SHIRIKA
la Madini la Taifa (STAMICO) leo linafunga upokeaji wa maombi ya nia
(expression of interest) ya makampuni yanayotaka kuingia ubia na STAMICO
katika uendelezaji wa mradi uchimbaji makaa ya mawe na ufuaji umeme
huko Kiwira.
STAMICO ilitangaza mwezi uliopita kukaribisha maombi hayo
yatakayowezesha ubia huo kupata fedha za kughramia mradi kwa asilimia
100 na kushiriki kuendesha mradi huo.
Makampuni
yenye nia ya kuwekeza kwa ubia na STAMICO yalitakiwa kuwasilisha
maelezo ya kutosha kuhusu makampuni hayo pamoja na uthibitisho wa uzoefu
wa kuendesha migodi ya makaa ya mawe na ufuaji umeme kwa kutumia makaa
ya mawe.
Makampuni hayo pia yanatakiwa kuonesha uzoefu wao katika kuendesha
miradi kama hiyo sehemu nyingine Duniani ikiwemo nchi za Afrika.
Aidha STAMICO inayataka makampuni yenye nia kuonesha uwezo wake wa kifedha na kiufundi.
Maombi
ya makampuni hayo pia yanatakiwa kuonesha namna gani yatakavyotumia
utaalamu na huduma za ndani kama ilivyoainishwa kwenye Sheria ya Madini
ya mwaka 2010.
Makampuni ambayo maombi yake yatakubaliwa na STAMICO yatakaribishwa
kuchukua nyaraka za zabuni na kuwasilisha michanganuo yao ya kiufundi na
kifedha.
Uendelezaji wa mradi Kiwira umegawanyika katika sehemu nne ambazo ni
upanuzi wa mgodi uliopo wa chini ya ardhi, ujenzi wa mgodi wa wazi,
ununuzi na ufungaji wa mitambo ya kufua umeme na ujenzi wa njia za
kusafirisha umeme.
Upanuzi
wa mgodi wa chini utakaoongeza uzalishaji wa makaa ya mawe kutoka tani
150,000 kwa mwaka hadi tani 300,000 kwa mwaka wakati mgodi mpya wa wazi
unategemea kuzalisha tani milioni 1.2 za makaa ya mawe kwa mwaka.
Uendelezaji wa mradi huu pia utahusisha ujenzi wa mtambo wa kufua
umeme wa Megawati 200 na ujenzi wa njia ya kusafirisha yenye urefu wa km
100 toka eneo la Kiwira Wilayani Ileje hadi Mbeya mjini.
Ujenzi wa mgodi wa Kiwira ulianza mwaka 1983 na kukamilika 1988 kwa
gharama za Sh.4.29 bilioni, ukiwa ni mkopo wa masharti nafuu kutoka
Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.
Mwezi Juni, 2005 mgodi wa Kiwira ulibinafsishwa kwa kampuni ya Tan
Power Resources (TPR) kwa asilimia 70 na Serikali ilibaki na asilimia
30.
Ubia huu ulilenga zaidi katika kuzalisha umeme wa MW 200 kwa kutumia makaa ya mawe ifikapo 2009.
Katika kipindi cha kuanzia Juni, 2005 hadi Julai,2009 zilifanyika kazi mbalimbali za kuendeleza mgodi huu.
Miongoni
mwa kazi hizo ni upembuzi yakinifu na usanifu wa mgodi, upembuzi
yakinifu kwa ajili ya kufua umeme wa MW 200 na kusainiwa kwa mkataba wa
mauzo ya umeme wa MW 200 na TANESCO mnamo mwezi Agosti 2006.
Kazi nyingine ni kusainiwa kwa mikataba ya ujenzi na utengenezaji wa
mitambo, kukamilika kwa tathmini nne za mazingira na kukamilika kwa
upimaji wa njia ya umeme ya kV 220 kutoka eneo la mgodi kwenda Mbeya.
Mwezi
Julai,2009 Serikali iliamua kuurudisha mgodi wa Kiwira Serikalini kwa
asilimia 100 kutokana na kukwama kwa uendelezaji wa Mgodi chini ya TPR
na kushindwa kuwalipa wafanyakazi mishahara yao kwa muda mrefu tangu
mwezi Agosti,2008.
Baada ya majadiliano ya muda mrefu, tarehe 28, Novemba 2011 Serikali
na TPR zilifikia muafaka wa Serikali kuuchukua mgodi kwa asilimia 100.
Mtaji
unaohitajika kuendeleza mgodi huu ni takriban Dola za Marekani Milioni
400 ambazo zinaweza kupatikana kwa njia mbili;kwa kumtafuta mbia mwenye
uwezo wa fedha au kwa kukopa katika taasisi mbalimbali za fedha.
Aidha STAMICO inaangalia uwezekano wa kufanyia ukarabati mashine ya
kufua umeme ya MW 6 iliyopo katika mgodi huu ili umeme utakaozalishwa
uuzwe TANESCO.
Katika mwaka wa fedha 2014/15, Serikali imeitengea STAMICO Shs.
bilioni 5 kwa ajili ya usimamizi na uangalizi wa mgodi katika kipindi
hiki cha mpito.
Hii inahitaji mbia mwenye uwezo wa kifedha kwa sababu gharama za kuwekeza na za uendeshaji ni kubwa..
ReplyDelete