Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Ofisi ya Hali ya Hewa ya
Uingereza (UK Met Office) wamesaini mkataba wa makubaliano ya uboreshaji
huduma za hali ya hewa hapa nchini. Mkataba huo umesainiwa tarehe
11 Novemba, 2014 wakati wa kikao cha masuala ya hali ya hewa (IBCS)
kilichofanyika mjini Geneva Uswiss.
Akizungumzia makubaliano hayo Dkt Agnes Kijazi alisema Mamlaka ya Hali
ya Hewa ililiomba Shirika la Hali ya Hewa Duniani kuisaidia TMA kuboresha
huduma zake ili ziwe za kisasa (Modernization of meteorological services in
Tanzania) na ofisi ya hali ya hewa ya Uingereza ilikubali kuisaidia TMA katika
zoezi hilo. ‘Makubaliano tunayosaini leo ni sehemu tu ya kazi kubwa ya uboreshaji
wa huduma za hali ya hewa nchini ambapo shirika la Kimataifa la Uingereza
(DFID) kupitia Ofisi ya Hali ya Hewa ya Uingereza limeipatia TMA Pound
70,000’ alisema Dkt. Kijazi .
Akifafanua kuhusu matumizi ya fedha hizo Dkt.
Kijazi alisema fedha hizo zitatumika kuijengea uwezo TMA kutunza data za hali
ya hewa za kihistoria kwa njia ya digitali na pia kuwajengea uwezo watumishi wa
TMA kutoa huduma bora zinazokidhi matarajio ya wadau na hivyo kulinda maisha
ya watu na mali zao.
Kwa upande wake mkuu wa Ofisi ya Hali ya Hewa ya Uingereza Dkt. Rob Varley
alisema anafurahia ushirikiano uliopo kati ya TMA na UK met office na akaahidi
kuendeleza ushirikiano huo na pia kuisadia TMA kuboresha huduma zake.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa, Dkt. Agnes Kijazi akisaini mkataba na mtendaji mkuu wa Ofisi ya Hali ya Hewa ya Uingereza Dkt. Rob Varley. Tukio hilo lilishuhudiwa na Dkt. Ladislaus Chang’a, Mkurugenzi wa Utafiti katika Mamlaka ya Hali ya Hewa na Bi. Jane Wardle mtaalam wa masuala ya hali ya hewa kutoka ofisi ya hali ya hewa ya Uingereza.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...