Na Anna Nkinda - Maelezo,  Nachingwea

Wanafunzi wa kike wa vyuo vya ualimu nchini wametakiwa kuvaa mavazi  nadhifu  yanayoendana na maadili ya kazi yao  ili wanafunzi na jamii inayowazunguka ijifunze  kutoka kwao kwani wao ni kioo cha jamii.

Mwito huo umetolewa  hivi karibuni  na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na baadhi ya wanafunzi wa kike  wa chuo cha Ualimu Nachingwea mara  baada ya kumalizika kwa futari aliyoiandaa kwa ajili ya viongozi wa wilaya iliyofanyika  chuoni hapo. 

Mama Kikwete ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa kupitia wilaya ya Lindi mjini alisema siyo jambo jema kwa mwalimu kuvaa mavazi yanayoonyesha sehemu za miili yao ikiwemo kata mikono, nguo zinazobana na sketi fupi  kwa kufanya hivyo ni kwenda kinyume na haiba ya ualimu. 

Alisema, “Sikuhizi kuna baadhi ya watu  wanavaa mavazi yasiyoendana  na utamaduni wa mtanzania,  nyinyi kama walimu ambao ni kioo cha jamii na mnawafundisha  wanafunzi madarasani msifanye hivyo  kwa kufanya hivyo watoto  wataiga na kufikiria  kuwa kuvaa mavazi hayo ni sawa”.

Mama Kikwete pia  aliwataka wanafunzi hao kutokuchagua  maeneo ya kwenda kufanya kazi pindi wamalizapo masomo yao na kupangiwa vituo vipya vya kazi kwani kazi ya ualimu ni wito na kama mtu  hakuipenda kazi hiyo basi angechagua fani nyingine za kusoma.

“Baadhi ya walimu wamekuwa wakikataa kwenda kufanya kazi katika maeneo ya vijijini, na wengine wakipangiwa vituo vya mbali na mjini wanaogopa na kudiriki hata kuacha kazi,  kama ni hivyo kwa nini ulipoteza fedha  na muda wako kusomea ualimu?” , aliuliza Mama Kikwete.

MNEC huyo alimalizia kwa kuwataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kujiepusha na mahusiano ya kimapenzi wawapo masomoni kitendo ambacho kitawasaidia  kumaliza masomo yao salama na kurudi nyumbani bila ya kufukuzwa chuo kwa ajili ya kupata ujauzito.

Mama Kikwete ambaye kitaaluma ni mwalimu miaka ya nyuma alisoma chuo cha ualimu Nachingwea na juzi akiwa chuoni hapo alitembelea Bweni la wasichana la Kawawa  ambalo ndilo alilokuwa analala wakati akiwa mwanafunzi wa chuo hicho.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 27, 2014

    Nakuunga mkono mama Kikwete
    Siku hizi hawa vijana waona ni ustaarabu kuvaa nguo zisizo na heshima, na nyingine kwa ufupi ni kama kwenda uchi.Vijana wana uhuru wa kuigiza mavazi ya vijana wenzao duniani au kubuni mavazi yao wenyewe, lakini lazima waweke heshima na mila zetu mbele

    ReplyDelete
  2. Kabisaaa! Nakuunga mkono Mama Salma Kikwete kuhusiana na suala hilo la kivazi kwa walimu. Na khasa kwa sasa hivi imekuwa too much kwa walimu khususan walimu wa kike kujivalia ndivyo sivyo wakati wanapokuwa katika mazingira yao ya kazi. Nakiri siyo kuwa ni wote, ila baadhi yao. Unaweza kumkuta mwalimu kavaa nguo makwapa nje, mapaja wazi, kivazi chenyewe kifupi na kiimembana kupita maelezo. Mbona katika mafunzo ya ualimu kuna kitu 'Haiba' (Personality) ya mwalimu, sasa imepelekwa wapi siku hizi? Maana kama "Mwalimu Haiba' naamini ina include so many things ili kumjenga na kumfanya huyu Mwalimu aonekaneje na kukubalika vilivyo katika fani yake hii ya ualimu na khasa katika mazingira yake husika ya kazi. Tujitahidi walimu kuirejesha ile hadhi, heshima na sifa ya Mwalimu bora. Naamini unapo mantain haiba yako, basi hata wanafunzi watakuelewa kile unachokiwakilisha kwao uwapo darasani, otherwise ni kuwachanganya tu psychologically.

    ReplyDelete
  3. AnonymousJuly 28, 2014

    Kufanikiwa kwa hoja hii inapaswa ifanyike kampeni kitaifa kwani tatizo hili ni kubwa na hivyo linaitaji nguvu kubwa kulikabili.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...