Ujumbe kutoka Tanzania ukiwa Chuo Kikuu cha Calgary katika jimbo la Alberta nchini Canada.Katika picha kutoka kushoto ni, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga (wa saba), Naibu Waziri TAMISEMI, Kassim Majaliwa (wa tano), Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira, Ummy Mwalimu (wa sita). Wabunge, Richard Ndasa (wa nne), Deogratias Ntukamazina (wa tatu), Murtaza Mangungu  (wa pili) na Shafin Sumar (wa kwanza kushoto. Wengine (kulia) ni wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini na watendaji kutoka Chuo Kikuu cha Calgary, Canada. 
Ujumbe kutoka Tanzania ukiwa katika makao makuu ya Taasisi ya Udhibiti Nishati katika jimbo la Alberta nchini Canada.Katika picha ni, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga (wa sita kutoka kulia), Naibu Waziri TAMISEMI, Kassim Majaliwa (wa tano kutoka kulia), Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira, Ummy Mwalimu (wa tatu kushoto). Wabunge, Richard Ndasa (wa nne kutoka kulia), Raya Khamisi (wa pili kutoka kulia). Wengine ni wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini na watendaji kutoka Mamlaka ya Udhibiti Nishati ya Alberta wakiongozwa na Zeeshan Syed, Mkurugenzi wa Mahusiano ya Kitaifa, Kimataifa na Serikali, (wa tatu kutoka kushoto).
============  =========  =========
Serikali yashauriwa kuwabana wawekezaji.
Serikali ya Tanzania imeshauriwa kuweka sheria madhubuti zitakazohakikisha wawekezaji wa kigeni wanaleta faida katika nchi badala ya kunufaisha makampuni yao tu.

Hayo yamesemwa na Bw. Zeeshan Syed, Mkurugenzi wa Mahusiano ya Kitaifa, Kimataifa na Serikali katika Taasisi ya Udhibiti Maendeleo ya Nishati ya Jimbo la Alberta nchini Canada wakati alipokuwa akizungumza na ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga uliofika katika makao makuu ya Taasisi hiyo ikiwa ni sehemu ya ziara ya mafunzo kuhusu sekta ya uziduaji.

“kwa kawaida wananchi huwa wana matarajio makubwa ya manufaa ya rasilimali zinazowazunguka hivyo ni muhimu kwa serikali kuwa na sheria zitakazowabana wawekezaji ili wanapomaliza shughuli zao, pia faida ibaki kwa wananchi” Alisema Bw.Syed.

Mkurugenzi huyo alieleza kuwa licha ya taasisi hiyo kuwa mdhibiti wa nishati lakini pia ina jukumu la kudhibiti uhifadhi wa mazingira ili kuhakikisha kuwa shughuli za uendelezaji wa nishati zinafuata sheria za nchi za utunzaji mazingira.

Naye Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Charles Kitwanga alimweleza Bw.Syed kuwa licha ya Tanzania kuwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) lakini bado nchi inahitaji kujifunza kutoka kwa nchi nyingine zenye uzoefu ili kuboresha shughuli za udhibiti nchini Tanzania.

“Shughuli za udhibiti nishati katika Taasisi hii zina zaidi ya miaka 75 na hivyo Tanzania inahitaji kupata uzoefu kutoka kwenu ili kufahamu hatua mlizopitia kufika hapa mlipo leo”. Alisema Waziri Kitwanga.
Wakati huohuo Naibu Waziri na ujumbe wake unaojumuisha baadhi ya wabunge kutoka Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini walitembelea Chuo Kikuu cha Calgary ambacho kimebobea katika kutoa elimu juu ya masuala ya sera za Uchumi, Nishati, Mazingira na kutoa ushauri katika utengenezaji sera katika sekta ya uziduaji.

Katika Chuo hicho ujumbe huo ulikutana na Mkurugenzi anayeshughulikia Sera za Umma, Bw.Jack Mintz ambaye   aliueleza ujumbe huo kuwa Tanzania ni moja kati ya nchi sita duniani (huku ikiwa ni pekee kutoka Afrika) ambazo zinapewa kipaumbele na chuo hicho katika masuala ya ushirikiano wa kujenga uwezo kwenye masuala ya sera.

Mkurugenzi huyo alieleza kuwa, Chuo cha Calgary pia kitashirikiana na Tanzania katika kuwajengea uwezo watumishi kwa kutumia pia vyuo vingine ambavyo wana ushirikiano navyo na kwamba mafunzo hayo yanaweza kufanyika ndani na nje ya Tanzania .

Pamoja na suala la kujenga uwezo kwa watanzania ili kuweza kuandaa sera zitakazokuwa na manufaa kwa nchi Bw.Mintz aliueleza ujumbe huo kuwa ni muhimu kwa serikali ikawa ndiyo msimamizi mkuu wa rasilimali  za nchi ili faida zinazotokana na rasilimali hizo ziwafikie wananch wote.

Naye Naibu Waziri Katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Kassim Majaliwa pamoja na kushukuru kwa Tanzania kupewa kipaumbele na Chuo hicho katika kujenga uelewa, alimweleza Mkurugenzi huyo wa Chuo kuwa Tanzania kwa sasa inakaribisha wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza Tanzania hivyo suala la kupata elimu na uzoefu zaidi ili kuendana na kasi ya uwekezaji linapewa kipaumbele. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 15, 2014

    Ukiona competitor wako anakuwa mshauri wako, basi umeliwa saaaaaaaaaaana!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...