wa Jimbo la Kiembe Samaki Mahmoud Thabit Kombo ambae ndie aliyedhamini michezo hiyo alisema Uongozi wa Jimbo hilo ulifikia hatua ya kuandaa mashindano hayo ya kombe la Muungano ili kupata mapumziko mazuri ya bunge Maalum la Katiba lililokuwa likiendelea Mjini Dodoma.
Timu za Chukwani United iliyovalia jezi rangi nyekundu na New Generation zikimenyana ndani ya dimba la Kiembe samaki katika mchezo wa fainali ya Kombe la Muungano ambapo chukwani United ilitawadhwa kuwa bingwa wa kombe hilo kwa kuichakaza New Generation goli 2-0 Mgeni rasmi akiwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif Ali Iddi.
Mwakilishi wa Jimbo la Kiembe Samaki Mahmoud Thabit Kombo akifafanua mpangilio wa zawadi zitakavyotolewa kwa washindi na washiriki wa Kombe la Muungano lililoandaliwa ndani ya Jimbo hilo. Kushoto yake ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na pembeni yake ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mahindano.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi Kikombe pamoja na baadhi ya zawadi Kepteni wa Timu ya Soka ya Chukwani United Mohd Golo baada ya Timu yake kushinda mchezo wa Fainal kwa goli 2-0 dhidi ya New Generation.
Wachezaji wa timu ya soka ya Chukwani United wakishangiria ushindi wao dhidi ya Timu ya New Generation iliyoupata wa Goli 2-0 kwenye mchezo wa fainali wa mashindano ya Kombe la Muungano lililoandaliwa ndani ya Jimbo la Kiembe Samaki. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...