Kufuatia kifo cha Rais Michael Chilufya Sata, kilichotokea tarehe 28 Oktoba 2014, mjini London, na kwa kuzingatia Katiba yake Kifungu cha 38 (1) kinachohusu mamlaka ya Rais, kwamba nafasi ya Rais ikiwa wazi kwa sababu yoyote ile, Makamu wa Rais atakaimu madaraka ya kiti cha Urais hadi uchaguzi mdogo utakapofanyika ndani ya siku tisini (90), hivyo Serikali imemteua Mhe. Guy Scott (MB), Makamu wa Rais, kukaimu nafasi hiyo katika kipindi hiki cha mpito.

Tayari aliyekuwa anakaimu madaraka ya Urais, Mhe. Edgar Lungu (MB) ameshamkabidhi madaraka hayo. 

Hadi sasa kulingana na taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, bado haijafahamika maombolezo rasmi yataanza lini na kwa siku ngapi au mazishi yatafanyika lini. Haya yote yanategemea maamuzi ya kikao cha Baraza la Mawaziri ambacho kinakutana hivi sasa.

Hizi ni taarifa tunazoendelea kupokea, hivyo nasi tutaendelea kuwataarifu kwa kadri tunavyozipata.

UBALOZI , LUSAKA , ZAMBIA

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameshtushwa na kusononeshwa sana na taarifa za kifo cha Rais wa Jamhuri ya Zambia, Mheshimiwa Michael Chilufya Sata ambacho kimetokea jana, Jumanne, Oktoba 28, 2014 kwenye Hospitali ya King Edward VII, London, Uingereza, ambako alikuwa anatibiwa akiwa na umri wa miaka 77.
Katika salamu ambazo amempelekea Makamu wa Rais wa Zambia, Mheshimiwa Dkt. Guy Scott kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Rais Kikwete amesema:
“Nimepokea kwa mshtuko mkubwa na huzuni nyingi, habari za kusikitisha za kifo cha Mheshimiwa Michael Chilufya Sata, Rais wa Jamhuri ya Zambia. Kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na hakika, kwa niaba yangu mwenyewe, napenda kukutumia wewe Mheshimiwa salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu, na kupitia kwako familia ya wafiwa na ndugu wa Hayati Rais Sata pamoja na Serikali na ndugu zetu wananchi wote wa Zambia kufuatia msiba huu wa ghafla.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Hayati Sata atakumbukwa daima kama mmoja wa viongozi wa mfano wa kuigwa katika Afrika. Katika kipindi chake kifupi cha uongozi wa juu wa Zambia, alifanikiwa kuleta mageuzi makubwa katika maisha ya wananchi wengi wa Zambia. Atakumbukwa pia kwa imani yake isiyoyumba ya kupigania uhuru, haki na usawa, sifa ambazo zilimfanya kiongozi mpendwa ndani na nje ya mipaka ya Jamhuri ya Zambia.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Hivyo, huyu ni kiongozi ambaye siyo tu atakumbwa na wananchi wa Zambia lakini atakumbukwa na sisi sote wenzake na watoto wote wa Afrika.”
“Katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na huzuni, tunaungana nanyi kuomboleza na kumwomba Mwenyezi Mungu awape nguvu na subira wana familia ya wafiwa, jamaa na ndugu zetu wote wa Zambia ili waweze kuhimili machungu ya kipindi hiki cha msiba mkubwa. Aidha, tuko pamoja nanyi katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke pema roho ya Marehemu Michael Chilufya Sata.”
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
29 Oktoba,2014.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 6 mpaka sasa

  1. waafrika watu wapole sana. weusi kupata hata uongozi wa mtaa ulaya hakuna. ila sisi hatuoni tatizo kwa wazungu, wahindi, warabu, na baadaye wachina kushika nafasi nyeti za uongozi wa nchi.

    upole wetu ndo ulifanywa tukawa watumwa na kukolonishwa.

    ReplyDelete
  2. we wacha ubaguzi huo,mbona weusi wengi tu ni viongozi ulaya na uarabuni .

    akili finyu,

    ReplyDelete
  3. Wapo wakenya, wakongo, walioshika nafasi za uongozi ulaya, gombania kama unakidhi taratibu zao. Mzambia mweupe kama kakubalika sisi ni nani tumseme?

    ReplyDelete
  4. Mawazo yako yamepitwa na wakati!
    Obama mjaluo USA
    Monem Mwarabu Ex president Argentina(Marekani ya kusini).

    Watu wanachagua kiongozi anayefaa sio ngozi au kabila au dini inabakia longolongo miaka 5 maendeleo nyuma miaka 100

    ReplyDelete
  5. Si kweli mbona obama mkenya anatawala marekani wapo wengi wanaongoza mitaa ulaya tuacheni ubaguzi

    ReplyDelete
  6. Nakubaliana nawe, pengine usemayo yana kina. Lakini ningependa kukukumbusha kuwa the most powerful man in this planet at this moment ni mmatumbi, hivyo the future will possibly be different.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...