MWENYEKITI wa kamati ya usajili ya Simba, Zakaria Hans Pope amewataka Simba ukawa kufuta kesi iliyopo mahakamani ili wawarejeshee uwanachama wao. 
Pope alisema leo  kuwa hawana ugomvi na Ukawa, na kwamba uongozi uliopo madarakani upo tayari kuwarudisha Ukawa na kuwa kitu kimoja kwa maslahi ya kuijenga Simba. 
"Ukawa ni matawi mawili ya Mpira Pesa na Mpira maendeleo, nimeshakutana na mpira pesa nikazungumza nao, nimewashauri wawasiliane na wenzao wakafute kesi ili tuungane na tuwe kitu kimoja kama zamani, kwa maslahi ya maendeleo ya Simba. 
“Wanachama hawa walifutwa kwa kufuata taratibu za kikatiba,tutawarudisha kwa kufuata sheria."alisema Pope Wanachama hao walikuwa wakihusishwa kuhujumu matokeo ya sare sita mfululizo za Simba kwenye mechi sita za kwanza za ligi kuu ya Bara, lakini Pope alisema "Matokeo mabaya ya Simba hayakuhusiana na Ukawa.
"Simba ilifanya vibaya kwa sababu za kiufundi. Tumeona mapungufu yaliyojitokeza kwenye mechi za mwanzo. Tumeyafanyia kazi kwa kusajili wachezaji wapya ambao tunaamini watatusaidia na kuziba mapungufu yaliyojitokeza. 
“Wanachama na wapenzi wa Simba waachane na dhana potovu kuwa kundi hili ni wasaliti, ndio waliosababisha kufanya vibaya.” Kundi la 'Ukawa' liliundwa na wanachama 71 waliofutiwa uwanachama baada ya kufungua kesi mahakamani wakipinga mchakato wa uchaguzi kwa kile walichodai umekiuka katiba kwa kumuondoa kwenye kinyang'anyiro aliyekuwa mgombea wa nafasi ya urais Michael Wambura. 
Baada ya mwenyekiti wa sasa Evans Aveva kuingia madarakani, akawafutia uwanachama Michael Richard Wambura pamoja na wanachama 71 katika mkutano mkuu wa wanachama uliofanyika mapema mwezi Novemba ulioudhuriwa na wanachama 860 wa Simba  kwenye Ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kukiuka katiba kwa kupeleka masuala ya soka mahakamani. 
Kabla ya kufikia uamuzi wa kufanya mkutano, Simba kupitia kwa Rais wake, Evans Aveva ilitoa nafasi kwa wao kumuona na kuwasilisha utetezi wao. Hata hivyo, hakuna hata mwanachama mmoja aliyejitokeza kwa ajili ya kulizungumzia suala hilo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...