Mfuko wa Maendeleo ya jamii TASAF umeanza kuwajengea uwezo wataalamu ngazi
ya Kata kutoka mamlaka nane za utekelezaji wa mpango wa Kunusuru Kaya Maskini
na kuwawezesha walengwa wa Mpango wa kunusuru kaya masini kuibua miradi
inayoweza kutekelezeka ndani ya kipindi kifupi katika mpango wa miradi ya ajira
kwa walengwa (Public Works Project kwa lengo la kuwaongezea kipato).
Akifungua warsha ya kuwajengea uwezo wataalamu hao mjini Bagamoyo mkoani
Pwani, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bwana Ladislaus Mwamanga amesema
miradi ya ujenzi itakayoibuliwa na walengwa wa Mpango wa kunusuru kaya maskini
itatekelezwa sambamba na Mpango wa uhawilishaji fedha kwa walengwa jambo
litakalosaidia kaya hizo kuongeza kipato
hususan wakati wa kipindi cha hari.
Bw. Mwamanga ameeleza kuwa lengo kuu la mpango huo ni kuhakikisha kuwa
wananchi wa Tanzania wanaondokana na umaskini ili waweze kumudu mahitaji yao muhimu
kama vile kupata huduma za elimu, afya na lishe.
"Utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini haulengi tu katika
kuhawilisha fedha kwa walengwa bali pia unahimiza ushiriki wa walengwa katika
kazi za mikono kupitia miradi ya mbalimbali katika maeneo yao ili waweze kupata
kipato, na kuwekeza" amefafanua Bw. Mwamanga.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa miradi wa TASAF Amadeus Kamagenge amesema
Mpango huo ni muhimu kwa vile unatoa fursa ya ajira kwa walengwa katika Kaya
Maskini, unawezesha kaya za walengwa kupata kipato zaidi, unawapataia walengwa
weledi na stadi za mbalimbali wakati wa utekelezaji miradi, unawezesha jamii
husika katika maeneo ya utekelezaji kuweza kuwa na rasilimali kama barabara
ambazo hubaki na kuendelea kutumika pamoja na kujenga moyo wa kufanya kazi ili
jamii iweze kutoka katika umaskini.
Awali, Mtaalamu wa Mazingira toka TASAF Makao Makuu Bw. Barnabas Jachi
alizitaja mamlaka za utekelezaji zitakazoanza kutekeleza mpango huo kuwa ni za
Bagamoyo, Kibaha, Chamwino, Mtwara Manispaa, Lindi Manispaa na halmashauri ya
wilaya ya Lindi.Warsha hizo zitafanyika katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa
ni mkakati maalum wa TASAF kujenga uwezo wa kitaalamu katika maeneo ya
utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini
PSSN.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Ladislaus Mwamanga
akifungua warsha ya kuwajengea uwezo wataalamu wa kisekta Mjini Bagamoyo.
Mkurugenzi wa Miradi wa TASAF Bw. Amadeus Kamagenge
akielezea manufaa ya mpango unaotoa fursa ya ajira kwa walengwa wa mpango wa
kunusuru kaya maskini PSSN kwa lengo la kuwaongezea fursa za kipato.
Mtaalamu wa Mazingira toka TASAF Makao makuu Barnabas Jachi akitoa
maelezo ya awali juu ya warsha ya kuwajengea uwezo wataalamu wa kisekta.
Picha hii na mbili zinazofuatia ni Washiriki wa Warsha ya
kuwajengea uwezo wataalamu wa kisekta (katika makundi tofauti) wakiwa katika
picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Ladislaus Mwamanga
(katikati waliokaa) Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Miradi TASAF Bw. Amadeus
Kamagenge
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...