Kufuatia wilaya ya Makete mkoani Njombe kuwa miongoni mwa wilaya zenye watoto yatima, wafanyakazi wa chuo cha VETA Makete wametembelea kituo cha kulelea watoto yatima cha Bulongwa kilichopo wilayani hapa na kutoa misaada mbalimbali

Akizungumza na mwandishi wetu kwa niaba ya wafanyakazi wenzake alioambatana nao Bw. Mathew Komba amesema wao kama VETA Makete wameguswa na namna watoto hao wanavyopata tabu kwani hawakupenda kuishi maisha hayo lakini kutokana na kufiwa na wazazi wao ndiyo maana wapo katika kituo hicho

Amesema awali walikuwa wamepanga kuwatembelea watoto hao kabla ya pasaka lakini kutokana na sababu zisizoepukika walishindwa kufanya hivyo lakini walijipanga kama walivyokuwa wamedhamiria na jana walifika kituoni hapo kuwaona watoto hao na kuwapa msaada huo

Bw. Komba amesema baadhi ya vitu walivyovikabidhi ni pamoja na mafuta ya kupikia, sukari, mchele, sabuni, juisi, dawa za meno na vingine vingi vyote vikiwa na thamani ya tsh. 329,000/=

Amewaomba wadau wengine kuwaunga mkono kwa kwenda kuwasaidia watoto yatima kwani ni jukumu la jamii kwa ujumla kuhakikisha wanawatunza watoto hao licha ya kwamba wanalelewa kwenye vituo mbalimbali

Kwa upande wake Bi Sekela Nkyami kutoka kituo hicho cha kulelea watoto yatima Bulongwa amesema ingawa kituo hicho kina vitega uchumi mbalimbali lakini bado kinategemea misaada kutoka kwa wafadhili mbalimbali wakiwemo wakazi wa Makete wenye moyo wa huruma kama walioufanya chuo cha VETA

Amesema watoto hao waliopo katika kituo hicho si mali ya kituo pekee bali ni wa jamii yote kwa hiyo kuiomba jamii kushirikiana nao katika matunzo ili watoto hao wasijisikie wapweke kutokana na uyatima walio nao


"Ni kweli uyatima unatesa, ila tunawaomba wananchi waje kutoa misaada mbalimbali kwa watoto hawa, kumekuwa na kasumba kuwa wakishaletwa hapa basi si wao tena bali ni wa kituo, hii sia sawa bali tunatakiwa tushirikiane kwa pamoja chochote kidogo utakachokipata kinatosha kutusaidia" amesema Bi. Nkyami
 Wafanyakazi wa VETA Makete wakiwa katika picha na watoto yatima wa kituo cha Bulongwa.
 Mfanyakazi wa VETA Makete akiwa amembeba mtoto yatima anayelelewa kituoni hapo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...