Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeikataa rufani ya  Michael Richard Wambura (pichani) kupinga kuenguliwa kugombea urais katika uchaguzi wa klabu ya Simba unaotarajiwa kufanyika baadaye mwezi huu.


Wambura aliwasilisha rufani yake mbele ya Kamati hiyo iliyokutana leo (Juni 19 mwaka huu) jijini Dar es Salaam chini ya Kaimu Mwenyekiti Wakili Mwita Waissaka kupinga uamuzi wa kumwengua katika kinyang’anyiro hicho uliofanywa na Kamati ya Uchaguzi ya Simba kwa kufanya kampeni kabla ya muda uliopangwa.

Baada ya kupitia vielelezo, kanuni na sheria, Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF imeridhika kuwa mrufani (Michael Wambura) alifanya kampeni kabla ya muda kinyume na Ibara ya 6(1)(a) na (g), Ibara ya 6(1)(l) pamoja na Ibara ya 14(3) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF toleo la 2013.

Kwa mujibu wa ibara hizo, Kamati ya Uchaguzi ya Simba inayo mamlaka ya kumwengua (disqualify) mgombea anayefanya kampeni ama kukiuka maagizo halali ya Kamati ya Uchaguzi.

Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF imeziagiza kamati zote za uchaguzi za wanachama wa TFF kufuata kanuni za uchaguzi kama zilivyoainishwa katika Katiba zao ili kuepusha rufani za mara kwa mara.


Uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF umezingatia Katiba ya TFF pamoja na kanuni zake, na pia Katiba ya Simba.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 20, 2014

    Kosa lake lilikuwa wazi na adhabu yake inajulikana, hii itakuwa fundisho kwa watu wengine. Alikuwa anachelewesha mahakama tu kwa kufanya ujanja ujanja.

    ReplyDelete
  2. AnonymousJune 20, 2014

    Hivi pale kila unapoenda wanakukataa kwa nini mtu hujiulizi? Ningekuwa mimi hata kama ni mpenzi wa kiasi gani ningeachana na michezo kwa muda wakati natafakari kujua wapi tatizo lipo. Niking'amua shida ni nini najirekebisha ndiyo nirudi tena huko kama muda utaruhusu. Haiwezekani kuwa kila anaponusa huyu jamaa ni fitina, lazima yeye ndiyo tatizo na ndiyo maana wanamkataa. Jichunguze ili ujirekebishe kaka, leo kwenye michezo wamekukataa kesho itakuwa mahali pengine

    ReplyDelete
  3. AnonymousJune 20, 2014

    Michael Wambura anaonekana kuwa mvurugaji tu. Kama anataka uongozi wa Simba kwa dhati, au uongozi wa TFF kwa dhati kabisa, basi angetafuta wanasheria wamshauri namna ya kumaliza matatizo yanayomsumbua kila wakati wa uchaguzi. haiwezekani kila uchaguzi unapofika wanam-disqualify kwa tatizo hilo hilo na yeye hilishughulikii anasubiri uchaguzi mwingine! huu ni upotezaji wa muda wa watu na rasilimali!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...