Na Saidi Mkabakuli

Ugeni kutoka Tume ya Mipango na Maendeleo ya China imevutiwa na kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania hali inayochochewa na mipango thabiti ya kuvutia uwekezaji hasa kwenye Maeneo Maalum ya Kiuchumi (SEZs).

Akizungumza wakati wa kikao cha pamoja na viongozi wa Tume ya Mipango ya Tanzania, Kiongozi wa Msafara huo, Bw. Wang Jianjun ambaye ni Naibu Mkurugenzi Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, alisema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika zenye fursa kubwa ya kufikia maendeleo na kuweza kuondoka kwenye kundi la nchi maskini ndani ya kipindi kifupi kijacho.

Bw. Jianjun aliongeza “ili kuweza kufikia maendeleo ya haraka zaidi, Tanzania inapaswa kuwekeza katika viwanda ili kuongeza tija katika uzalishaji na kuongeza thamani bidhaa zake ili kuvutia masoko toka nje ya nchi.”

Akizungumza wakati wa kuwakaribisha wageni hao, Naibu Katibu Mtendaji anayeshughulikia Biashara za Kimataifa na Mahusiano ya Kiuchumi, Bw. Paul Sangawe, amesema kuwa Tanzania imedhamiria kuwa nchi ya viwanda ndani ya muda mfupi ujao.

“Tumedhamiria kuwekeza nguvu zetu kwenye uwekezaji katika viwanda; katika Mpango wa Pili wa Maendeleo, nguvu kubwa tunaiweka katika maendeleo ya viwanda ili kuweza kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025,” alisema Bw. Sangawe.

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 imedhamiria kuifikisha Tanzania kuwa nchi yenye hadhi ya kipato cha kati na kuondokana na umaskini kufikia mwaka 2025.
Naibu Katibu Mtendaji (Uchumi Jumla), Prof. Longinus Rutasitara (Wapili kushoto) akizungumza na Ugeni kutoka Tume ya Mipango na Maendeleo ya China wakati walipofanya ziara nchini. Kushoto ni Naibu Katibu Mtendaji (Biashara za Kimataifa na Mahusiano ya Kiuchumi), Bw. Paul Sangawe.
Naibu Katibu Mtendaji (Biashara za Kimataifa na Mahusiano ya Kiuchumi), Bw. Paul Sangawe akizungumza wakati wa ziara hiyo. Kushoto ni Kaimu Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Tunashukuru sana kwa kupata fursa ya ukuaji wa uchumi Tanzania. Lakini mbona kuna viwanda kama kule mkoani Mbeya vilishakufa zamani sana, kwa nini visifufuliwe kwa kutafuta wawekezaji na kuwapatia ajira vijana? kuna kiwanda cha sabuni almaarufu "Hisoap" kiwanda cha majembe "ZZK Mbeya" kiwanda cha kusindika nyama, "Tanganyika Peakaz" national milling na viwanda vinginevyo. Hivyo vingetafutiwa wawekezaji nina uhakika nchi yetu ingezidi kuboreka zaidi na zaidi.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...