Wateja wa huduma ya M-pesa wamehakikishiwa usalama wa fedha zao wakati ambapo huduma hiyo ikiwa imerejea kwa asilimia mia moja baada ya kukosekana kufuatia tatizo la kiufundi lililojitokeza mwishoni mwa wiki.

Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania Rene Meza amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo kuwa huduma hiyo kwa sasa iko imara na kuchukua nafasi hiyo kuwoamba radhi wateja kwa usumbufu walioupata wakati huduma hiyo ilipokosekana.

“Napenda kuwaomba radhi wateja wetu ambao wamekuwa na wakati mgumu kupata huduma ya M-pesa katika siku chache zilizopita. Tunatambua umuhimu wa huduma hii kwao. Hali iliyojitokeza ilikuwa nje ya uwezo wetu na kamwe hatukulitarajia.”Alisema Meza

Meza amesema kilichotokea kwenye mfumo wa M-pesa ni changamoto ambayo mfumo wowote unaotumia teknolojia unaweza kukumbana nayo bila kutarajia lakini jambo la muhimu ni kwa jinsi gani mtoa huduma anavyoweza kujipanga kuitatua kwa uharaka kudhibiti madhara makubwa zaidi kwa wateja.

“Unapokuwa katika suala la teknolojia chochote kinaweza kutokea ni kama vile inavyoweza kutokea kompyuta kukataa kuwaka lakini cha msingi ni kwa uharaka gani unaweza kudhibiti tatizo na kufikia ufumbuzi, hilo ndilo tulilolifanya na kwa sasa tunayo furaha kwamba wateja wetu wanaendelea kupata huduma.”Aliongeza

Kuhusu usalama wa fedha Meza amewahakikishia wateja wa Vodacom na wabia wake wote wanaoutumia huduma hiyo kwamba fedha zote zipo salama na zinalindwa kwani kilichotokea ni wateja kushindwa kuipata huduma hiyo kwenye menyu za simu zao  za mkononi na sio tatizo kwenye mfumo mzima wa M-pesa.

‘Fedha zote zipo salama na zinalindwa. Kama wakati tatizo lilipotokea mteja alikuwa na Sh 1/- au Sh 100/- ,Milioni basi ni kiwango hichohicho atakuwa amekikuta kwenye akaanti yake ya M-pesa au hata ya M-pawa mara baada ya huduma kurejea.”Alifafanua Meza

Meza amewashukuru wateja wa M-pesa kwa uvumilivu na ustahamilivu wao wakati timu ya watalaamu wa ndani na nje ya nchi walipokuwa katika juhudi  za kutafuta uvumbuzi wa tatizo lililojitokeza.

“Wateja wetu wamekuwa wavumilivu na wameendelea kuitumia kupitia mawakala zaidi ya 70,000 walioko nchi nzima. Hili unaweza ukaliona kupitia namna ambavyo wateja walivyoendelea kuitumia M-pesa mara baada ya kurejea, tunawashukuru sana na tunaendelea kuwaahidi huduma bora.”Aliongeza

“Hakuna madhara ya kibiashara kwetu, ila kutokana na M-pesa kuwa tegemezi kwa mamilioni ya watanzania katika maisha yao ya kila siku ikiwa ndio huduma kinara ya fedha kwa njia ya simu za mkononi, ni wazi kwamba imeleta usumbufu mkubwa kwa watumiaji.”

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...