Katika
kile kinachoonekana kama nia thabiti ya kuzuia tatizo sugu la msongamano wa
magari katika jiji la Dar es Salaam, utaratibu mpya wa kudhibiti changamoto
hiyo uko mbioni kutangazwa.
Mara
utakapotangazwa, kila anayehusika hasa madereva katika jiji hilo kubwa la
biashara watatakiwa kuuheshimu na kuufuata.
Akitangaza
utaratibu huo mpya unaotarajiwa kuanza hivi karibuni, Afisa Mkuu Mtendaji wa
Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka
(DART), Bi. Asteria Mlambo hatua hiyo inalenga kuondoa msongamano, kuimarisha
usalama na usafi katika njia zote zilizokamilika za mradi wa mabasi hayo.
Mradi
unaoendelea wa mabasi yaendayo haraka katika jiji la Dar es Salaam, unalenga kuimarisha
huduma za usafiri na kuwa za kisasa zaidi pamoja na kupunguza msongamano ambao
umekuwepo kwa kipindi kirefu sasa.
Katika
awamu hii ya kwanza mradi huo unahusisha ujenzi wa barabara maalum ya umbali wa
kilometa 20.9 kutoka Kimara hadi Kivukoni; barabara ya Msimbazi kuanzia Faya
hadi eneo la Kariakoo-Gerezani na sehemu ya barabara ya Kawawa kuanzia Magomeni
hadi njia panda ya Morocco.
“Tunatarajia
utaratibu huu kuanza hivi karibuni,” Bi. Mlambo aliwaambia waandishi wa habari.
Akizungumzia
mahitaji ya utaratibu huo mpya alisema gari zote zitakazotumia njia katika
mfumo wa njia hizo mpya hazitatakiwa kuzidi mwendo wa kilometa 50 kwa saa hasa
katika barabara ya Morogoro ambapo mradi huo unakaribia kukamilika.
Akielezea
zaidi alisema magari hasa daladala hazitaruhusiwa kusimama njiani na pia
itakuwa marufuku kufanya biashara ndogondogo au biashara ya aina yoyote katika
maeneo ya njia hizo.
“Kwa
sasa tunaangalia maeneo ya muda ambayo daladala zitaruhusiwa kusimama,” alisema
na kuongeza kuwa taratibu zote zimekamilika na kuwa polisi wataanza kuhakikisha
kuwa utaratibu huo unafuatwa hivi karibuni.
Kwa
mujibu wa Afisa huyo wa DART, kupaki magari au kufanya biashara katika maeneo
ya waenda kwa miguu haitaruhusiwa na watakaokiuka watakumbana na adhabu kali
kwa mujibu wa taratibu.
Pamekuwa
na mazoea ya madereva wa bajaji na pikipiki kupaki vyombo vyao katika njia za
watembea kwa miguu.“Napenda pia kuwataarifu wafanyabiashara
kuacha kupaki magari ya mizigo katika njia kuu na kupakua au kupakia mizigo,”
alisisitiza.
Aliongeza kuwa itakuwa marufuku pia kupaki
magari katika njia za pembeni na wala pikipiki hazitaruhusiwa kupita katika
njia za waenda kwa miguu.
“Makosa yatahusisha adhabu kali na faini ya
pesa taslimu,” alisema.
Utaratibu huo utasimamiwa na kufuatiliwa na
vyombo mbalimbali kama DART, askari wa usalama barabarani, Mamlaka ya Usafiri
wa majini na nchi kavu (SUMATRA) pamoja na TANROADS.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...