Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia Baraza Kuu la 69 la Umoja wa Mataifa siku  ya Alhamisi ambapo pamoja na  masuala mengine alitoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa wa    kutoinyanyapa Afrika    kwa sababu ya Ebola na kusisitiza kuwa Afrika ni  Bara la lenye nchi 53 na  kwamba si   nchi zote zenye Ebola kauli iliyopigiwa makofi na wajumbe wa Baraza Kuu la 69 waliokuwa wakimsikiliza ikiwa ni  ishara ya kuunga mkono kauli yake.

Na Mwandishi Maalum, 
New  York
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.   Jakaya Mrisho Kikwete ameungana na viongozi wengine duniani  katika  kuichagiza Jumuiya ya  Kimataifa  kuzisaidia  Liberia, Siera Leone na Guinea  mataifa ambayo yameathirika   vibaya  na mlipuko wa Ugonjwa wa Ebola. Amesema  misaada inayopelewa  na itakayopelewa katika nchi hizo    inatakiwa kuwa endelevu na ya uhakika hadi pale ugonjwa huo utakapodhibitiwa.

Rais Kikwete ametoa wito huo siku ya alhamisi wakati alipokuwa akilihutubia Baraza Kuu la 69 la  Umoja wa Mataifa  katika majadiliano ya jumla  ( General Debate) yaliyoanza siku ya  jumatano hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa. Akaongeza  pia kwamba   nchi za Afrika ya Magharibi na nyingine barani Afrika  zinatakiwa    kujengewa uwezo ukiwamo wa namna ya kuchunguza ugonjwa huo,  kuwa na maeneo maalum ya wagonjwa  pamoja na huduma za matibabu. Kwa mujibu wa Rais Jakaya Kikwete  juhudi zaidi zinatakiwa kufanyika za kufanikisha  upatikanaji wa tiba ya uhakika ya ugonjwa huo, tiba ambayo amesema itasaidia pia kuimarisha afya za wale ambao tayari wameathiria.

Akizungumzia zaidi kuhusu mlipuko wa Ebola na athari zake,  Rais  ametaka  kuwapo kwa ushirikiano  ndani ya  jumuiya ya  kimataifa hususani nchi   zenye uwezo mkubwa wa kifedha na utaalam ili  kwa umoja wao waweza kuwasaidia wanasayasi ambao  wanaendelea na   jitihada za kutafuta tiba na chanjo ya ugonjwa  wa Ebola. Pamoja na  kutaka  mataifa  yaliyoathirika na Ebola kusaidiwa kwa hali na mali,  Rais wa Jamhuri ya Muungano  wa Tanzani ameitaka pia Jumuiya ya Kimataifa  kutoinyanyapaa Afrika  kwa sababu ya Ebola.

Akasema  taarifa za kuwapo kwa watu wanaofuta au kuahirisha safari zao za kwenda   Afrika eti kwa sababu ya Ebola zinasikitisha.“Umoja wa Mataifa na  Marafiki wa Afrika,saidieni kuwaeleza  kwamba Afrika  ni  Bara lenye nchi 53.Afrika siyo nchi moja,  Nchi nyingi ziko mbali sana na  nchi  nchi ambazo zimeathirika kwa Ebola. Na kwa  kweli pengine nchi  zilizoathirika ziko  karibu zaidi na   Ulaya kuliko mataifa mengine ya Afrika”.

Akaongeza  “Tusaidieni kupaza sauti ya Afrika ya kutonyanyapaliwa kwa sababu ya Ebola” akasema  Rais.   Kauli  iliyopigiwa makofi na wajumbe waliokuwa wakimsikiliza.

Katika hotuba yake  pamoja na kuuzungumzia kwa  kina  mlipuko wa  Ebola, Rais Kikwete pia alizungumzia  kuhusu maeneo mengine muhimu  hususani katika Usalama wa  Kimataifa, ambapo aligusia matukio ya kigaidi yanayoendeshwa na makundi kama  Al Shaabab, ISIS na Boko Haram   katika   maeneo mbalimbali na kwamba makundi hayo hayapashwa kuachwa kuendelea na uovu wao.

Akayataja  maeneo mengine ambayo yanaendelea kuifanya dunia kutokuwa mahali salama  kuwa ni pamoja na  mwendelezo  wa uvunaji haramu wa mali asili, uwindaji haramu,  biashara haramu ya dawa za kulevya na silaha. Aidha  ametoa wito wa kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu wa  migogoro inayoendelea  huko Libya,  Jamhuri ya  Afrika ya Kati na  Sudani ya Kusini. Kuhusu Palestina Rais amesema  dunia haihitaji kusubiri zaidi hasa  kutoka na mikasa ambayo imesababisha  maisha ya watu wasiokuwa na hatia wakiwamo watoto, wanawake na wanaume kupotea bila sababu.

