Na. Ally Mataula – Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Baraza la Maadili limetoa amri ya kukamatwa mara moja Mkuu wa Wilaya ya Korogwe
Mhe. Mrisho Gambo kwa kukaidi wito wa kufika mbele ya Baraza hilo kujibu tuhuma
zinazomkabili.
Akizungumza baada ya kuahirisha kikao cha Baraza hilo lililoanza vikao vyake tarehe
9/10/2014, Mwenyekiti wa Baraza la Maadili Mhe Balozi Jaji (Mst.) Hamisi Msumi
alisema kuwa amri hiyo imetolewa kwa mujibu wa fungu la 24 (4) la Sheria ya Maadili
ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya 1995 ambayo imempa mamlaka Mwenyekiti wa Baraza
hilo kutoa amri ya kukamatwa Kiongozi yeyote atakaekaidi wito wa kufika mbele ya
Baraza na kwa mujibu wa fungu hilo amri hiyo itatekelezwa na Afisa wa Polisi.
Kiongozi huyo ambaye anatuhumiwa kwa makosa ya matumizi mabaya ya Madaraka
aliitwa mbele ya Baraza hilo ili aweze kujibu tuhuma zinazomkabili.
Baraza la Maadili limeanza vikao vyake ambapo mashauri 19 ya viongozi wa kada
mbalimbali wanaotuhumiwa kikiuka Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa
kutumia vibaya madaraka yao na kushindwa kuwasilisha Tamko la Mali na Madeni
yatasikilizwa.
Vikao hivyo vya Baraza la Maadili vinafuatia kukamilika kwa uchunguzi wa awali
uliofanywa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuhusu tuhuma za
ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma dhidi ya Viongozi husika.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma
Baraza hilo litaendelea na vikao vyake mpaka tarehe 17/10/2014.
Mwenyekiti wa Baraza la Maadili Mhe. Balozi Jaji (Mst.) Hamisi Msumi katikati akiwa
na Wajumbe wa Baraza hilo Bibi Selina Wambura kushoto na Bibi Hilda Gondwe kulia
kabla ya kuanza kusikiliza Mashauri ya ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa
Umma yaliyowasilishwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bw. Hassan Mayunga
akifafanua jambo mbele ya Mwenyekiti wa Baraza la Maadili Mhe. Jaji Hamis Msumi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...