Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imekutana leo (Septemba 7 mwaka huu) na kupitia masuala mbalimbali ikiwemo mgogoro wa kimkataba kati ya klabu ya Yanga na mchezaji Emmanuel Okwi (pichani kushoto akipokea jezi baada ya kusajiliwa na Simba). 
Mkataba huo ulipitiwa na Kamati ikiwemo kumsikiliza mchezaji mwenyewe pamoja na upande wa Yanga, na kuridhika kuwa mkataba kati ya pande hizo umevunjika. Ukiwa ni mkataba wa pande mbili, Yanga ilikiuka kipengele namba 8 kuhusu malipo ya ada ya usajili.
 Yanga ikiwa mwajiri, haikutekeleza kipengele hicho cha kimkataba hadi kufikia Juni 27 mwaka huu ilipoandika barua TFF kuomba mkataba huo uvunjwe. Kwa maana hiyo Okwi ni mchezaji huru, hivyo yuko huru kujiunga na timu yoyote. 
Mkataba ni uhusiano kati ya mwajiri (Yanga) na mwajiriwa (Okwi), ambapo Kamati imebaini kuwa uhusiano huo haupo, hivyo hakuna mazingira ya pande hizo mbili kuendelea kufanya kazi pamoja. 
Pamoja na Yanga kuwasilisha pingamizi la kuwepo mmoja wa wajumbe katika kikao kwa sababu za kimaslahi (conflict of interests), walifahamishwa kuwa kilichopo mbele ya kamati ni mgogoro wa kimkataba kati ya Yanga na Okwi, na si usajili. 
Pia lilijitokeza suala la Okwi kutakiwa na klabu ya Wadi Degla ya Misri. Kamati imeiagiza Sekretarieti ya TFF kulifanyia uchunguzi suala hilo na kulitolea taarifa katika kikao kijacho. 
Hata hivyo mjumbe huyo hakushiriki katika kuchangia hoja na kutoa maamuzi. Uamuzi wa kamati ulifanyika baada ya majadiliano, hivyo hakukuwa na suala la kupiga kura. 
Kuhusu pingamizi la Coastal Union kwa Abdi Banda, Kamati imebaini kuwa klabu hiyo imevunja mkataba kati ya pande hizo mbili kwa kushindwa kumlipa mchezaji huyo mshahara wa miezi mitatu mfululizo kama takwa la mkataba. 
Klabu ya Coastal Union iliwakilishwa na mmoja wa viongozi wake, wakati Banda aliwakilishwa na mwanasheria wake. 
Vilevile Kamati imekubaliana na pingamizi la Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro (MRFA) kuhusu wachezaji waliofanyiwa uhamisho kutoka katika mkoa wake bila kulipiwa ada za usajili, hivyo klabu husika zinatakiwa kulipa ada hizo. 
Pia Kamati imeagiza klabu zote zilizosajili wachezaji bila kuwafanyia uhamisho, kulipa ada za uhamisho kwa pande husika kabla ya kuanza ligi, vinginevyo leseni zao zitazuiwa hadi watakapolipa.
Mashauri mengine ya pingamizi yatasikilizwa baadaye kwa vile klabu husika hazikupata fursa ya kufika mbele ya kamati.Kamati inasisitiza kwa wanachama wa TFF kuheshimu mikataba.

BONIFACE WAMBURA
KAIMU KATIBU MKUU
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 5 mpaka sasa

  1. Hii Virus iliyoingia kwa wasomi wetu wa sheria itaendelea kuligharimu taifa.Shida ya kusaini mikataba bila kuielewa vyema haiishii tu kwa viongozi wetu wa siasa,wakuu wa mashirika sasa hata vilabu vya michezo ni wahanga wa Virus hii..Feel sorry 4 u Yanga,mamilioni ndio hayo yameshaondoka kirahisi kabisa...

    ReplyDelete
  2. NI SAKATA LINALOTUFEDHEHESHA WATANZANIA KATIKA UKANDA HUUWA AFRIKA MASHARIKI NA LINATHIBITISHA NI JINSI GANI TULIVYO MAMBUMBUMBU. ANZIA HUYU MCHEZAJI ALIVYOUZWA KWA WATUNISIA BILA TIMU ILIYOMUUZA KUAMBULIA CHOCHOTE MWAKA JANA IKARIPOTIWA KWAMDA WATUNUSIA WAKO TAYARI KUMRUDISHA HUYO NCHEZAJI KWA TIMU ILIYOWAUZIA WAUNGWANA WAKAGOMA, WAKATOKEA VILAZA WENGINE WA KUFIKIRI INGAWA WAMEJALIWA UWEZO WAKAMTWAA KWA MBWEMBWE WALIOMUUZA KWA WAARABU WAKAKASIRIKA SANA WAKAWEKA MAPINGAMIZI WAKASHINDWA LEO HII WALIOMTWAA KWA MBWEMBWE WAMEZINGULIWA WALIOMUUZA BILA KUAMBULIA CHOCHOTE NA KUKATAA KURUDISHIWA MCHEZAJI WAO WAMEAJILI KWA MBWEMBWE KWA SABABU TU ZA ITIKADI SIDHANI KAMA HII INAWEZA KUTOKEA KWENYE NCHI NYINGINE YOYOTE YA UKANDA HUU. USHAURI: WALIONGIZWA MJINI WATULIE HAKUNA HAJA YA KUENDELEA KUPOTEZA KWA VILE SIKU ZOTE WANASEMA CHA MLEVI HULIWA NA MGEMA. POLE KANJIBHAI AMBAYE BINAFSI SIAMINI KAMA KWELI ANA NIA YA KUINDELEZA TIMU ANAYOIONGOZA

    ReplyDelete
  3. Simba na Yanga mnapoteza muda mwingi kwenye masuala ya 'kitoto'.Angalia timu mbili za Congo DR(TP Mazembe na AS Club Vita zilivyoingia nusu fainali ya ORANGE CAF CHAMPION LEAGUE.Tunataka kusikia Yanga na Simba ziko Nusu Fainali ya ORANGE CAF CL.

    David V

    ReplyDelete
  4. Philemon MuhanuziSeptember 08, 2014


    Nauonea huruma sana mpira wa miguu Tanzania...namuonea huruma kila kocha wa timu ya ligi kuu, kwani wanajikuta wakilazimika kufanya kazi na viongozi wenye uelewa mdogo sana kuhusiana na kile wanachokifanya. Taifa Stars hujengwa na vilabu bora na vilabu bora huongozwa na watu wenye umakini katika kazi zao.....hata wakija akina ferguson, mourinho na anchelloti bado watalazimika kufanya kazi na hawa viongozi duni tulionao

    ReplyDelete
  5. Huyu Okwi ana CV mbaya africa nzima na hajulikani kokote duniani, nashindwa kuelewa vilabu vyetu mbumbumbu vya simba na Yanga vinavyompa jina huyu mtu . Kila kukicha ni habari zake na tunashindwa kujadili mambo ya muhimu

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...