Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe akimpongeza mmoja wa askari wa bandari ya Dar es Salaam, Cornel Kufahaidhuru katika hafla fupi ya kuwazawadia askari 18 wa mamlaka ya bandari Tanzania (TPA) kwa kazi nzuri ya kuimarisha ulinzi katika bandari hiyo jana jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Serikali imetoa sifa kwa kitengo cha usalama cha Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa
kuimarisha ulinzi katika bandari na hivyo kuchangia kuifanya bandari hiyo kuongeza ufanisi.
Akitoa zawadi kwa askari wa mamlaka hiyo walioonyesha moyo wa kujitolea na ufanisi jana
jijini Dar es Salaam, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe alisema kazi yao nzuri
imeongeza usalama na kuvutia zaidi wateja.
“Ninawasifu kwa kazi nzuri mnayofanya,” alisema.
Alielezea kuwa kujitolea kwao na ueledi wao umesaidia kuokoa mamilioni ya shilingi
ambayo yangepotea kwa wizi katika bandari hiyo.
Kutokana na kazi yao nzuri, Waziri alisema, sasa nchi mbalimbali zinaanza kuonyesha nia ya
kutumia zaidi bandari hiyo kupitisha mizigo yao.
Akitoa mfano, Waziri huyo alisema ujumbe wa maafisa wa serikali ya Kongo na
wafanyabiashara toka jimbo la Katanga waliotembelea bandari hiyo wiki hii ni ishara kubwa
kuwa sasa bandari inaanza kurudisha heshima yake.
Baadhi ya zawadi zilizotolewa ni pamoja na pikipiki, televisheni, simu za mkononi, pesa
taslim na kompyuta mpakato.
“Natoa shukrani za dhati kwa wadau wote waliochangia zawadi hizi,” alisema Waziri.
Takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya meli zinazotumia bandari hiyo imeongezeka kutoka
1,236 mwaka 2011/12 hadi kufikia meli 1,301 mwaka 2012/13.
Kwa upande wa shehena mwaka 2012/13 bandari ilihudumia jumla ya tani milioni 12.5
ikilinganishwa na tani milioni 10.9 mwaka 2011/12, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 15.
Pia kwa mwaka wa 2012/13 bandari ilizihudumia nchi zinazotumia bandari hiyo shehena ya
tani milioni nne ambayo ni sawa na asilimia 32 ya shehena yote.
Mwaka 2012/13 wastani wa Tshs bilioni 371.7 zilikusanywa, sawa na ongezeko la asilimia
14.3 ukilinganisha na Tsh. bilioni 325.3 mwaka 2011/12.
Matukio ya uhalifu na wizi yamepungua kutoka matukio 21 mwaka 2011 hadi matukio 7
mwaka 2012, na kufikia matukio 3 mwaka 2013.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Madeni Kipande alisema
juhudi za polisi hao wa mamlaka zimezaa matunda.
“Ninatoa shukrani zangu kwa kitengo cha ulinzi na wafanyakazi wote kwa juhudi
wanazoonyesha,” alisema.
Alimshukuru Waziri Mwakyembe kwa kuweka swala la usalama katika vipaumbele vya
wizara. TPA iko chini ya wizara ya Uchukuzi.
“Mamlaka itaendelea kutambua wafanyakazi bora na kuwapatia motisha,” alisema Kipande.
Mkuu wa Kitengo cha usalama cha TPA, Bw. Lazaro Twanga alisema kutambuliwa huko
kumewapatia motisha na nguvu ya kufanya kazi nzuri zaidi.
Hata hivyo, alisema swala la kuhakikisha usalama katika bandari hiyo ni la wafanyakazi wote
na hivyo akataka ushirikiano wao.
“Tushirikiane wote kuhakikisha bandari yetu inakuwa imara na yenye kuleta ushindani kwa
faida ya taifa letu,” alisema.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...