Na Johary Kachwamba-MAELEZO.
TAKWIMU
zinaonesha kwamba watoto 130000 wana maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU) kati
ya hao 39317 wamefikiwa na kupatiwa huduma ya dawa za kupunguza makali ya virusi
hivyo.
Hayo yamesemwa leo na
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dkt. Pindi Chana wakati
akifungua kongamano la nne la kitaifa la VVU na UKIMWI kwa watoto linalofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa
Mwalimu Nyerere uliopo jijini Dar-es-salaam.
Dkt . Chana alisema asilimia
39 ya watoto walio katika hatari ya kupata maambukii ya UKIMWI hupimwa vipimo vya kubaini maambukizi
ya VVU ndani ya miezi miwili baada ya kuzaliwa hivyo basi kuna umuhimu kwa watoto hawa kupata huduma za tiba
mapema.
Akizungumzia maambukizo ya
VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto waziri huyo alisema Tanzania imepiga hatua
katika kuzuia maambukizo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto lengo likiwa ni kutokomeza kabisa maambukizi mapya kwa
watoto wachanga. “Mama wajawazito na wale
wanaonyoyesha wanapatiwa huduma ya dawa za kupunguza makali ya VVU mara tu
wanapogundulika kuwa na maambukizo, kupitia mpango mpya unaojulikana kama
‘uwezekano namba 2 au (Option B+)”, alisema Dkt.Chana.
Alisema kufikia mwezi Juni mwaka huu jumla ya akina mama 940900 kati ya 1050043 hii
ni sawa na asilimia 89.6% ya waliohudhuria kliniki walipimwa UKIMWI kati ya hao
47856 takribani asilimia 5 walikutwa na maambukizi ya VVU.
Kwa upande wa watoto 20569
walipima kipimo cha DBS kati ya hao
2063 hii ni sawa na asilimia 10
walikutwa na maambukizo ya VVU. Naye Katibu Mkuu wa Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Donan Mbando, alisema ingawa nchi imepiga
hatua katika mapambano ya kudhibiti UKIMWI hali halisi
inaonyesha kuwa bado kuna maambukizo
yanatokea sio tu kwa watu wazima bali na kwa watoto pia.
“Ni jukumu letu kuendelea kuweka
mikakati ya dhati na kuisimamia ili kuhakikisha lengo la kutokomeza maambukizo
ya VVU tunalifikia kwani mwaka 1986 maambukizi yalikuwa juu kwa asailimia 18
lakini hivi sasa yameshuka na kufikia asilimia 5.3”, alisema Dkt. Mbando.Kwa upande wake Mkurugenzi wa ufundi kutoka Taasisi ya
Elizabeth Glaser Pediatric Aids (EGPAF) ambao ni waandaaji wa kongamano hilo Chrispin Kimario alisema ni muhimu kwa wazazi na
jamii kushirikiana kwa pamoja na kulibeba jukumu la kuhakikisha kila mama mjamzito anapata huduma
ya vipimo husika na matibabu kwa wakati.
Kimario alisema, “Watoto
wameachwa nyuma, ni vyema tukumbuke kuwa mtoto hawawezi kujipeleka wenyewe hospitali
kupima afya zao, hivyo ni jukumu letu wazazi, walezi na jamii kwa ujumla
kuhakikisha watoto hawa wanapata huduma wanazostahili”.
Kauli mbiu ya kongamano
hilo la siku mbili ambalo limehudhuriwa na wadau wa afya kutoka asasi za umma
na binafsi za ndani na nje ya nchi ni ongeza kasi: Rahisisha upatikanaji wa
utumiaji wa huduma za VVU na Ukimwi, pata matokeo chanya ya afya za mama na
watoto wanaoishi na VVU.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...