![]() |
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Joyce Mapunjo |
Mkutano wa 16 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki utafanyika Tarehe 30 Novemba, 2014 Nairobi, Kenya.
Kwa mujibu wa Mkakaba Mkutano huu utatanguliwa na Mkutano wa Baraza la Mawaziri
la Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika Tarehe
20 – 27 Novemba, 2014 katika ngazi ya
Wataalam, Makatibu Wakuu na Mawaziri. Aidha, katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi,
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajiwa kukabidhiwa uwenyekiti wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki kwa kipindi cha mwaka mmoja na Jamhuri ya Kenya inayomaliza
kipindi chake, Ikiwa ni utekelezaji wa Ibara ya 12 (2) ya Mkataba wa Uanzishaji
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Akizungumzia Tanzania kuchukua Uenyekiti wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki Katibu Mkuu
wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Joyce Mapunjo alisema, “Katika
kipindi cha uenyekiti wake, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendeleza
mafanikio yaliyopatikana wakati wa kipindi cha uenyekiti wa Jamhuri ya Kenya.
Aidha, mkazo utawekwa katika kuhakikisha mtangamano wa Afrika Mashariki
unaendelezwa kwa kuzingatia matakwa ya Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya pamoja
na Kanuni na Taratibu za Jumuiya. Aidha, mkazo utawekwa katika kuhakikisha
Sekta binafsi na Wadau wengine wanashirikishwa kikamilifu katika utekelezaji wa
mtangamani wa Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na kuzitumia fursa zitokanazo na
Jumuiya ya Afrika Mashariki,”
Mkutano wa 16 wa Wakuu wa Nchi utatanguliwa na
Mkutano wa tatu wa Kazi wa Wakuu wa Nchi kuhusu uendelezaji wa miundombinu
katika Jumuiya. Mkutano hu utapokea taarifa ya utekelezaji wa maagizo
waliyoyatoa katika mkutano wa pili uliofanyika mwezi Novemba, 2012 na
kuidhinisha miradi 72 ya miundombinu ya kipaumbele ya barabara, reli, nishati
na bandari. Kwa upande wa utekelezaji miradi 16 imekamilika, 39 utekelezaji
unaendelea na 17 ipo katika hatua za awali za kutafutiwa fedha kwa ajili ya
utekelezaji wake.
Kwa upande wa Tanzania miradi nine imekamilika
ambayo ni kuupatia mji wa Kibondo umeme, mradi wa barabara ya
Mbezi-Shule-Tangibovu-Makutano ya Nelson Mandela na barabara ya Tabata.
Barabara nyingine iliyokamilika ni Nyangunge – Musoma-Airari. Shemu ya
Simiyu-Musoma inayounganisha Kenya na Tanzania ujenzi unaendelea.
Kwa mujibu wa Agenda, Wakuu wa Nchi watapokea
taarifa ya Baraza la Mawaziri la Jumuiya kuhusu utekelezaji wa mtangamano wa
Afrika Mashariki kwa kipindi cha Novemba, 2013 – Novemba, 2014.
Aidha, Wakuu wa
Nchi watajadili hatua iliyofikiwa katika majadiliano ya Sudan Kusini kujiunga
na Jumuiya ya Afrika Mashariki, maombi ya Jamhuri ya Somalia kujiunga na
Jumuiya ya Afrika Mashariki, suala la uchangiaji katika bajeti ya Jumuiya na
mapitio ya mfumo wa Kitaasisi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Wakuu wa Nchi
watajadili pia hatua iliyofikiwa katika majadiliano ya uanzishaji wa Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki
Ikiwa ni pamoja na maandalizi ya Mpangokazi wa kuelekea katika Shirikisho
pamoja na mchakato wa kuiongezea mamlaka Mahakama ya Afrika Mashariki ili iweze
kushughulikia mashauri yanayohusu biashara, uwekezaji na utekelezaji wa Umoja
wa Fedha wa Afrika Mashariki.
