Na Sultani Kipingo

Wengi tumesoma  vitabu vya James Hadley Chase (pichani),  mwandishi wa riwaya za kusisimua  maarufu sana wa Uingereza, hasa wakati tukipambana na kujua lugha ya Kiingereza wakati wa shule kidato cha kwanza hadi cha nne, na hata high school.
Nadhani kwa hili hata Profesa Mbele ataniunga mkono ninaposema kuwa utamaduni wa kupenda kusoma huanzia kwenye kuwepo kwa vitabu vya kusisimua kama vya Chase. Na wengi tuliua ndege wawili kwa jiwe moja – yaani kupenda kusoma na pia kujifunza Kiingereza bila shuruti. Au unasemaje Profesa Mbele?
Enzi hizo hamasa ya kusoma vitabu vya riwaya vya Kiingereza ilikuwa kubwa mno kiasi hata kulikuwa na mashindano ya nani kasoma “Chase” nyingi kuliko wenzie. Binafsi nimesoma “Chase” kama 30 hivi, na steringi wangu niliyempenda  sana ni Mark Girland, nikianza na kitabu cha “This is for Real” na baadaye “Have this one on me”, “You have yourself a deal”na “The Whiff of money”. Vic Malloy pia nilipenda visa vyake.

Pamoja na kumsoma sana James Hadley Chase, wengi wetu hatukujisumbua kumjua yeye ni nani, zaidi ya kuburudika na riwaya zake za kusisimua, ambazo nina uhakika zilihamasisha hata waandishi wetu kina Elvis Musiba , Ben Mtobwa,  Hammie Rajabu, Eddie Ganzel ambao sasa wote ni marehemu – ila vitabu vyao bado vingali hai.
Tukirudi kwa James Hadley Chase mstuko wa kwanza utaokupata ni kwamba yeye jina lake halisi halikuwa hilo ambalo alilitumia kiuandishi tu. Jina lake lilikuwa René Lodge Brabazon Raymond. Alitumia pia majina mengine ya kiuandishi kama vile  James L. Docherty, Raymond Marshall, R. Raymond na   Ambrose Grant.
Pamoja na hayo Chase aliibuka kuwa mwandishi mashuhuri wa riwaya, akiwa ameandika jumla ya vitabu 90, na kujulikana kama mfalme wa riwaya za kusisimua barani Ulaya na duniani kote, ambapo riwaya ya vitabu vyake 50 zilichezewa filamu.
René Lodge Brabazon Raymond (James Hadley Chase) alizaliwa Desemba 24,  1906  huko London, Uingereza., akiwa mtoto wa mwanajeshi wa jeshi la kikoloni la India Kanali  Francis Raymond. Huyu baba akiwa daktari wa mifugo, alipania mwanae asomee sayansi pia, na kumpeleka shule ya  King's School, Rochester, huko Kent.
Hata hivyo Chase aliondoka nyumbani akiwa na umri wa miaka 18. Mwaka 1932 alimuoa Sylvia Ray, nao wakajaaliwa mtoto wa kiume. Mwaka 1956 wakahamia Ufaransa, ambapo mwaka 1969 wakaenda kuishi Uswisi, wakiishi  maisha ya kipweke maeneo ya Corseaux-sur-Vevey, katika ziwa Geneva. Chase alifariki huko Februari 6, 1985
Wakati wa vita kuu ya pili ya dunia, Chase alijiunga na jeshi la anga na kupanda vyeo hadi kufikia Kiongozi wa Skwadi (Squardon leader). Huko pia alikuwa akihariri jarida la Jeshi la Anga la Uingereza, na kuandika riwaya kadhaa kutoka humo baada ya vita katika kitabu kilichoitwa Slipstream: A Royal Air Force Anthology.
Baada ya  Chase  kuondoka nyumbani akiwa na umri wa miaka 18, akawa anafanya kazi za kuuza vitabu, hasa vya watoto, katika duka moja la vitabu. Kabla ya kuanza kuandika riwaya, aliwahi kuwa mpiga picha wa kulipwa, na hobby zake kubwa zilikuwa muziki wa classic na opera,
Matatizo ya kiuchumi huko Marekani kati ya miaka 1929 na 1939, iliyopelekea kuwepo na Usongo mkuu (Great Depression) kuliibua makundi mengi ya kijambazi. Hayo na kuchanganya na biashara ya vitabu ya Chase, akagundua kuna fursa ya kuwa mwandishi wa riwaya za kijambazi. 
Na baada ya kusoma kitabu cha James M. Cain cha “The Postman Always Rings Twice cha mwaka 1934, na baada ya kusoma hadithi ya kundi la kijambazi liloongozwa na mwanamke aitwaye Ma Barker na watoto wake, akaandika kitabu chake cha kwanza cha riwaya za kusisimua kilichoitwa “No Orchids for Miss Blandish. Kitabu kilipanda chati sana na kuweza kuwa bora kwa mwongo mzima. Kuanzia hapo kitabu kimoja baada ya kingine kikafuata hadi kufikia 60.

























Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. Dah! Hapa bwana Kipingo whoever ur kwa kweli umenipeleka Ikulu. Kwanza ni kweli sikuwahi kumuona huyu Chase kama alivyo. Pia naomba hata Profesa Mbele hajajibu nikwambie kwamba siku hizi watu wanadhani mtandao ndio mwisho wa matatizo ya kusoma. Zamani usipotoa stori za Chase kijiweni wewe ulikuwa unaonekana fala tu. Uzuri wa mada hii ni kwamba mtu mavitabu ya elimu (text books) pekee hupati stimulation ya kusoma hata mistari miwili. Sie shuleni kila Ijumaa ulitakiwa ulete review ya kitabu ulichosoma cha hadisi.Sijui kama ipo siku hizi. Ila the bottom line ni kwamba ili kurejesha utanmaduni wa kusoma vitabu lazima usome vitabu vya kusisimua kama Chase. Mitaani vipo kibao. JARIBU UONE!!

    ReplyDelete
  2. Asanteni kwa kunikumbuka. Namshukuru Sultani Kipingo kwa makala yake. Nami imenikumbusha mbali.

    Nilipokuwa nasoma Mkwawa High School, 1971-72, hali ilikuwa hivyo hivyo alivyoelezea Sultani Kipingo kuhusu kupendwa kwa riwaya za James Hadley Chase. Kwa kweli, sina la kuongeza.

    Nakushuru pia ndugu "anonymous" kwa hayo uliyosema. Tuko pamoja.

    ReplyDelete
  3. Thanks to African Writers Series, David Maillu ( My dear Bottle) After four Thirty and many more, and Chase. I remember his writing he was so descriptive, he described streets so well, especially parts of the USA. Seriously technology has served us well, but it has also robbed us of imagination.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...