*Ni kwa njia ya kielektroniki kupitia huduma ya M-Pesa
*Imelenga wanaohitaji huduma katika sekta ya usafiri wa anga na hoteli
Katika kuzidi kurahisisha huduma za malipo wakati tukielekea msimu wa sikukuu za Krismas na Mwaka Mpya,kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania leo imezindua huduma mpya ya kufanya malipo kwa njia ya kielektroniki.
Huduma hii mpya inayozinduliwa leo inajulikana kama Vinjari na M-Pesa ambayo itawawezesha wateja wa Vodacom kufanya malipo ya huduma katika sekta ya usafiri wa ndege na utalii kwa njia ya kieletroniki kama ambavyo yamekuwa yakifanyika kwa kutumia kadi mbalimbali za kufanyia malipo kimataifa.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa huduma hii Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Umma wa Vodacom Tanzania, Rosalynn Mworia amesema huduma hii kwa kuanzia itafanyika kwa kushirikiana na mtandao wa malipo ya kieletronikali nchini ujulikanao kama Vinjari.co.tz ambao unafanya kazi na zaidi ya taasisi 300 za kutoa huduma yakiwemo mahoteli ya utalii na makampuni mbalimbali yanayotoa huduma hususani za masuala ya utalii na sehemu za mapumziko na burudani.
“Kadri siku zinavyozidi kusonga mbele tunazidi kushuhudia mapinduzi makubwa ya kiteknolojia hususani katika masuala ya biashara, Vodacom tumeona umuhimu wa kuanzisha huduma hii ili kuwawezesha wateja wetu kufanya miamala yao kwa njia ya kieletroniki kupitia huduma ya M-Pesa ili kwenda na wakati zaidi. Kwa kuanzia tutatoa huduma hii kupitia mtandao mpana wa malipo ya kielektronoki wa vinjari.co.tz na kadri siku zitakavyosonga mbele tutazidi kuboresha huduma hii,” alisema.
Aliongeza kuwa Vodacom inaelewa kuwa idadi kubwa ya Watanzania hawana kadi za kimataifa za kufanya miamala ya malipo kwa njia ya kielekroniki ndio maana imekuja na huduma hii ikiwa inawalenga wateja wetu wanaotumia huduma ya M-Pesa.
Naye Mkurugenzi wa Vinjari.com,Andrew Mboma amesema ili kupata huduma hii mteja anaingia katika sehemu ya kawaida ya kufanya miamala ya M-Pesa kwenye simu yake atakuta sehemu inayomuelekeza jinsi ya kupata huduma kupitia Vinjari na M-Pesa ambapo ataweza kufanya muamala kwa kadri ya huduma atakayokuwa anahitaji na atakatwa fedha kutoka akaunti yake ya M-Pesa kulipia huduma hiyo na malipo kidogo ya kutumia huduma hiyo. Maelezo zaidi yanapatikana kwa kutembelea tovuti ya vinjari.co.tz
Katika miaka ya karibuni kumekuwepo na ongezeko kubwa la matumizi ya simu za mkononi nchini ambapo pia kumekuwemo na ongezeko la watumiaji wa mtandao wa internet. Inakadiriwa kuwa zaidi ya watanzania milioni 28 wanatumia huduma za simu za mkononi ambapo zaidi ya watanzania milioni 6 wanatumia huduma za internet.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...