NA ANDREW CHALE, BAGAMOYO
NAIBU Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, ametoa rai kwa Taasisi za Kiserikali na zisizo za Kiserikali kuona umuhimu wa kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi katika shughuli za upimaji ardhi ili kuwaepusha na adha zinazoweza kuwapata pale yanapotokea maafa.
Hayo alisema mjini hapa siku Desemba 8, wakati wa ufunguzi wa mradi na ugawaji wa hati kwa wanunuzi wa Viwanja katika Kijiji cha Mapinga- Bagamoyo ulioratibiwa na Taasisi ya Maendeleo ya Miundombinu chini ya Dhamana ya Uwekezaji Tanzania (UTT -PID).
“Wananchi wapewe elimu ya kutosha katika shughuli za upimaji ardhi na umuhimu wa kuishi kwenye maeneo yaliyopimwa. Hii itasaidia serikali kutoingia gharama hususani pale yanapotokea maafa kama vile mafuriko nikitolea mfano wa eneo kama Jangwani Jijini Dar es Salaam ambapo serikali imekuwa ikiingia gharama mara kwa mara katika uokoaji wa watu katika eneo hilo kipindi mafuriko yanapotokea,” alisema Nchemba.
Naibu Waziri huyo wa Fedha ambaye aliwakilishwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Janeth Mbene alieleza pia kuwa migogoro ya ardhi nchini ni moja ya matatizo makubwa yanayotokana na watu wengi kununua viwanja au ardhi ambazo hazijapimwa.
Aliipongeza Taasisi inayoratibu miradi hiyo ya maendeleo ya UTT PID kwa jitihada kubwa inayofanya na kueleza kwamba kupitia mifumo ya kisasa ya upimaji wa maeneo unaofanywa na taasisi hiyo ya serikali ndio utakaokuwa msingi utakaoziwezesha Halmashauri, Miji na Majiji ya nchini kuwa na maendeleo ya kasi kutokana na mipango hiyo ya kisasa.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, miongoni mwa mambo yanayochangia umaskini kwa wananchi ni pamoja na kutopimwa kwa ardhi wanayomiliki na kueleza kuwa inakadiriwa kuwa asilimia 10 tu ya ardhi yote ya nchini ndiyo iliyopimwa huku nchi ikikadiriwa kuwa na zaidi ya kilometa za mraba milioni moja.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa UTT PID, Elpina Mlaki alisema katika mradi huo wa Mapinga ambao ni wa awamu ya pili utahusisha uuzaji wa viwanja 246 vilivyo na huduma zote muhimu kama vile maji ya Dawasco mpaka eneo la mradi na ujenzi wa tanki la kutunzia maji ya dharura lenye ujazo wa lita 150,000 , umeme pamoja na huduma nyinginezo.
Alisema kutokana na uhitaji mkubwa wa viwanja katika eneo hilo taasisi hiyo iliyo chini ya serikali inatarajia kuwekeza zaidi katika miundombinu na kuongeza wigo wa viwanja zaidi ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka siku hadi siku kutoka kwa watu mbalimbali katika eneo la Mapinga.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Janeth Mbene akiwahutubia wananchi (Hawapo pichani) wakati wa hafla hiyo.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...