Na Sultani Kipingo 
wa Globu ya Jamii
Siku ya tatu tu tokea michuano ya kombe la Dunia ianze nchini Brazil, tayari mabingwa watetezi Spain wanakuta kombe hilo linateleza mikononi mwao. 
Japokuwa miaka minne iliyopita walipoteza mchezo wao kwa kwanza dhidi ya Switzerland huko Afrika ya Kusini, lakini hiyo haiwezi kulinganishwa na kilichotokea uwanja wa Fonte Nova katika mji wa Salvador ulio Kaskazini-Mashariki ya Brazil usiku wa kuamkia leo baada ya kuchwapwa bao 5-1 na Holland.
Hilo ni pigo kubwa kwa Spain kupata tokea mwaka 1963 walipochabangwa na Scotland, ila safari hii aibu yake ni maradufu kwa vijana hao wa kocha Vicente del Bosque. Ni sawa na matokeo ya ndondi pale Tyson alipopigwa na kuvuliwa ubingwa Las Vegas. Wadadisi wanasema ni timu chache zinaweza kuzinduka baada ya kipigo kama hicho. Sasa wanasubiri kuona Spain itakuwaje.

Kimchezo Holland ngoma iliwakubali. Walikuwa wakihaha kila pembe ya uwanja kusaka magoli, huku nyota wao tishio  Robin van Persie na  Arjen Robben wakiwatoa raha Spain  kila sekunde. Matokeo yakaja kama ilivyokuwa mwaka 1990 wakati Cameroon walipoichapa Argentina, ama Ufaransa kufungwa na Senegal mjini Seoul miaka 12 baadaye.

Ukifikiria sana unajikuta unakubali kwamba kipigo cha 5-1 ni janga kwa Spain, hasa ukizingatia ilianza kuongoza kwa bao 1-0 na kuwa mbele kabla ya mapumziko. Saa moja baadaye Spain wakajikuta wanasujudu kwa mabao hayo ambayo kama si kipa wao Iker Casillas kuokoa mikwaju mingine kibao ingekuwa 7-1 ama hata 8-1. Kitu pekee kilichowaokoa isiwe hivyo ni kipyenga cha mwisho…

Ngoma ilianza kuwa tamu pale Spain ilipojipatia bao la kwanza kwa njia ya penati iliyopigwa na Xabi Alonso. Dakika moja kabla ya ya mapumziko, ndipo Robben Van Persie  akaanzisha kalamu ya magoli pale aliposawazisha kwa goli tamu la kichwa cha kuchupa (pichani) akiwa mita 30, kabla ya kuongeza lingine kwa kumpita Gerard Pique.  Stefan de Vrij akaweka kimiani bao la 3, kabla Van Parsie hajautumia kwa manufaa yake uzembe wa kipa Iker Casillas na kufunga la nne na la tano. 
Katika mchezo mwingine Chile imeifunga Australia bao 3-1 katika uwanja wa Pantanal Cuiba. 
Leo timu ingine ya Afrika, Ivory Coast, inatupa karata yake ya kwanza kwa kucheza na Japan katika uwanja wa Pernambuco mjini Recife, wakati Enland inakipiga na Italy katika mchezo mwingine wa kukata na shoka katika uwanja wa Amazonia mjini Manaus.
Leo pia Columbia watacheza na Greece, wakati Uruguay itapambana na Costa Rica. Kuona muda wa kuanza michezo hiyo angalia ratiba hapo juu.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 14, 2014

    Kichapo cha kutisha lakini dont write the obituary yet, dont write them off.Hata hivyo kwangu man of the match must be Iker Casillais.Kama angeshindwa kuzuia mikwaju mingi mingine wengelala kwa mabao tisa.Kisha kumbuka kama angemwangusha Van Persie,angepigwa red card na Spain wengecheza dakika ishirini za mwisho bila kipa wao.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...