Kaimu mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Kuhifadhi Wanyamapori Bw. John Muya akiwaeleza
waandishi wa habari mafanikio yaliyofikiwa na Mfuko huo katika Kupambana na Ujangili katika kipindi
cha miezi mitatu iliyopita.
Kaimu mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Kuhifadhi Wanyamapori Bw. John Muya akitoa wito kwa
waandishi wa habari (hawapo pichani) kushiriki katika mapambano dhidi ya ujangili ili kulinda rasilimali
za Taifa ambazo ziko hatarini Kutoweka,Kulia kwake ni Afisa Habari wa Idara ya Habari Maelezo Bi
Georgina Misama,kutoka kushoto ni Afisa Habari wa Mfuko huo Bi. Tabu Nziku , Kaimu Katibu Tawala
wa Mfuko huo Bi Antonia Raphael.
(Picha zote na Frank Mvungi )
Na Georgina Misama-MAELEZO
MFUKO wa Kuhifadhi Wanyamapori Tanzania (TWPF) umebuni miradi ya
maendeleo kama vyanzo vya mapato ili kukabiliana na changamoto ya ufinyu wa
bajeti katika kutekeleza majukumu yake.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa mfuko huo Bw John Muya wakati
wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo.
Alisema kwamba mfuko umebuni miradi ya maendeleo ili kujiendeleza kwa
kuongeza mapato ambapo alitaja miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa Jengo la
Kakakuona na Pori la akiba la Pande.
Miradi mingine ni Bustani ya Wanyamapori ya Tabora, Bustani ya Wanyamapori
ya Ruhila-Songea na kambi ya Utalii katika Pori la akiba Selous.
Muya alisema TWPF husimamia ukusanyaji wa maduhuli, usimamizi wa uwindaji
wa kitalii na wa wenyeji, utalii wa picha, biashara ya wanyamapori hai na mazao
yatokanayo na wanyamapori, mashamba na bustani za ufugaji wa wanyamapori.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala wa TWPF Bi. Antonia Raphael alisema
mfuko hugharamia shughuli mbalimbali za usimamizi wa wanyamapori ikiwa ni
pamoja na usimamizi wa maeneo ya jumuia za hifadhi za wanyamapori (WMAs),
kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii na uendelezaji wa miundombinu katika mapori
ya akiba.
Mfuko hufanya malipo ya kifuta machozi kwa wananchi ambao ndugu zao
wameuawa au kujeruhiwa na wanyamapori ambapo kwa kipindi cha miezi mitatu
Januari –Machi 2014, kiasi cha shilingi milioni 9 kililipwa kwa ajili waliouwawa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...