Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi)
Katibu na Mshauri Mkuu wa Sheria wa Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL) na Pan Africa Power Solutions (T) Ltd, Joseph Mwakandege akizungumza na waandishi wa habari kuhusu sakata la ununuzi wa IPTL. Kushoto ni Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya IPTL na PAP, Harbinder Singh Sethi.
  Habari na Mwene Said 
wa Blogu ya Jamii. 
 KAMPUNI ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania (IPTL), imewasilisha maombi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam ya kutoa zuio la muda kwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) la kutoendelea kutangaza maneno ya kashfa juu yake. 
Imeiomba mahakama hiyo kutoa zuio hilo, hadi shauri la msingi walilolifungua mahakamani hapo dhidi ya mbunge huyo kwa kuwatuhumu kuchota fedha katika akaunti ya Escow isivyo halali litakapoamriwa. 
IPTL kwa kushirikiana na kampuni ya Pan African Power Solutions (T) Limited (PAP) na Mtendaji Mkuu wa kampuni hizo, Harbinder Sign Seth, wamewasilisha maombi hayo mahakamani hapo chini ya hati ya kiapo cha dharura na yameungwa mkono na Seth.
Maombi hayo namba 306 ya mwaka huu, yalitajwa mahakamani hapo Alhamisi iliyopita, mbele ya Jaji Rose Teemba, ambapo aliyaahirisha hadi Agosti 28, mwaka huu, kwa kutajwa. 
 Kwa mujibu wa hati ya maombi hayo, wadai hao kwa kupitia wakili wao Augustine Kusalika, wanaiomba mahakama hiyo itoe zuio la muda kwa Kafulila kwa kutoendelea kutangaza maneno ya kashfa kwa IPTL, PAP na Seth hadi shauri lao la msingi litakapoamuriwa. 
 Pia, wanaiomba mahakama kutoa zuio la muda kwa Kafulila kutoendelea kutangaza maneno ya kashfa kwa IPTL na PAP na aamuriwe kulipa gharama za maombi hayo. 
 Hivi karibuni IPTL, PAP na Seth kwa kupitia wakili wao Kusalika, walimfungulia kesi ya madai Kafulila, mahakamani hapo wakiiomba aamuriwe kuwalipa fidia ya jumla ya sh. bilioni 310 kutokana na kutangaza taarifa za kashfa dhidi yao. 
 Katika kesi yao ya msingi, wadai hao wanaiomba mahakama kuu katika hukumu yake, imwamuru Kafulila awalipe sh. bilioni 210 kama fidia kutokana na kashfa hizo na hasara ya taswira ya biashara na hadhi yao. Aidha, aamriwe kuwalipa sh. bilioni 100 kama fidia ya madhara ya jumla kutokana na usumbufu walioupata kutokana na taarifa za kashfa zilizotolewa dhidi yao na awaombe radhi kutokana na taarifa hizo, gharama ya kesi, riba kwa kiasi cha fedha yote wanayodai kwa kiwango cha asilimia cha mahakama kutoka tarehe ya hukumu hadi tarehe ya mwisho wa malipo hayo. 
 Pia, wanaiomba mahakama kutoa amri nyingine itakazoona zinafaa. Kwa kupitia hati yao ya madai ya kesi ya msingi, wadai hao wanadai kwa nyakati tofauti ndani na nje ya Bunge na kupitia mitandao ya kijamii, Kafulila ametoa maneno ya kashfa dhidi yao kwamba wamejipatia fedha katika akaunti ya Escow iliyoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa njia zisizo halali. 
 Wadai hao wanadai IPTL iliingia mkataba na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) la kuisambazia umeme na imekuwa ikitekeleza majukumu yake kama walivyokubaliana. 
 Inadaiwa IPTL ilikuwa na mgogoro na kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited na TANESCO ambapo sh. bilioni 200 zilihifadhiwa katika akaunti ya Escrow iliyofunguliwa BoT, kusubiri kumalizika kwa mgogoro huo uliokuwa mahakama kuu. 
 Kwa kupitia hati hiyo inadaiwa kuwa baada ya kumalizika na kuhimitishwa kwa mgogoro huo, mahakama ilitoa amri ya IPTL kukusanya fedha hizo na BoT kutakiwa kuziachia. 
 Wadai hao wanadai katika hali ya kushangaza na bila ya uhalali wowote, Kafulika katika shughuli mbalimbali nje na ndani ya Bunge na kupitia mitandao ya kijamii  alimua kusambaza taarifa za kashfa kwa IPTL na Mkurugenzi Mtendaji wake. 
 Inadaiwa Juni, 2014, Kafulila alichapisha taarifa za kwamba IPTL na Seth walijipatia fedha kutoka katika akaunti ya Escrow isivyo halali, wakati si kweli na imehusika katika vitendo viovu vya kuchukua fedha katika akaunti hiyo. 
 Kwa kupitia hati hiyo, inadaiwa Kafulila amekuwa akitoa taarifa za kashfa, kwa kumtaja Seth kwa jina la singasinga, jambo ambalo si sawa na hivyo kumharibia sifa yake na kumsababishia uendeshaji wa biashara zake zinazotekelezwa na IPTL na PAP kudorora. 
 Inadaiwa kutokana na taarifa zilizotolewa na Kafulila, ameisababishia jamii kuamini kuwa ni kweli IPTL imejipatia fedha hizo katika akaunti ya Escow bila uhalal na zimesababisha hasara au kupungua kwa hadhi ya kampuni hizo. 
 Hata hivyo, wadai hao wanadai Kafulila akiwa mbunge ana kinga ya kutochukulia hatia za kisheria kwa masuala ambayo ameyasema bungeni, lakini amekuwa akitoa taarifa za kashfa dhidi ya wadai ndani na nje ya shughuli za bunge. 
 Wadai hao wanadai taarifa zilizosambazwa na Kafulila mbali ya kuwashushia hadi pia zimesababisha hasara ya kibiashara na ameendelea kufanya hivyo licha ya kupewa taarifa ya maneno na ya maandishi. Inadaiwa kutokana na taarifa hizo, Kafulila amesababisha hadhi ya kampuni hizo kushuka sio tu nchini bali hata kimataifa, hivyo kuwasabishia hasara kibiashara na madhara ya kisaikolojia na usumbufu kwa menejimenti. 
 Wadai hao wanadai kitendo cha Kafulila kuelezea mambo yaliyotokea katika mahakama za kisheria kuhusu maombi baina ya IPTL na kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited kimesabaisha si tu kuingilia uhuru wa mahakama bali pia hasara kwa IPTL, wakati alikuwa akijua kilichoendelea mahakani. 
Inadaiwa IPTL inatoa huduma ya kuisambazia umeme Tanesco, hivyo kutokana na taarifa za mdaiwa zimehatarisha uhusiano baina yake na shirika hilo hivyo kusababisha kudorora kwa uchumi na biashara yao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...