Na Mwandishi wetu, Lubumbashi
Wafanyabiashara wa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC) wamesema wana matumaini makubwa na hatua ya Tanzania kufungua ofisi ndogo ya mawasiliano ya Mamlaka ya Bandari (TPA) mjini Lubumbashi, jimbo la Katanga nchini humo.
Wakiongea kwa niaba ya wenzao baada ya kuzinduliwa kwa ofisi hiyo hivi karibuni, wafanyabiashara hao wanaopitisha mizigo yao katika bandari ya Dar es Salaam, wamesema kuanzishwa kwa ofisi hiyo kumekuja wakati muafaka na kuwa itawarahisishia biashara yao.
Sasa wafanyabiashara hao wataweza kufanya malipo ya bandari wakiwa Lubumbashi na kuepuka hatari ya kusafiri na kiwango kikubwa cha pesa na kuibiwa.
Mmoja wa wafanyabishara hao, Bw. Mubanzo Fils anayeendesha kampuni ya ETS Mubanzo alisema jumuiya ya wafanyabiashara Lubumbashi imefurahia sana kupata ofisi hiyo wanayotarajia kurahisisha kazi zao na kukuza biashara baina ya nchi hizo mbili.
“Tuna furaha kubwa sana kwa hatua hii muhimu,” alisema.
Inatarajiwa kwamba tatizo lililokuwa linawakabili wafanyabiashara hao la kukabiliana na wakala wa kupakia na kupakua mizigo wasio waaminifu, sasa litakuwa historia kwa kuwa ofisi ya Lubumbashi itakuwa na orodha ya wakala wanaokubalika na waaminifu.
Pia mienendo ya taarifa za mizigo itafanyika mjini humo na hivyo kuharakisha taratibu za mizigo bandarini hapo.
Kwa upande wake, Bw. Lumbu Useni wa kampuni ya Luwang SPRL alitoa wito kwa wafanyakazi kwenye ofisi hiyo ili kutimiza lengo lilikusudiwa.
“Wafanye kazi kwa bidii na akili zao zote ili lengo lililokusudiwa na nchi hizi lifikiwe na sisi tuweze kufaidika,” alifafanua.
Mizigo ya DRC inayopita katika bandari ya Dar es Salaam imekuwa ikiongezeka kwa asilimia takribani 24 kwa mwaka tangu mwaka 2004 ikiongezeka toka tani 155,611 hadi tani 1,117,249 mwaka 2013.
Nchi hiyo ni ya pili kwa kupitisha mizigo mingi katika bandari ya Dar es Salaam.  kwa mujibu wa takwimu zilizopo, mizigo ya DRC inachukua asilimia 25 ya mizigo yote ya nchi jirani inayopita katika bandari hiyo.
Mfanyabiashara mwingine, Bw. Mohamed Hassan Hammy, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Drill Tek ya mjini humo alisema Kongo ni soko kubwa hivyo Tanzania imefanya busara kubwa kufungua ofisi hiyo.
Bw. Hammy ambaye ni mtanzania alisema pamoja na kwamba kufungua ofisi hiyo ya TPA ni hatua kubwa, jumuiya ya wafanyabiashara mjini hapo wanaomba serikali kufungua ofisi ndogo ya ubalozi wa Tanzania Lubumbashi ili kuwasaidia katika mambo yao mbalimbali.
“Tunaipongeza serikali kufungua ofisi hii ya TPA lakini pia tunaiomba ifungue ubalozi mdogo hapa Lubumbashi ili kutusaidia sisi watanzania tunaoishi hapa,” alisema, na kuongeza kuwa kwa sasa wanalazimika kusafiri umbali wa kilometa 2,000 hadi mjini Kinshasa wanapohitaji huduma za ubalozi wa Tanzania.
“Kinshasa ni mbali sana na ni gharama kubwa,” alifafanua.
Awali, Waziri ya Uchukuzi wa jimbo la Katanga, Bw. Kahozi Sumba alisema ufunguzi wa ofisi hiyo sio tu utarahisisha na kuleta ufanisi katika kusafirisha mizigo ya wafanyabiashara wa Kongo wanaotumia bandari ya Dar es Salaam, bali pia utasaidia kuboresha maisha yao.
“Kurahisisha biashara ina maana ya kupata maendeleo na kuboresha maisha yetu, tunaishukuru sana serikali ya Tanzania kwa uamuzi huu,” alisema baada uzinduzi huo uliofanywa na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe.
Aliihimiza jumuia ya wafanyabiashara wa nchi hiyo kuthibitisha kuwa kweli walikuwa wanaihitaji ofisi hiyo kwa kuitumia kutatua matatizo yao.