Kumekuwepo na mafanikio kupitia ushiriki wa Tanzani katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Tangu kuanza kwa Umoja wa Forofha wa Afrika Mashariki, mauzo ya Tanzania katika
Jumuiya ya Afrika yameongezeka kutoka Dola za Marekani Milioni 142 mwaka 2005
hada kufikia Dola za Marekani Milioni 1,120 mwaka 2013.
Bidhaa ambazo zimekuwa
zikiuzwa kwa wingi ni pamoja na nafaka, karatasi, mbole, vifaa vya umeme,
mashine, bidhaa za mafuta na vimiminika, vyandarua, bidhaa za plastiki, chai,
na bidhaa za karatasi. Bidhaa nyingine ni saruji, matunda, chuma, samaki,
ngano, sukari na nguo. Kwa upande wa uwekezaji, miradi iliyowekezwa hapa nchini
kutoka nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki imeongezeka kutoka miradi
35 yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 39.65 mwaka 2005 na kufikia Miradi
244 yenye thamani ya Dola za Marekani
milioni 676.45 mwaka 2013. Miradi
hii imezalisha jumla ya ajira 15,721 katika kipindi husika.
Katika kuimarisha biashara na fursa za masoko
ndani ya Jumuiya, Tanzania imeanza utekelezaji wa mfumo wa Himaya ya Forodha
ulioanza 1 Julai, 2014. Katika mfumo huu, uthamini wa bidhaa na ukusanyaji wa
kodi unafanyika katika Nchi mwanachama iliyoagiza bidhaa na baada ya kuthibitisha kwamba kodi imelipwa
bidhaa zinaondolewa kutoka bandari ya Dar es salaam na kusafirishwa kwenda nchi
husika mwanachama chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Forodha kwa kutumia mfumo wa
Kieletroniki wa Ufuatiliaji wa bidhaa. Aidha, bidhaa zilizolipiwa kodi katika
Nchi husika husafirishwa hazihitaji kuwekewa dhamana na hivyo kupunguza gharama
za kufanya biashara.
Kwa upande wa uendelezaji wa Miundombinu Jumuiya
imeandaa Mipango Kabambe ya uendelezaji wa barabara na reli zinazounganisha
Nchi Wanachama. Utekelezaji wa mipango hiyo unaendelea na kwa upande wa
Tanzania umehusisha ujenzi wa barabara ya Arusha- Namanga-Athi river,
Arusha-Holili-Voi-Mwatate na Malindi-Lingalinga lunga/Tanga-Bagamoyo zote
zikiunganisha Tanzania na Kenya. Kwa upande wa mtandao unaounganisha Tanzania,
Burundi, Rwanda na Uganda ujenzi wa barabara zinazoanzia
Tunduma-Iringa/Sumbawanga na kuelekea nchi hizo jirani umekamilika.
Ibara ya 124 ya Mkataba inatambua kuwa amani na
usalama ndiyo msingi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Jumuiya ya
Afrika Mashariki. Nchi Wanachama zimeidhinisha na kutekeleza Mkakati wa kikanda
wa Amani na Usalama tangu mwaka 2006. Katika kukabiliana na changamoto za
kiusalama katika Jumuiya Mkakata huu umefanyiwa mapitio na kuongeza masuala ya
Kukabiliana na Uharamia, Kupambana na uhalifu wa kimtandao, Biashara Haramu ya
Usafirishaji wa Binadamu, Mauaji ya Kimbari na Usafishaji wa fedha haramu ambazo ndizo zimekuwa zikitumika
kufadhili uhalifu.
Aidha, ili kushirikisha wadau zaidi katika kuimarisha
usalama, Jumuiya iliandaa kongamano la viongozi hao katika kuzuia kusambaza kwa
waumini wa itikadi kali za kidini na pia kuwashirikisha katika kufundisha umuhimu
wa imani yao ya dini na amani kwa waumini wao. Katika kuhakikisha wanachi
wanashirikishwa utaratibu wa Katibu Mkuu wa Jumuiya kukutana na Sekta binafsi,
Asasi za kiraia na wadau wengine kwa ajili ya mashauriano na kupata maoni yao
juu ya uendeshaji wa Jumuiya.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...