Mkuu wa wilaya ya Hai Mhe. Novatus Makunga ameeleza kuwa serikali wilayani humo imejipanga kuondoa kero zote zinazoawakabili wananchi wanapoenda kutibiwa katika hospitali ya serikali ya wilaya hiyo zikiwemo lugha chafu za watumishi wa hospitali hiyo 
Mhe.  Makunga ametoa kauli hiyo katika mikutano yake ya hadhara na wananchi wa mitaa ya Kingereka na Kibaoni katika kata ya Hai Mjini. 
 Awali wananchi wa mitaa hiyo walieleza kuwa kero kubwa wanayokumbana nazo katika hospitali hiyo ni pamoja na lugha chafu katika eneo la mapokezi,ukosefu wa dawa pamoja na madaktari kutokaa katika vyumba vyao vya kuwahudumia wagonjwa. 
 Mkuu huyo wa wilaya ameeleza kuwa hatua za awali zimeshaanza kuchukuliwa ikiwemo kuanzisha mpango unaojulikana kama sauti ya jamii ambapo kupitia mpango huo wananchi wanaokumbana na kero katika hospitali hiyo wamekuwa wakitoa taarifa. 
 "Taarifa hizo zimekuwa zikijadiliwa na kamati ya uongozi ya hospitali hiyo kila mwezi na kuchukuwa hatua na baadaye mrejesho kutolewa kwa wananchi,hivyo zote kwa pamoja tupambane na uvunjaji wa maadili katika hospitali yetu" alisema Makunga 
 Aidha amewataka wananchi hao kutoa taarifa mara moja pale wanapokumbana na kero yoyote kwa mganga mkuu wa wilaya ama mganga mfawidhi ama muuguzi mkuu na hata yeye kama mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ambapo wote hao walitoa nambari zao za simu za mkononi. “Tumeanza kuchukuwa hatua na itakuwa vyema pale unapokumbana na kero kutuletea taarifa hapo hapo bila ya kuchelewa,sasa wakati umefika wa kuambiana ukweli,kama mtu anaona kuhudumia umma kunampotezea wakati basi akaanzishe zahanati yake ambapo huko atakuwa huru kutumia lugha chafu,”aliongeza Makunga 
 Ameeleza maboresho makubwa yaliyofanywa na serikali katika hospitali hiyo hayatakuwa na maana endapo kero hizo zitaendelea kudumu na kusababisha wananchi kupata huduma kwa mateso makubwa. Makunga amezitaja huduma zilizoboresha kuwa ni pamoja na upasuaji mkubwa kwa kuwa na chumba cha kisasa,ukamilishaji wa wote ya upasuaji pamoja na kukamilishwa kwa huduma za X-Ray ambayo itafunguliwa rasmi na mwenge wa uhuru mnamo tarehe 22 ya mwezi huu
 Kwa upande wake mganga mfawidhi wa wilaya ya Hai,Dk Fanuel Mollel alikiri kwamba huko nyuma kulikuwa na tatizo kubwa la madaktari wa hospitali hiyo kutumia muda mrefu kwenda kunywa chai kwa kutoka pamoja kwa makundi na hivyo kusababisha wagonjwa kusota kwa muda mrefu.
 Amesema hatua za kudhibiti tabia hiyo zimeshachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuanzisha kantini eneo la hospitali hiyo. 
 Kuhusiana na upungufu wa dawa ameeleza hali hiyo inatokana na taratibu za serikali ambapo kwa sasa zinataka dawa ziagizwe kutoka katika bohari kuu ya madawa(MSD) ambapo mara nyingine ukumbwa na upungufu wa dawa

Wananchi wa mitaa ya Kingereka na Kibaoni katika kata ya Hai Mjini wakiwa katika mkutano huo
Mkuu wa Wilaya ya Hai Mhe.  Novatus Makunga akikabidhi kadi kwenye  mkutano wake wa  hadhara na wananchi wa mitaa ya Kingereka na Kibaoni katika kata ya Hai Mjini. 
Mganga mfawidhi wa wilaya ya Hai,Dk Fanuel Mollel akiongea na wananchi
Mkuu wa Wilaya ya Hai Mhe.  Novatus Makunga akiongea mkutano wake wa  hadhara na wananchi wa mitaa ya Kingereka na Kibaoni katika kata ya Hai Mjini. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...