KLABU  ya Simba imeingia kambini leo Zanzibar huku ikimtema mshambuliaji wake raia wa Gambia Omar Mboob.

Katibu mkuu wa Simba Steven Ally alidhibitisha kuwa mchezaji huyo ameenguliwa kwenye kikosi cha Simba kwa vile ameshindwa kuonyesha kiwango cha kumshawishi kocha Patrick Phiri ili aweze kusajiliwa.

"Mboob kwa sasa tunamfanyia taratibu ili aweze kurudi nchini kwao, kesho (leo) au kesho kutwa ataondoka, ameshindwa kuonyesha makali."alisema

Wakati Ally akisema hayo, Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba Zakaria Hanspope alisema "Mimi nilikutana na meneja wake katika shughuli zangu za kibiashara akaniambia kijana wake ni mzuri na muda wowote atakwenda kufanya majaribio barani Ulaya. Nikaona si mbaya akaja hapa tukamwangalia, lakini kiwango chake bado” alisema  Hanspope.

Hata hivyo, tayari Simba imefikisha idadi ya wachezaji watano wa kigeni kwa mujibu wa kanuni za Ligi ambao ni Dan Sserunkuma aliyechukua nafasi ya Raphael Kiongera, Mganda Emmanuel Okwi, Joseph Owino na warundi Pierre Kwizera na Amissi Tambwe.

Katika hatua nyingine, Simba imeingia kambini Zanzibar jana jioni kujiandaa na mechi yao dhidi ya Yanga huku makocha wa timu hizo kila mmoja ana matumaini ya kushinda mchezo huo huku kocha wa Yanga Marcio Maximo akiingia mchecheto na kutamka kuwa "Kocha anaajiriwa ili afukuzwe, hayo ndio maisha hasa Afrika, sihofii kufukuzwa iwapo tutafungwa na Simba, ninachoangalia si tu mechi ya mtani Jembe bali na za ligi.

Kauli ya Maximo aliiotoa baada ya kuulizwa, kocha Ernie Brandts alitimuliwa baada ya matokeo ya mechi ya mtani jembe msimu uliopita, na yeye amejiandaje katika hilo.

"Kocha anaajiriwa ili afukuzwe, mimi sijali, matokeo yoyote nitayapokea na uongozi utaangalia kama wanifukuzea au la wao ndio wameniajiwa, kikubwa ninachoangalia ni uwezo wa wachezaji wangu na zaidi naangalia mbele."alisema na kuongeza

"Muhimu ni kushinda, haijalishi ni mechi ya kirafiki au ni Ligi, zinapokutana timu kubwa za watani wa jadi hakuna mechi raisi, nimejipanga vizuri, lengo ni kushinda, nisingependa nipoteze."alisisitiza Maximo.

Wakati Maximo akisema hayo,  Kocha wa Simba Patrick Phiri alisema timu yake imeingia Kambini Zanzibar  kujiandaa na mechi ya watani zao   Yanga ambao wameshindwa kuwafunga katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa Oktoba 18, kwa kutoka suluhu.

Phiri alisema wameanza kujipanga kwa mazoezi makali ya viungo katika klabu ya mazoezi (gym) ya Chang’ombe, Dar es Salaam kwa ajili ya kuwajengea nguvu ya mwili wachezaji wake na sasa wanfanya mazoezi ya uwanjani.

“Mechi inayokuja dhidi yetu na Yanga hakuna droo tena, Simba ni timu kubwa tunahitaji kushinda,” alisema Phiri.

Hata hivyo matumaini makubwa ya Phiri yapo kwa Dan Sserunkuma kwa kile alichoeleza mchezaji huyo ni mzuri na amemfuatilia kwa muda mrefu akiwepo timu ya taifa ya Uganda 'Uganda Crenes' na Gor Mahia.

“Daniel ni mchezaji mzuri, nimemfuatilia akiwa katika timu yake ya Taifa na hata akiwa Gor Mahia kule Kenya, huyu ni mshambuliaji aliyekamilika… naamini atatusaidia sana,” alisema. 

" Nataka mashabiki wasihofu juu ya matokeo ya sasa ya Simba na michezo ya kirafiki badala yake nitawafurahisha mwaka ujao utakapoanza. 

"Kwa sasa nina michezo miwili migumu iliyobaki mwaka huu, tutacheza na Yanga wikiendi hii kisha tutavaana na Azam  kwenye Ligi Desemba 26 mwaka huu. Mwakani nitakuwa nimebakiza michezo 18 ili ligi imalizike  hivyo ninataka kuhakikisha ninafanya vizuri na kuchukua ubingwa tena kwa kupata matokeo mazuri.

Hivi karibuni Simba imecheza michezo miwili ya kirafiki. Mmoja dhidi ya Express ya Uganda ambao uliisha kwa sare ya 0-0. Kisha wakacheza na Mtibwa na kupokea kipigo cha 4-2.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...