“Thibitisheni kwa vitendo kuwa kweli mlikuwa mnaihitaji ofisi hii,” aliwaambia baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa katika tukio hilo la uzinduzi.   
 Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe (katikati) akisaini kitabu cha wageni katika ofisi mpya ndogo ya mawasiliano ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) mjini Lubumbashi, jimbo la Katanga hivi karibuni.  Wanaoshuhudia ni Waziri wa Uchukuzi wa Jimbo la Katanga, Bw. Kahozi Sumba (kushoto) na mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Bi. Zarina Madabida (kulia).

 Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe (wa pili kushoto) na Waziri wa Uchukuzi wa Jimbo la Katanga, Bw. Kahozi Sumba wakifuatilia jambo wakati wa uzinduzi wa ofisi ofisi ndogo ya mawasiliano ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) mjini Lubumbashi katika jimbo hilo hivi karibuni.  Wengine katika picha ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Bw. Peter Serukamba (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Eng. Madeni Kipande (kulia).

 Sehemu ya wafanyabiashara wa DRC Congo waliohudhuria uzinduzi wa ofisi ndogo ya mawasiliano ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) mjini Lubumbashi, jimbo la Katanga hivi karibuni.  Uzinduzi huo ulifanywa na Waziri Harrison Mwakyembe kusaidia wafanyabiashara wa nchi hiyo wanaotumia bandari ya Dar es Salaam.

 Sehemu ya wafanyabiashara wa DRC Congo waliohudhuria uzinduzi wa ofisi ndogo ya mawasiliano ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) mjini Lubumbashi, jimbo la Katanga hivi karibuni.  Uzinduzi huo ulifanywa na Waziri Harrison Mwakyembe kusaidia wafanyabiashara wa nchi hiyo wanaotumia bandari ya Dar es Salaam.


Sehemu ya wafanyabiashara wa DRC Congo waliohudhuria uzinduzi wa ofisi ndogo ya mawasiliano ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) mjini Lubumbashi

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 06, 2014

    Nchi yetu inaona mbali kama twiga, huu ni ushindani tusizubae.

    ReplyDelete
  2. AnonymousMay 06, 2014

    kWEMYE PICHA YA KWANZA HAPO JUU HIYO BENDERA SIO YA TZ

    ReplyDelete
  3. AnonymousMay 06, 2014

    Kuna haja sasa Wizara ya Mambo ya Nje kufungua Ubalozi Mdogo huko Lubumbashi ili kuzikamata fursa zote za kiuchumi. Pia benki kama CRDB,NMB na zingine zivuke mipaka, Lubumbashi kuna Watanzania wengi na biashara ni kubwa sana.

    ReplyDelete
  4. AnonymousMay 08, 2014

    Hii ni Kiboko ya 'Coalition of Willing' !

    Wao wamefungua Ofisi ya KPA (Kenya Ports Authority) kule Kigali-Rwanda kwenye uchumi ulio anguka baa ya vita ya Congo-DRC kuisha wakati sisi Tanzania Mabingwa tumefungua kule kwenye uchumi ulio imarika kwa ndugu yetu wa ukoo Joseph Kabila!

    Heko Tanzania!!!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...