Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeikataa rufani ya Michael Richard Wambura (pichani) kupinga kuenguliwa kugombea urais katika uchaguzi wa klabu ya Simba unaotarajiwa kufanyika baadaye mwezi huu.
Wambura aliwasilisha rufani yake mbele ya Kamati hiyo iliyokutana leo (Juni 19 mwaka huu) jijini Dar es Salaam chini ya Kaimu Mwenyekiti Wakili Mwita Waissaka kupinga uamuzi wa kumwengua katika kinyang’anyiro hicho uliofanywa na Kamati ya Uchaguzi ya Simba kwa kufanya kampeni kabla ya muda uliopangwa.
Baada ya kupitia vielelezo, kanuni na sheria, Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF imeridhika kuwa mrufani (Michael Wambura) alifanya kampeni kabla ya muda kinyume na Ibara ya 6(1)(a) na (g), Ibara ya 6(1)(l) pamoja na Ibara ya 14(3) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF toleo la 2013.
Kwa mujibu wa ibara hizo, Kamati ya Uchaguzi ya Simba inayo mamlaka ya kumwengua (disqualify) mgombea anayefanya kampeni ama kukiuka maagizo halali ya Kamati ya Uchaguzi.
Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF imeziagiza kamati zote za uchaguzi za wanachama wa TFF kufuata kanuni za uchaguzi kama zilivyoainishwa katika Katiba zao ili kuepusha rufani za mara kwa mara.
Uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF umezingatia Katiba ya TFF pamoja na kanuni zake, na pia Katiba ya Simba.
Kosa lake lilikuwa wazi na adhabu yake inajulikana, hii itakuwa fundisho kwa watu wengine. Alikuwa anachelewesha mahakama tu kwa kufanya ujanja ujanja.
ReplyDeleteHivi pale kila unapoenda wanakukataa kwa nini mtu hujiulizi? Ningekuwa mimi hata kama ni mpenzi wa kiasi gani ningeachana na michezo kwa muda wakati natafakari kujua wapi tatizo lipo. Niking'amua shida ni nini najirekebisha ndiyo nirudi tena huko kama muda utaruhusu. Haiwezekani kuwa kila anaponusa huyu jamaa ni fitina, lazima yeye ndiyo tatizo na ndiyo maana wanamkataa. Jichunguze ili ujirekebishe kaka, leo kwenye michezo wamekukataa kesho itakuwa mahali pengine
ReplyDeleteMichael Wambura anaonekana kuwa mvurugaji tu. Kama anataka uongozi wa Simba kwa dhati, au uongozi wa TFF kwa dhati kabisa, basi angetafuta wanasheria wamshauri namna ya kumaliza matatizo yanayomsumbua kila wakati wa uchaguzi. haiwezekani kila uchaguzi unapofika wanam-disqualify kwa tatizo hilo hilo na yeye hilishughulikii anasubiri uchaguzi mwingine! huu ni upotezaji wa muda wa watu na rasilimali!
ReplyDelete