KAMPUNI ya Haak Neel Production kwa kushirikiana
na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), imezindua rasmi
Siku ya Msanii Tanzania itakayoenda sambamba na utoaji
tuzo kwa kwa wasanii na wadau wanaotoa mchango katika
sanaa ili kuenzi, kuhamasisha, kukuza na kuendeleza vipaji
vyao.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika Jumamosi
usiku katika Hoteli ya Sea Cliff, jijini Dar es Salaam,
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk.
Fenella Mukanagara, alisema Siku ya Msanii ni programu
iliyobuniwa na Basata mwaka 2008 lakini ilishindikana
kutekelezeka kutokana na ufinyu wa bajeti na kukosekana
mtu wa kuendesha mradi huo ambaye angeweza kuingia
ubia na Basata kama ilivyo kwa Tuzo za Muziki Tanzania.
“Nichukue fursa hii kuwapongeza Kampuni ya Haak
Neel Production pamoja na Basata kwa kubuni na
kufanikisha uzinduzi wa Siku ya Msanii, lakini
program hii itatuwezesha kuungana na wenzetu duniani
kuadhimisha ‘Siku ya Kimataifa ya Msanii’ ambayo
huadhimishwa kila Oktoba 25,” alisema.
Alisema Wizara inataka wasanii kujituma na kuzalisha kazi
bora zitakazotambulika ndani na nje, kutokana na kuwepo
Siku ya Msanii.
Alisema amefurahishwa na fursa ambazo zimeelezwa
kuwepo katika Siku ya Msanii kama semina, uwepo wa
tuzo, ambazo zitaonyesha utambuzi wa kazi za wasanii.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Haak Neel
Production, Emmanuel Mahendeka, alisema Siku ya Msanii
ni fursa nzuri kwa wasanii kuona na kujifunza kutoka kwa
wenzao na hivyo kuboresha kazi zao na Taifa kwa ujumla.
“Uhai wa sanaa yoyote inategemea kwa kiasi kikubwa
uwezo wa kurithishana kutoka kizazi hadi kizazi, ni
matumaini yangu Siku ya Msanii itasaidia sana kujenga
misingi imara na endelevu ya kurithisha sanaa katika jamii
zetu,” alisema.
Naye Kaimu Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey
Mungereza, alisema baraza hilo limekuwa likibuni miradi
mbalimbali kwa lengo la kuleta maendeleo ya sanii nchini
na kushirikiana sekta binafsi katika kuendeleza sanaa na
utamaduni na ndio maana wameshirikiana na Haak Neel
Production ili kuendeleza sanaa.
Tuzo zitakazotolewa ni Sinema bora yenye ubunifu halisia
na vionjo vya Kitanzania, kikundi bora cha sanaa za
maonyesho kinachochipukia, Mpigaji mahiri wa ala za
asili za muziki , Mbunifu wa mitindo ya mavazi yenye
vionjo vya Kitanzania, Msanii chipukizi anayeibukia,
Msanii aliyetoa mchango mkubwa katika jamii na Msanii
aliyetumia maisha yake vkatika sanaa.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, akipiga Gitaa kuashiria uzinduzi wa siku ya Msanii katika hafla iliyofanyika kwenye hoteli ya Sea Cliff Dar es Salaam.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk Fenella Mukangara akipokea zawadi ya picha aliyochorwa na msanii chipukizi, Meddy Jumanne wakati uzinduzi wa sherehe ya Siku ya Msanii uliofanyika mjini Dar es Salaam.
Meneja wa Masoko wa Siku ya Msanii, Catherine Metili (kulia) akiwa na ofisa Masoko wa Mradi, Veronica Martin (kushoto) wakiangalia kitabu cha wageni wakati wa uzinduzi wa Siku ya Msanii.
Mkurugenzi wa Utamaduni, Profesa Hermas Mwansoko akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Sihaba Juma wakifuatilia tukio la Siku ya Msanii.
Wageni walialikwa wakimesimama kutoa heshima kwa wasanii mbalimbali waliofariki katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita.
Mkurugenzi wa Haak Neel Production, Sebastian Mahendeka akizungumza wakati wa uzinduzi wa Siku ya Msanii.
Burudani ya Ngoma ya Asili.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...