Na Vedasto Msungu, Singapore 
Makatibu wakuu wa baadhi ya wizara katika serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na baadhi ya watendaji wakuu wa mashirika ya umma wako nchini Singapore kwa ziara ya mafunzo iliyoandaliwa na taasisi ya Uongozi, UONGOZI Institute ya Tanzania. 
Akiongea nchini Singapore, kiongozi wa ujumbe wa makatibu wakuu hao, Dk Frolens Turuka ambae ni Katibu mkuu ofisi ya Waziri mkuu amesema ziara hiyo ya viongozi waandamizi wa serikali inalenga kujifunza kuhusu mfumo wa uendeshaji wa shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi kwa kushikisha sekta binafsi chini ya mfumo wa PPP (Public Private Partnership). 
Dk Turuka amesema mfumo huo umeisaidia sana nchi ya Singapore kupiga hatua kubwa kimaendeleo tangu ilipopata uhuru wake mwaka 1965 na ikaanza kuwekeza katika teknolojia na biashara ya kimataifa. Amesema Tanzania kupitia taasisi ya Uongozi ambayo imekuwa ikiandaa mafunzo ya aina mbalimbali kwa viongozi, inachukua mfumo huo kama mfano wa PPP kuigwa ambao unaweza kuisaidia nchi kupiga hatua kubwa za kiuchumi na kijamii. 
Aidha Dk Turuka amesema licha ya kuwa nchi hii ya Singapore ni ndogo ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 716 tu lakini ina maendeleo makubwa ambayo hayafanani na nchi nchi duniani zenye rasilimali nyingi za kiuchumi ikiwemo Tanzania.
Hata hivyo amesema mfumo chini ya mpango wa mapokeo makubwa sasa unaotekelezwa na serikali ya Tanzania na ushirikiano kati ya sekta binafsi, anayo imani kwamba nchi itapata mafanikio makubwa. 
Nae Denis Rweyemamu kutoka taasisi ya Uongozi, inayoratibu ziara ya mafunzo kwa viongozi hao amesema hii siyo mara ya kwanza kwa Uongozi Institute kuandaa mafunzo kama hayo kwa viongozi wa ngazi mbalimbali.
 Amesema taasisi hiyo itaendelea kuandaa mafunzo kama hayo kwa viongozi mafunzo yanayolenga kusaidia kuharakisha maendeleo ya Tanzania kijamii na kiuchumi chini ya mfumo wa utekelezaji wa majukumu mbalimbali kwa ubia kati ya serikali na sekta binafsi.
 Pamoja na Katibu Mkuu ofisi ya waziri mkuu Dk Frolens Turuka, wengine waliomo kwenye ziara hiyo ya mafunzo nchini Singapore ni Katibu Mkuu wizara ya Fedha Dr Servacius Likwelile, Katibu Mtendaji tume ya Mipango, Ofisi ya rais Dk Philip Mpango, Katibu mkuu wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi, Katibu Mkuu wizara ya Maji, Injinia Bashir Mrindoko, Naibu Mwanasheria mkuu wa serikali, George Masaju na Dk Shaban Mwinjaka, Katibu mkuu wizara ya Uchukuzi. 
Wengine ni Injinia Joseph Nyamhanga, Naibu katibu mkuu wizara ya ujenzi, Mkurugenzi mkuu wa shirika la umeme nchini TANESCO injia Felichesmi Mramba, Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania,TPA injinia Madeni Kipande, Kamishina wa PPP, wizara ya Fedha, Dk Frank Mhilu, Mkuu wa Idara ya utafiti na sera kutoka taasisi ya Uongozi, Denis Rweyemamu, Amir Said kutoka kituo cha uwekezaji Tanzania TIC na Linda Manu kutoka taasisi ya Uongozi 
Wakiwa nchini Singapore, ujumbe huu wa viongozi waandamizi wa serikali ya Tanzania na watendaji wakuu wa mashirika ya umma, wanatembelea taasisi mbalimbali za sekta binafsi ambazo zinatekeleza majukumu mbalimbali ya kwa ubia kati ya serikali ya Singapore na sekta binafsi katika maeneo ya usafiri, Bandari, maji, nishati usafirishaji. Ziara hiyo kwa nchini Singapore inaratibiwa na taasisi ya kimataifa ya biashara ya serikali ya Singapore iitwayo International Enteprise Singapore (IES)
 Picha ya pamoja ya viongozi waandamizi wa serikali ya Tanzania walioko nchini Singapore kwa mafunzo yaliyoandaliwa na taasisi ya Uongozi ya Tanzania. Picha hii imepigwa nje ya jengo la taasisi ya HYFLUX ya nchini Singapore, taasisi binaffsi inayojishughulisha na kusafisha maji ya baharini na maji machafu kwaajili ya matumizi ya majumbani. Singapore haina chanzo cha maji ya mito wala visima kwahiyo maji yake kwa matumizi ya majumbani huagizwa kutoka nchini Malayisia
 Nchi ya Singapore ni miongoni mwa nchi zenye majengo marefu duniani, nchi hii ni ndogo yenye ukubwa wa kilomita za mraba 716 tu eneo ambalo ni dogo hata kuliko ukubwa wa baadhi ya vijiji vya Tanzania hivyo inalazimika kujenga majengo yake kwenda juu yaani maghorofa kama yanavyoonekana na kuna majengo yenye ghorofa mpaka 72 kwenda juu.
Baadhi ya viongozi waandamizi wa Tanzania walioko kwenye ziara ya mafunzo nchini Singapore wakipata maelezo ya namna mitambo ya kuchuja na kusafisha maji ya baharini kwaajili ya matumzi ya majumbani inavyofanya kazi,. Ziara ya viongozi hawa wa serikali ya Tanzania iliyoandaliwa na taasisi ya Uongozi inalenga kujifunza kuhusu uendeshaji wa serikali chini ya mfumo wa ubia kati ya serikali na sekta binafsi ambao umesaidia kuharakisha maendeleo ya nchi ya Singapore.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 11, 2014

    Hata kama sijatembea mikoa yote hivi Tanzania kuna mkoa wowote wenye majengo kama haya ya singapore kweli?, hata siyo kama kwa kujenga kwa mipango ya miji ya baadaye?

    ReplyDelete
  2. AnonymousJuly 12, 2014

    Hhahahahaha ziara ya mafunzo alafu nini kinafuata baada ya kuhitimu???? walishakwenda wengi ziara kama hizi tena nchi mbalimbali......Tandale, Vingunguti,Mburahati na Uwanja wa fisi ziko vileile.....

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...