Bi Scholastika Mhagama akiwa katika mlango wa nyumba yake.
 ---------------------
Na Oswald Ngonyani wa demashonews - Peramiho.
Wahenga walisema ‘Ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni;’ Jamii inazidi kujawa na chuki na ukatili ndani yake, imekuwa kawaida siku hizi kusikia fulani kamuua fulani kwa kisa kisichokuwa na maana.

Maalbino wanakatwa viungo vyao kwa visingizio vya kupata utajiri kwa watu wasiokuwa na huruma, watoto wadogo wananyimwa haki zao na kuwekwa ndani ya maboksi na wengine kuishi maisha yao katika uvungu za kitanda yote haya ni mambo ya kutisha yanayotendeka katika jamii zetu.
Hali imekuwa tete amani na upendo vinazidi kuyeyuka kama barafu, watu hawana utu tena, wamejivika ngozi za kondoo wakati mioyo yao ni ya Simba, hakuna tena roho ya huruma kwa wanadamu wa dunia ya leo.
Choo cha bibi Scholastika Mhagama

Wakati haya yote yanaendelea kutendeka katika jamii zetu ni kama vile tunazidi kuugeuza ulimwengu tunaoishi kuwa ‘Uwanja wa dhambi’ ulimwengu wa kutojaliana  tena, wanadamu wamebadilika na kuwa kama wanyama na tena hata zaidi ya mnyama.
Katika hali isiyo ya kawaida Bibi mmoja ambaye ni mlemavu wa miguu na mzee sana anayeishi peke yake katika kibanda ambacho kwake ni kama gereza ambalo hataweza kutoka tena maisha yake yote, amejikuta akifanya kitu kisicho cha kawaida kwa binadamu wa kawaida.
Jeneza la bibi likitolewa ndani kwake na wanachama wa Kombination Camp

Namzungumzia Bibi Scholastica Mhagama mwenye umri unaokadiriwa kufikia (76), ambaye ni mlemavu wa miguu anayejongea kwa kutambaa ambaye anaishi peke yake katika kibanda chake katika kijiji cha Lundusi mtaa wa Linga huko Peramiho Songea mkoani Ruvuma. Ni jambo la kusikitisha sana kwa bi kizee kama huyu kuishi peke yake akiwa hana msaada wa kueleweka kutoka kwa jamii inayomzunguka.

Bibi huyu anayeishi kwa uchungu na majonzi amekata tamaa kabisa ya maisha hali iliyomfanya aamue kuchonga jeneza lake mwenyewe akijiandaa kufa siku yoyote.Bibi huyu anaishi na jeneza hilo chumbani kwake.
“Maisha yangu ni magumu sana, naishi kama mnyama, sipendwi na ndugu zangu wala na jamii inayonizunguka. Wamenichoka sina raha natamani hata Mungu anichukue sasa hivi ili nikapumzike, nasali kwa sala zote natubu na kujuta kila siku lakini wala Mungu hanichukui, sijui kwanini” Anasema Bi Scholastica Mhagama kwa uchungu.
  Jeneza la Bi Scholastika Mhagama

Akielezea historia ya maisha yake Bi Scholastika anasema alizaliwa akiwa na miguu yote lakini alipata bahati mbaya ya kugongwa na nyoka alipokuwa darasa la pili hali iliyomfanya kukatwa mguu ili kuepusha madhara mengine kama vile kifo. Hivyo maisha yake yalibadilika na tangu hapo akawa mlemavu.

 Hali hiyo ya ulemavu lakini pia uzee alionao vimemfanya ashindwe kujihudumia kwa lolote zaidi ya kupika tu. Hata hivyo anakosa mahitaji muhimu kama vile maji na chakula hali inayomfanya alale na njaa kwa baadhi ya siku.

Kwa hali aliyo nayo ni wazi kuwa Bi Scholastika anahitaji baiskeli ya miguu mitatu (wheel chair) ambaye itamwezesha  kutembea  kwa kuwa hivi sasa anatambaa na kupata maumivu makali kutokana na nyama iliyobakia kwenye nyonga baada ya kukatwa mguu.

Bi Scholastika anazidi kueleza kuwa kuna watu waliwahi kufika kumuandikisha jina lake na kumuingiza katika orodha ya watu wanaostahili kupata msaada lakini anasikia misaada inafika kwa jina lake lakini yeye mwenyewe hajawahi kuipata.

