Ndugu zangu,
Msafara wa tembo huwa na kawaida ya kutokurudi nyuma,ndio maana porini huzioni nyayo za tembo zenye kwenda mbele na kurudi nyuma.
Ni ukweli, kuwa tembo ndiye mnyama mkubwa porini, na ni mfalme wa pori. Lakini tembo hufika mahali akasumbuliwa na siafu kiasi cha kuweweseka na hata kutamani kulihama pori. Ni kwa kosa la tembo kukanyaga kichuguu cha siafu. Naam, siafu mia tano ni wengi kuliko tembo mmoja, pamoja na ukubwa wa tembo.
Na adili ya jambo hilo ni ukweli kuwa duniani hapa mkubwa anapaswa kumuheshimu mdogo, na mdogo pia kumuheshimu mkubwa.Hivyo, wanadamu tunapaswa kuheshimiana.
Kwenye hili la hofu ya mkwamo wa mchakato wa Katiba nayaona mapungufu mawili kwa pande zinazohusika; KUTOHESHIMIANA na KUTOAMINIANA.
Kwenye awamu ya kwanza ya Bunge Maalum la Katiba mawili hayo yalijidhihiri. Hakika UKAWA na CCM kwa pamoja wamebeba dhamana kubwa ya hatma ya nchi yetu. Kuna makosa yameshafanyika tangu kuanza kwa mchakato huu. Hatupaswi kama taifa kuwa kama tembo kwenye msafara wao, kwamba hawarudi nyuma.
Kabla ya kuendelea na mchakato huu wa Katiba, kama taifa, na kwa kupitia viongozi wakuu wa UKAWA na CCM. Viongozi hao, kwa namna yeyote ile, wana lazima ya kujiandalia au kuandaliwa mazingira ya kukaa meza moja kama Watanzania. Kuendelea kufanya vikao vya siri na kuyapitia mapungufu yaliyojitokeza kwenye Awamu ya kwanza, kisha watoke kwa pamoja na kwa kauli moja ya namna ya kwenda mbele.
Wakishindwa kukaa meza moja,basi,ni heri mchakato mzima ukahairishwa kusubiri wakati muafaka, kuliko kusonga mbele kwa staili ya msafara wa tembo, maana, huko njiani kutakuwa na vichuguu vingi vya siafu vitakavyokanyagwa, na tembo pamoja ukubwa wao, wataweweseka sana porini, na hata kusababisha pori lichafuke. Pori kukosa amani.
RAI YANGU: Kinachoonekana kwa sasa ni kwamba CCM hawako tayari kwa Serikali Tatu, kuna mengine basi, ya muhimu kwa nchi, ambayo CCM wako tayari nayo. Na UKAWA nao hawako tayari kurudi bungeni kwa kujadili Serikali Mbili, kuna mengine pia UKAWA wako tayari nayo na muhimu sana kwa taifa. Na katika dunia hii, si yote anayotaka mwanadamu anayapata katika wakati huo huo anapoonyesha kuyataka, mengine husubiri.
Na kubaki kuelekeza lawama kwa Rais wa nchi na hata kumtaka aombe radhi kwa wananchi hilo nalo haliwezekani na ni kuendelea kupoteza muda. Pamoja na kuwa Urais ni taasisi, lakini, Rais naye ni mwanadamu kama wengine, si malaika, na ni MwanaCCM pia, si Mwana UKAWA.
Na katika dunia tunayoishi, yumkini kuna UKAWA ndani ya CCM na CCM ndani ya UKAWA. Hivyo,yawezekana haya tunayoyashuhudia si mepesi sana. Si mepesi maana hata kuamini kuwa Bunge liendelea na UKAWA warudi Bungeni ina maana ya kuendelea kwa malumbano na ushindani wa CCM na UKAWA. Ni kwa vile itakuwa na tafsiri ya kuendelea kuwepo Bungeni kwa wajumbe wa ' Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi' dhidi ya ' CCM'. Nao watakuwa wakitetea Katiba ya nani? Ni mazungumzo tu ya pande mbili katika mazingira ya kuheshimiana na kuaminiana ndiyo yanapaswa kuandaa mazingira ya wajumbe wa Barazala Katiba kurudi Bungeni kwa maslahi ya taifa na si makundi yao.
Na zaidi, tumwamini Rais wetu katika dhamira yake ya kuanzisha mchakato wa kupata Katiba Mpya. Tumsaidie pia, maana, yumkini, Katiba Mpya ni moja ya mambo anayotaka kuyaacha nyuma yake na akumbukwe nayo-legacy.
Hivyo, tulikofikia ni mahali ambapo kila mzalendo wa nchi hii anapaswa kujisikia huzuni na hata kujutia. Tulikofikia hakuna mshindi, sote tumeshindwa, kama taifa. Maana, tumetumia rasilimali nyingi kama taifa, muda na fedha . Mchakato huu kukwamia hapa ni aibu kwa taifa. Na wahenga walisema; majuto ni mjukuu, na kwamba yaliyopita si ndwele, tugange yajayo.
Kongamano la Kitaifa la Katiba lililoandaliwa na Baraza la Vyama Vya siasa, liwe ni fursa ya kutukwamua kutoka tulikokwama, hivyo, kusonga mbele kwa KUHESHIMIANA na KUAMINIANA. Ndio,kongamano hilo litoke na ' AZIMIO LA DODOMA' la kusonga mbele kama taifa.
Ni Neno La Leo.
Maneno yako mazima nchi hii ina viongozi wastaafu wa chama cha ccm kwa nn wasisuluhishe kuliko mzigo wote wa lawama kuachiwa rais peke yake na wao wawemo katika kusuluhisha
ReplyDeleteCCM wana wasiwasi wa bure tu na serikali tatu. Bado hata zikija s3 au 10 ccm ndo wataibuka washindi, tena kwa kila serikali. Nawasihi waachane na mawazo ya kizamani wakubaliane na matakwa ya wananchi.
ReplyDeletehao ukawa ni wapumbavu kabisa hawataki amani wanakaa kuchochoe kutokuelewana tuu agrrrrrrrrrr damn you ukawa laiti baba wa taifa angelikuwapo.
ReplyDelete