Na Allan Ntana, Sikonge
MWENYEKITI wa halmashauri ya wilaya ya Sikonge mkoani Tabora Robert
Kamoga amepongeza jitihada zinazofanywa na mradi wa PROSPER katika
kutokomeza utumikishwaji watoto katika shughuli za kilimo huku akisifu
utaratibu wa kurudishwa shule watoto wote waliokosa nafasi hiyo.
Kamoga ametoa pongezi hizo alipokuwa akizungumza na mamia ya wananchi
waliojitokeza katika maadhimisho ya siku ya kupinga utumikishwaji
watoto iliyofanyika kimkoa katika kijiji cha Udongo kata ya Ipole
wilaya ya Sikonge mkoani Tabora.
Alisema mradi huu unastahili kupongezwa kwa sababu mkoa wa Tabora ni
miongoni mwa mikoa 5 inayoongoza kwa umaskini hapa nchini na asilimia
kubwa ya wananchi wake ni maskini hali inayochangia watoto wengi
kutumikishwa katika kazi ngumu kwa ujira mdogo.
Mradi huu ni mkombozi kwa watoto wadogo kwa sababu wazazi wengi
walikuwa hawawapeleki shule kwa kisingizio cha umaskini na badala yake
wanawapeleka shambani wakawasaidie kulima tumbaku au kuchunga ng’ombe,
alisema.
Kamoga aliongeza kuwa utumikishwaji watoto ni hatari sana katika
ustawi wao kwa sababu huwakosesha fursa mbalimbali katika makuzi yao
ikiwemo haki ya kupata elimu na malezi bora. "Wataalamu wanasema ukimnyima mtoto haki zake anaathirika kisaikolojia
mpaka ukubwani mwake na watoto ndio taifa la leo na kesho, hivyo
wanapaswa kulindwa, kutunzwa na kupendwa, kwa kufanya hivyo tutakuwa
tunajenga taifa kuanzia ngazi ya familia mpaka taifa, alifafanua.
Aidha alisema sheria ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009 kifungu cha 78 (1)
inakataza mtu yeyote kuajiri au kutumikisha watoto katika shughuli
yoyote ile inayowaadhili watoto hao, hivyo kumtumikisha ni kwenda
kinyume na sheria za nchi anapaswa kushitakiwa mara moja.
Kamoga alisema PROSPER imefanikiwa kuwarudisha shuleni watoto wengi
sana waliokosa elimu katika wilaya za Sikonge na Urambo na
kuwagharamiwa masomo yao kuanzia darasa la kwanza mpaka la saba huku
vikundi mbalimbali vya vijana na akina mama vikipewa mafunzo ya
ujasiriamali, kilimo, ufugaji na mikopo kwa lengo la kuwawezesha
kiuchumi.
Mradi huu umefanya kazi nzuri sana katika vijiji 20 vilivyoko katika
wilaya hizo, Mkurugenzi (Bahati Nzunda) naomba uangalie uwezekano wa
kupanua huduma hii katika vijiji vingine kwani wapo watoto wengi sana
walioathiriwa na utumikishwaji huu, aliongeza.
Ili kudhibiti vitendo hivyo, Kamoga aliagiza waalimu wakuu wa shule
zote za msingi katika wilaya hiyo kuhakikisha wanafuatilia mahudhurio
ya watoto shuleni ili kubaini watoto wasiofika shule ili wazazi wao
wakamatwe mara moja na kutozwa faini.
Sambamba na hilo aliagiza watendaji wote wa halmashauri kuanzia ngazi
ya vijiji na kata kuwachukulia hatua kali watu wote watakaobainika
kujihusisha na vitendo vya utumikishwaji watoto katika maeneo yao huku
akiomba asasi zingine kuunga mkono jitihada hizo.
BW.ROBERT KAMOGA (WA KWANZA KULIA) MWENYEKITI WA HALMASHAURI SIKONGE AKIWA NA MKURUGENZI WA MRADI WA PROSPER BAHATI NZUNDA (WA KWANZA KUSHOTO) AKIFUATIWA NA DR MTIBA NA MWENYEKITI HALMASHAURI YA WILAYA URAMBO ADAM MALUNKWI.JPG
ROBERT KAMOGA AKIHUTUBIA UMATI WA WANANCHI WA VIJIJI VYA UDONGO NA MAKAZI KATIKA KATA YA IPOLE WILAYANI SIKONGE MKOANI TABORA KATIKA MAADHISHO YA SIKU YA KUPINGA UTUMIKISHWAJI WATOTO KATIKA MASHAMBA YA TUMBAKU.JPG
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...