Na: Hassan Hamad, OMKR.
Wakati Chama Cha
Wananchi CUF kikiingia katika uchaguzi Mkuu Taifa kuanzia kesho tarehe 23/06/2014,
Viongozi wakuu wa Chama hicho wamewataka wajumbe watakaokosa nafasi za uongozi
kutobabaika, na badala yake waendelee kukijenga chama hicho.
Akizungumza katika
hafla maalum ya kuagana na wajumbe wa Baraza Kuu pamoja na watendaji wengine wa
ngazi mbali mbali, Katibu Mkuu wa Chama hicho Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad,
amesema kila mwanachama ana wajibu wa msingi wa kukijenga chama bila kujali
wadhifa alionao.
“Wasiorudi kwenye
baraza kuu na ngazi nyengine yeyote ya uongozi bado wana mchango mkubwa wa
kukijenga chama chetu ili kiweze kushika dola mwaka 2015, na jukumu hilo limo
ndani ya katiba ya chama chetu”, alisisitiza Maalim Seif katika hafla hiyo
iliyofanyika nyumbani kwa Mwenyekiti wa Chama hicho Prof. Ibrahim Lipumba
katika eneo la Kunduchi Dar es Salaam.
Amewapongeza wajumbe
wa Baraza Kuu la Uongozi kwa mashirikiano waliyokuwa nayo katika kipindi chote
cha miezi 64, hali ambayo amesema imeleta mafanikio makubwa ndani ya chama
hicho.
Maalim Seif amesema
ndani ya kipindi hicho Chama pia kilikabiliwa na changamoto mbali mbali ambazo
hata hivyo kwa kutumia busara na hekima za viongozi waliweza kuzitatua.
Amewasisitiza wajumbe
watakaochaguwa kuendeleza umoja na mshikamano uliopo, ili kuweza kufikia
malengo waliyojiwekea ya kukamata hatamu za dola katika uchaguzi mkuu ujao.
Mapema akizungumza
katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa CUF Taifa Prof. Ibrahim Lipumba ambaye anakabiliwa
na upinzani katika uchaguzi huo, ameahidi kukubaliana na matokeo ya uchaguzi
huo, na iwapo atashindwa ataendelea kukiunga mkono chama hicho kwa kutoa kila
msaada unaostahiki kwa maendeleo ya chama.
“Mimi nikiangushwa
katika uchaguzi nitaendelea kuwa mwanachama na kutoa mchango wangu wote kwani
suala hili la kugombea nafasi ni haki ya kikatiba kwa wanachama wote” alieleza
Prof. Lipumba na kuongeza,
“Nilikuwa mwanachama
wa kawaida kwa kipindi kirefu ndipo ikafika wakati chama kikaniteua kugombea na
kuchaguliwa Mwenyekiti hadi leo, kwa hivyo haki hii anaweza kuwa nayo
mwanachama yeyote”, aliweka bayana Prof. Lipumba.
Jumla ya wagombea
watatu wamejitokeza kugombea nafasi ya Uenyekiti Taifa akiwemo Mwenyekiti wa
sasa Prof. Ibrahim Haruna Lipumba.Wagombea wengine wa
nafasi hiyo ya Mwenyekiti Taifa ni M’bezi
Adam Bakar kutoka Temeke Dar es Salaam na Chifu Lutalosa Yemba kutoka
Shinyanga.
Nafasi ya Makamu
Mwenyekiti ina mgombea mmoja ambaye ni Mhe. Juma Duni Haji na Ukatibu Mkuu ni
Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad.
Aidha Prof. Lipumba
ametumia fursa hiyo kuwaeleza wajumbe kuwa bado chama hicho kinaendelea na
juhudi zake ili kuweza kupata katiba ya wananchi, katika mchakato wa katiba
mpya unaotarajiwa kuendelea tena mwezi Ogasti, 2014.
Katika
hatua nyengine Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Mhe.
Machano Khamis Ali, amesema ameamua kwa hiari yake kutogombea tena nafasi hiyo
kutokana na sababu mbali mbali zikiwemo sababu za kiafya.
“Mimi nimeamua kuwa
mfano ndani ya chama chetu, sitaki kuwa king’ang’anizi wa nafasi hii, nimeona
nisigombee tena nafasi hii kutokana na sababu nilizozieleza, lakini nakuahidini
kwamba sitokwenda chama chengine na nitaendelea kutoa mchango wangu wote katika
kukijenga na kukiendeleza Chama chetu”, aliweka wazi Mhe. Machano.
Mapema akitoa neno la
shukrani kwa niaba ya wajumbe wa Baraza Kuu na watendaji wengine wa Chama hicho, Bibi Najma Khalfan amewatanabahisha viongozi
na wanachama kuungana ili waweze kupata ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka
2015.
Ni ukweli uliokosa shaka kwamba siku Maalim akiamua kutogombea nafasi yoyote ndani ya CUF basi ndio kusambaratika kwa chama hicho. Pia kwa nafasi yoyote atakayoamua kugombea basi hakutakuwa na atakayejichomoza kupinzana naye na endapo atatokea wa kuthubutu huyo uanachama wake itakuwa kauweka rehani mwenyewe. Usifanye mchezo na Maalim, huyo ndio kila kitu ndani ya chama!!
ReplyDelete