Na kwa sababu hiyo ametoa wito wa Umoja wa Mataifa, Marekani, Urusi na  Mataifa ya  mengine ya Ulaya yafikie mahali  pa kuutafutia ufumbuzi wa kudumu mgogoro  kati ya  Palestine na Israel jambo alilosema kuwa linawezeka.

Kwa upande wa Sahara ya Magharibi ambalo ni koloni pekee barani Afrika, Rais Kikwete ameiutaka   Umoja  wa Mataifa na wadau wengine kulitafutia ufumbuzi ili nalo lifike tamati.Rais pia alizungumza tatizo la muda mrefu la vikwzo vya kiuchumi ambavyo imewekewa Cuba, akazungumzia pia   tatizo na changamoto  ya mabadiliko ya Tabia nchi,na  mchakato wa maandalizi ya malengo mapya ya maendeleo endelevu ambayo alisema Tanzania  iko tayari kushirikiana na  mataifa mengine katika eneo hilo.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 6 mpaka sasa

  1. Ugonjwa huu ni janga unaopashwa kuhamasisha waafrika wote kuboresha vituo vyetu vya afya.

    ReplyDelete
  2. SIJAMSIKILIZA AKIZUNGUMZA; KATUMIA LUGHA YETU? MANAKE SIYE NI WASWAHILI. KILA MMOJA NA LUGHA YAKE; KUWA NA LUGHA SI DHAMBI

    ReplyDelete
  3. Sawa kabisa mdao wa kwanza. Halafu rais anasema Afrika isinyanyapaliwe kwa sababu ya Ebola. Watu wanaogopa na huku majuu hawajui hata Afrika bora rais kaelezea ila bado wezetu wa majuu kuelewa si rahisi. Waliona wale wagonjwa wa Ebola walivyoletwa huku marekani walivyofunikwa kama nusu maili ni ngumu sana kuelewa. Na kuzingatia hatuna vituo vya afya vya kueleweka ni shida tupo

    ReplyDelete
  4. Magonjwa mengi yanaletwa na tabia za watu wa eneo husika. Ebola imeletwa na ulaji wa nyama pori hususan nyama ya nyani ambayo ni maarufu Africa magharibi na Africa ya kati. Ugonjwa wa SAR uliletwa na ulaji nyama ya paka China. Magonjwa mengine yako kwa wanyama tu, yakiingia kwa binadamu huwa ni maafa na kwa kuwa Ebola ni ugonjwa wa Africa, huchukua muda kwa Dunia ku-react kama tunavyoshuhudia.

    ReplyDelete
  5. Mdau wa nne hapo juu fanya utafikti kikamilifu kwanza kabla ya kufikia hitimisho kuhusu chanzo cha magonjwa hayo!!

    Jambo moja ambalo hatujaliweka vizuri hapa Afrika ni utegemezi wetu uliokithiri kiasi kwamba tunaweza kutoweka wote kama likitokea tatizo kubwa. Hatuwekezi kwenye maarifa na tafiti ya kutufanya tuwe self-reliant! Tatizo kidogo tu tunaomba jumuia ya kimataifa! Na huu ni uzembe wetu sisi wenyewe kwa kukosa visheni ya Bara letu. Hatuweki nguvu zetu pamoja kwenye kupanga! Utamsikiliza kila kiongozi wa Afrika akisimama anaongea mambo tofauti na mwingine, wakati sisi watawaliwa katika Afrika tuna mambo yanayofanana katika kujikwamua kwenye hizi changamoto tulizonazo! Sasa AU inakazi gani kama sio kwenda kujenga hoja ya pamoja? Enzi za Mwalimu, nchi za Afrika zilikuwa zinaenda UNO na ajenda moja, au zinazoshabihiana! Lakini kwa bahati mbaya sasa hivi inaonekana kana kwamba hawa watishi wametugawa kiasi kikubwa hadi baadhi ya viongozi wanapenda kutowaudhi wakubwa, hivyo wanaongea lugha laini.

    We have common challenges but different voices! Nakumbuka Enzi za Thomas Sankara!!

    ReplyDelete
  6. Mataifa makubwa yataendelea kututawala hata kama tumepata uhuru,Uhuru wa nchi za kiaafrika Utabaki kuwa wa nadharia kwani hakuna dalili ya kujiondoa katika utegemezi na uegemezi wa mataifa haya. Na hakika hatutakuwa na wakumlaumu isipokuwa sisi wenyewe kwa kushindwa kusimamamia rasilimali zetu vyema kwa manufaa yetu wote.viongozi wa Africa wanakula mpaka wanasahau kutenga budget ya maafa. Kila kukicha kunapiga foleni na bakuli mkononi tukiomba misaada wakati tunarasilimali lukuki. Hata tukichekwa,au kusimangwa ni haki yetu.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...