Vipi kuhusu Sera ya Wazee?
Kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003 inaweka bayana kuwa suala la uzee na kuzeeka limekuwa lenye umuhimu mkubwa ambapo karne ya ishirini imeshuhudia ongezeko kubwa la idadi ya wazee.

Kwa kurejelea takwimu zilizopo ni kwamba, ifikapo mwaka 2050 idadi ya wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 60 nchini hapa itaongezeka na kufikia wazee milioni 8.3 (Sawa na asilimia 10 ya watanzania wote)

Kama hiyo haitoshi, Taarifa ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 1999 inaeleza kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya wazee duniani na kwamba ongezeko hilo linaonekana zaidi katika nchi zinazoendelea (Tanzania ikiwepo) ambapo viwango vya ongezeko hilo havilingani na uwezo wa rasilimali zilizopo za kuwahudumia.

Rasilimali hizo zinajikita zaidi katika Nyanja za msingi katika makuzi ya binadamu yoyote zikiwemo Nyanja za afya, lishe na huduma nyingine za msingi zisizoweza kuepukwa na binadamu yeyote.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. Inasikitisha na kutilisha imani kwa kweli, na uwe pole bibi yangu, kweli dunia ya leo, hujafa hujaumbika na wala hujastirika bado. Basi wahusika madhali mmefanikisha kutukhabarisha yote hayo, pia ingelikuwa la busara na maana, alau mkamtengenezea jeneza zuri akaliona, pengine atafarijika alau akajuwa ni wapi atakuja hifadhiwa siku umauti utakapomfika(MOLA akuzidishie umri bibi yangu). Isiwe tu kutupigia picha mkatuonyesha hapa na kisha mkamuacha kama alivyo, itakuwa ni sawa na kumkejeli bibi wa watu.
    Tayari hapo keshajisemea mwenyewe, misaada inakuja kwa jina lake lakini haambulii kitu, kweli binaadam imani zimetutoka na wala huruma hatuna. Watu tunashindwa hata kummithilisha bibi huyo na wale bibi zetu mwenyewe, alau tukaingiwa na huruma japo kidogo.

    ReplyDelete
  2. Hata tukifuata mfumo gani wa uchumi tusije hata siku moja tukajisahau mpaka tukashindwa kusaidiana na kutembeleana. Bibi huyu kama ana watoto, jamaa, majirani au ndugu wa karibu hata nyumba za ibada ziwajibike wahakikishe anapata chakula. Katika umri huu wa bonasi hawezi kupata nguvu za kulima au kupata kazi au biashara ya kujikimu na maisha kama mna uwezo kidogo mmjengee nyumba ya maana kitanda godoro na nguo nzuri msisahau redio ya kumburudisha na betri zake na tanki la maji na taa ya sola. Jeneza liwekwe stoo bibi aendelee kuishi kwa amani.

    ReplyDelete
  3. Ni hatari sana.
    Sina mengi ya kusema kwani maelezo yako wazi.
    Zaidi nasema aibu kwenu viongozi mnaomzunguka bibi huyu masikini.

    Mkumbuke "machozi yake ni laana kwenu"

    ReplyDelete
  4. Jamani tumuogope Mungu huyu bibi akifa ambao wako karibu nae watakuwa na dhambi kubwa sana hasa sasa wanadhabi kubwa sana kwani. Jamii inayomzunguka huyu bibi wawe na huruma au ni wanyama yani wanashindwa kukaa kikao wakajadili jinsi ya kumlea mama wa watu wapike chakula kwa zamu kweli hali ngumu kwani wao wanaishije hicho icho kitamtosha na ataridhika, kwani eneo hilo hakuna makanisa/misikiti kweli wanadamu tumekuwa wanyama mi nilivyoona hilo jeneza lake jamani majonzi yamenitoka basi awepo mtu wa huruma apewe simu tumchangie sidhani kama watanzania wote tuna roho mbaya kivile hapana huyu bibi apate mtu apewe mchango apikiwe mwenyewe atafurahia maisha pia tangazeni pakumpelekea nguo tupeleke sio ziende kwa watu wengine Mungu atawaona na kuwalaani Mungu ambariki alieona huyu bibi yetu anavyoteseke labda itakuwa mwisho wa mateso yake - AMINA

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...