Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki leo wameendelea na mchakato wao wa kumuondoa spika Mhe. Dkt. Margaret Nantongo Zziwa, baada mahakama ya Afrika ya Mashariki ( East Africa court of Justice) jijini Arusha kukataa kuzuia zoezi la kumuondosha katika kiti hicho.
Ripota wetu anataarifu kutoka huko kuwa bunge liliahirishwa kukutana tena leo asubuhi baada ya suluhu kukosekana. "Hili linazuia mchakato mzima wa bajeti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kusomwa", Mbunge mmoja alisikika kusema.
Habari kutoka ndani ya Bunge hilo zinasema baadhi ya Wabunge wa Tanzania katika bunge hilo wameondoa saini zao na kusema kuwa wao hawaungi mkono kumuondoa Spika huyo madarakani, jambo ambalo limeleta zongo zaidi bungeni leo.
Wabunge walioondoa saini ni Mh Maryam Ussi Yahya, Mh Adam Kimbisa na Mh Shyrose Bhanji. Wabunge kutoka Tanzania - Mh Abdullah Mwinyi na Mh Nderakindo Kessy, inasemekana hawakutana kuondoa saini zao.
Tayari barua ya kuomba saini za Wabunge wa Tanzania ziondolewe katika orodha za wanaopinga imeshaandaliwa na kupelekwa kunakohusika.
Bunge hilo lililoanza Mkutano wake wa Tano mwezi Machi 26, mwaka huu, kwa ufunguzi uliofanywa na Mwenyekiti wa EAC ambaye pia ni Rais wa Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta, lilipangwa kumaliza shughuli zake Aprili 4.
Lakini haikuwa hivyo. Kiti cha Spika kiliwaka moto na mwishowe alikipooza kiti kwa kuahirisha Bunge kwa muda usiojulikana. Spika alitumia kifungu cha kanuni ya 82(2) ya kanuni za mwenendo wa Bunge hilo kufafanua kanuni.
Inasemekana kwamba Wabunge 36 kati ya 44 hawamtaki. wakimtupia shutuma za kuwagawa wabunge na kupoteza imani kwao.Wanamtuhumu kwa kuliongoza bunge hilo bila kuwa na viwango na ujuzi mdogo wa uongozi, matumizi mabovu ya ofisi, dharau kwa wabunge wenzake inayoambatana na matumizi ya lugha chafu na ubabe kwenye vyombo vya habari dhidi ya wabunge na hivyo kuvunja heshima ya wabunge hao mbele ya jamii.
Mazingira ya kuwaka moto kiti yalijitokeza Aprili Mosi mwaka huu, majira ya saa 10 jioni baada ya hoja ya kumuondoa kwenye kiti kuwasilishwa bungeni na Mbunge wa Kenya, Peter Mathuki.
Dk Zziwa anasema tuhuma dhidi yake zinatokana na yeye kugoma kupandisha mishahara yao, na kwamba baadhi ya wabunge walikuwa wakidai nyongeza ya asilimia 100 ambayo ingeongeza maradufu mishahara yao hadi kufikia dola za Marekani 10,000 (Sh 16.25 milioni.
Alisema ameshindwa kukubaliana nao ndiyo maana sasa wamemtafuta mbunge mwingine ambaye ameahidi kuwatekelezea nyongeza hiyo hadi asilimia 200 kama watamchagua kuwa Spika.
Kuhusu suala la uwezo wake kiutendaji na madai ya kufanya kazi kwa kiburi, alisema inatokana na hatua yake ya kulivalia njuga suala la wabunge kupokea posho na baadaye kutohudhuria vikao.
wabunge wa EALA walimchagua Dk Zziwa kuwa Spika wao kwa kipindi cha miaka mitano, Katika ukumbi wa bunge wa jengo la Mikutano la Kimataifa la Arusha (AICC), Juni 5, mwaka juzi katika Uchaguzi uliojaa ushindani mkubwa kati yake na mpinzani wake, Dora Byamukama.
Wagombea wote hao ni wanasheria wakitokea Uganda kwa kuwa awamu hii ni zamu ya nchi hiyo kutoa Spika baada ya Tanzania na Kenya kumaliza zamu zao. Iwapo wabunge watafanikiwa kumng’oa Dk Zziwa nafasi hiyo itaendelea kubakia Uganda.
Inasemekana uchaguzi huo ulizua makundi ya kampeni na wapambe wao. Matokeo ya uchaguzi yalipotangazwa, mpinzani wake alikataa kumpa mkono wa kumpongeza, hawakuweza kukumbatiana kama ishara ya kukubali kushindwa na kushinda na kuahidi kufanya kazi kwa pamoja. Aliendelea kununa na inawezakana mpaka sasa bado amenuna wakiwamo wapambe wake.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...