Serikali ya Tanzania inatarajia kutuma wataalam kwenda nchini Canada
katika Kamisheni ya Mafuta na Gesi ya jimbo la British Columbia (BC Oil&
Gas Commission), ili kupata uelewa zaidi katika masuala ya udhibiti wa
mafuta na gesi nchini.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia
Nishati, Charles Kitwanga wakati akiongea na watendaji wa Kamisheni ya
Mafuta na Gesi ya Jimbo la British Columbia katika Ofisi za kamisheni hiyo
zilizo katika mji wa Victoria nchini Canada.
Akiongoza ujumbe wa Tanzania uliotembelea Kamisheni hiyo ili kujifunza
masuala ya udhibiti wa sekta ndogo ya gesi asilia, na mafuta, Naibu Waziri
alisema kuwa lengo la serikali ya Tanzania ni kuhakikisha kuwa rasilimali
zilizopo zinaendelezwa na faida yake kuonekana kwa wananchi hivyo
wataalam watakwenda nchini Canada katika Kamisheni hiyo ili kuongeza
uelewa katika masuala ya udhibiti ambao kwa kiasi kikubwa unachangia
katika kuhakikisha kunakuwa na maendeleo endelevu ya rasilimali zilizopo
Tanzania.
" Mtazamo wa wananchi wengi ni kuwa makampuni ya kigeni yanakuja
nchini Tanzania kuchukua rasilimali na kuondoka nazo bila wananchi
hao kufaidika hivyo serikali inafanya kila jitihada ili faida za rasilimali zetu
ziwafikie wananchi wote na moja ya vigezo vya jitihada hizo ni kuwa
na mamlaka madhubuti za udhibiti zitakazohakikisha makampuni ya
nje na ndani ya nchi yanafanya kazi kwa kuzingatia kanuni na sheria
zinazoongoza sekta husika" alisema Kitwanga.
Naibu Waziri alieleza kuwa Tanzania ikiwa katika mchakato wa
kutengeneza sheria na kanuni zitakazoongoza sekta ya gesi asilia na
mafuta, inahitaji kupata maoni na uelewa zaidi kutoka katika nchi zilizopiga
hatua katika uendelezaji wa rasilimali hizo ikiwemo jimbo la British
Columbia ambalo limegundua gesi asilia kiasi cha zaidi ya futi za ujazo
trilioni 2900.
Naye Ofisa Mkuu wa Operesheni katika Kamisheni ya Gesi na Mafuta ya
British Columbia, Mhandisi Ken Paulson alieleza kuwa Kamisheni hiyo
ambayo imeanzishwa zaidi ya miaka 15 iliyopita ina jukumu la kudhibiti
shughuli zote za mafuta na gesi asilia ikihusisha, utafiti, uendelezaji na
usafirishaji wa rasilimali hizo kwa njia ya bomba.
Mhandisi Paulson alieleza kuwa Kamisheni hiyo pia ina jukumu la
kukusanya takwimu za kijiolojia zinazotumika katika shughuli za utafutaji
wa gesi asilia na mafuta na kuzitangaza kwa njia ya tenda ili makampuni
yanayohitaji kufanya shughuli za utafutaji mafuta na gesi katika jimbo hilo
yanunue takwimu hizo kutoka Kamisheni hiyo.
Kuhusu matumizi ya gesi asilia, Afisa Mkuu wa Operesheni aliueleza
ujumbe huo kutoka Tanzania kuwa asilimia 15 ya kiasi cha gesi
kilichogunduliwa katika jimbo hilo kinatumika ndani ya jimbo la British
Columbia kwa matumizi mbalimbali na kiasi kinachobaki kinasafirishwa
kwenda bara la Amerika Kaskazini.
" Ingawa tunasafirisha gesi kwenda Amerika Kaskazini, mahitaji ya soko
hilo yanashuka kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa gesi nchini
Amerika, hata hivyo tumejipanga kukabiliana na hali hiyo kwa kutumia
gesi hii kwa masuala mengine ikiwemo kuzalisha methano, matumizi ya
majumbani na kutumika katika vivuko ambavyo vitakuwa vinatumia mafuta
na gesi" alisema Mhandisi Paulson.
Kuhusu mfumo wa ugawanaji mapato (PSA) kati ya makampuni ya
utafutaji na uchimbaji gesi asilia na mafuta, Bw. Mhandisi Paulson alieleza
kuwa kampuni ikianza uzalishaji wa gesi au mafuta, serikali ya jimbo hilo
hukusanya mrabaha wa asilimia 10 hadi 20 ya Mapato.
Katika ziara hiyo ya mafunzo nchini Canada, Naibu Waziri Nishati na
Madini ameambatana na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Nishati na Madini, Mhe. Victor Mwambalaswa pamoja na baadhi ya
wajumbe wa Kamati hiyo akiwemo, Murtaza Mangungu (Mb.), Raya
Ibrahim (Mb.), Richard Ndasa (Mb.), Deogratias Ntukamazina(Mb.), Shafin
Sumar (Mb.) na wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga (wa tatu kutoka kushoto), Mwenyekiti Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa (wa pili kutoka kushoto) na Mbunge wa
Sumve, Richard Ndasa (wa kwanza kushoto) wakimsikiliza Eng. Ken Paulson, Afisa Mkuu wa Operesheni
katika Kamisheni ya Gesi na Mafuta ya Jimbo la British Columbia nchini Canada mara walipofika katika
Kamisheni hiyo ikiwa ni sehemu ya ziara ya mafunzo kwa ujumbe huo katika sekta ya uziduaji.
Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (wa kwanza kushoto) akieleza kitu katika
mkutano kati ya watendaji wa Kamisheni ya Gesi na Mafuta ya Jimbo la British Columbia nchini Canada
pamoja na ujumbe kutoka Tanzania ukiongozwa na Naibu Waziri Nishati na Madini, Charles Kitwanga
(wa tano kutoka kushoto).Wengine katika picha ni Mwenyekiti Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini,
Victor Mwambalaswa (wa nne kutoka kushoto) Mbunge wa Ngara, Deogratias Ntukamazina (wa pili
kutoka kushoto), Richard Ndasa (Mb. Sumve), (wa tatu kutoka kushoto), Raya Ibrahim (Mb.) (wa pili
kutoka kulia) pamoja na watendaji kutoka Wizara ya Nishati . Katikati ni Eng. Ken Paulson, Afisa Mkuu
wa Operesheni katika Kamisheni ya Gesi na Mafuta ya Jimbo la British Columbia nchini Canada.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...