Bw. Antonio Guterres, Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi ( UNHCR) akiwasilisha Taarifa ya  Shirika hilo mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pamoja na mambo mengine,  Bw. Guterres amesema wakati idadi ya wakimbizi ikiongezeka maradufu,  UNHCR inakabiliwa na  upungufu mkubwa wa bajeti yake  kiasi cha kupunguza  kiwango cha chakula wanachopewa wakimbizi hasa Afrika.
Na Mwandishi Maalum, New York

Shirika la Umoja wa Mataifa  linalohudumia wakimbizi ( UNHCR) linakabiliwa na upungufu mkubwa wa raslimali fedha kiasi cha kuathiri utoaji wa misaada ya kibinadamu kwa wakimbizi  wanaoendelea kuongezeka kila  mwaka.
Hayo yameelewa siku ya  jumatano  na  Kamishna Mkuu wa UNHCR, Bw. Antonio Guterres wakati alipokuwa akiwasilisha taarifa  ya  Shirika hilo mbele ya  wajumbe wa Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa.
Katika taarifa  yake hiyo ambayo imeainisha  utejaji wa UNHCR katika  kipindi cha mwaka uliopita,  mafanikio na changamoto  , Bw. Guterres amesema, idadi ya wakimbizi kwa mwaka 2013 ilikuwa zaidi ya watu milioni 50 ikiwa ni idadi kubwa tangu  Vita Kuu  ya Pili ya Dunia. Na kwamba idadi hiyo  inaweza  kuongezeka ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Amesema,  idadi ya  wakimbizi wa ndani  katika Afrika imeongezeka kutoka  wakimbizi milioni 10.4  na kufikia milioni 12.5.
Aidha ameongeza kuwa    wanawake na watoto  chini ya miaka 18 ndio kundi kubwa zaidi . Kundi ambalo amesema linakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwamo za  udhalilishwaji wa kijinsia,  ndoa za utotoni,   biashara ya haramu ya binadamu ambapo wengi wao huuzwa na kugeuzwa watumwa.
Amesema  ongezeko hilo la wakimbizi haliendani na  raslimali fedha  na misaada mingine hali  inayolifanya  kutowafikia wakimbizi wengi kwa wakati  na pia   Shirika  kulazimika  kupunguza hata kipimo cha chakula ambacho wakimbizi wanapewa hususani   Barani Afrika.
Amebainisha kuwa  Afrika inahitaji msaada wa haraka wa dola  186 milioni ili wakimbizi waweze kupata mlo kamili kwa mwaka huu wa 2014.  Aidha Kupunguzwa kwa kipimo  cha chakula kumesababisha watoto wengi  kupata utapia mlo.
Amezitaja baadhi ya sababu zinazopelekea uzalishaji mkubwa wa wakimbizi kuwa ni vita vya wenyewe kwa wenye, ukame ,  uhaba wa maji na mabadiliko ya tabia  nchi.
Aidha  ameeleza kuwa kwa upande wa Bara la Afrika ambalo limeshuhudia  ongezeko la wakimbizi kumetokana na   vita vya wenyewe kwa wenye katika nchi za Mali,  Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudani ya Kusini, Somalia na  baadhi ya maeneo ya Jamhuri ya  Kidemokrasia ya Kongo.
Eneo jingine ambalo Kamishna amelitaja kuzalisha wakimbizi wengi ni pamoja na Mashariki ya Kati hususani Syria.
Kamishna Mkuu  pamoja na  kuhimiza Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kulichangia  Shirikia hilo ili liweze kuendelea na jukumu la  utoaji wa misaada ya kibinadamu.  Amesisitiza  kuwa   suluhisho pekee la  kumaliza tatizo la kuwapo kwa wakimbizi  ni  la kisiasa zaidi kwa pande zinazohusika  kumaliza tofauti zao.
Amesema, wanasiasa hawawezi kuendelea kuwa chanzo cha migogoro na machafuko yanayopelekea wananchi wao  kuyakimbia makazi yao    na nchi  zao na kisha kuyaachia Mashirika    yanayotoa misaada ya kibinadamu   jukumu la  kuwahudumia wahanga wa machafuko hayo.
“ Tufikie mahali sasa tubadilike  na tulikatae hili, haiwezekani wengine waazishe  machafuko na  kuwaachia watu wengine wasafishe uchafu wao” amesema Bw.
Aidha  ametumia  mkutano huo kuzishukuru nchi mbalimbali ambazo  kwa muda mrefu zimekuwa wenyeji wa wakimbizi ikiwa ni pamoja na kutumia raslimali zao  kuwasaidia.
Akasema nchi hizo  ikiwamo Tanzania  zimeratibu  na kuwezesha  baadhi ya wakimbizi kurejea makwao kwa hiari ikiwani  ni  pamoja  na kuwapatia uraia kwa wale ambao wameomba.
Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania, Balozi Ramadhan Mwinyi, akizungumza kwa  niaba ya SADC  amesema  Jumuiya hiyo  inapinga kuendelea kuitegemea UNHCR hata katika  mambo ambayo nchi mwenyeji inaweza kuyatekeleza.
Akatoa mfano wa baadhi ya majukumu ambayo nchi mwenyeji inaweza kuyatekeleza pasipo kutegemea UNHCR  kuwa ni pamoja na ukusanyaji wa  takwimu na utambuzi wa  wakimbizi.
Amesema  jukumu ambalo UNHCR inaweza kuchangia ni katika uwezeshaji na si utekelezaji   wa zoezi lenyewe kutokana uenyeti wake.
Kuhusu  kupungua kwa bajeti ya Shirika hilo, SADC imeelezea wasi wasi wake kuwa  pamoja na athari ambazo zimeanza kujitokeza pia kutaathiri uwezo wa nchi wenyeji kuendelea kutoka huduma kwa wakimbizi  na hasa  ikizingatiwa kuwa pamoja na matatizo ya kiuchumi  waliyonayo bado  nchi hizo zimekuwa zikitumia  raslimali zake 
 Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania, Balozi Ramadhan Mwinyi akizugumza kwa niaba ya nchi za SADC katika mkutano huo ambapo wajumbe wa Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa  wamepokea na kujadili  taarifa ya  UNHCR katika mkutano uliofanyika siku ya Jumatano.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...