Mwenyekiti wa Kamati ya uchaguzi ya Simba na mjumbe wa Bodi ya Ligi Kuu, Wakili Damas Ndumbaro (pichani) amesema hatma yake ya kujihusisha na masuala ya soka itajulikana kwenye mkutano mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Mkutano huo umepangwa kufanyika mapema mwezi Machi mwakani ambapo ajenda ya mkutano huo ni Kufungua kikao, kuthibitishwa kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu, kusoma nakuthibitisha ajenda, hotuba ya Rais, kupokea taarifa za utekelezaji za wanachama, kupitisha taarifa za utekelezaji wa Kamati ya Utendaji, kupitisha taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu za mwaka uliopita, kupitisha
taarifa ya wakaguzi na hatua zilizochukuliwa, kupitisha bajeti ya mwaka 2015.
Mkutnao huo utakuwa ni wa kwanza kufanyika tangu rais Jamal Malinzi aingie madarakani ambapo awali ulitakiwa ufanyike mapema mwaka huu lakini haukufanyika huku habari ambazo Mwananchi ilizipata zinasema kuwa ukata unaokabili Shirikisho hilo ndio ulisababisha kutofanyika kwa mkutano mkuu, huku kukiwa na hofu ya uongozi uliopo kuondolewa madarakani kutokana na baadhi ya wajumbe kujipanga kupiga kura za kutokuwa na imani za Rais wa TFF kutokana na makundi yaliyopo ndani ya shirikisho hilo.
Dk. Ndumbaro alisema kuwa atatumia fursa hiyo ya mkutano mkuu kujua hatma yake baada ya TFF kuikalia rufaa yake zaidi ya miezi miwili baada ya kufungiwa kwa miaka saba kujihusisha na masuala ya soka ndani na nje ya nchi baada ya kuzitetea klabu zisikatwe asilimia tano ya mapato ya wadhamini na TFF.
"Mimi nimenyamaza tu, wala sitaki kuongea nao chochote, wasubiri mkutano mkuu mwezi wa tatu, mbivu na mbichi zitajulikana."alisema Ndumbaro
Miezi michache iliyopita TFF ilikuwa inashinikiza klabu kukatwa asilimia tano za mapato yatokanayo na fedha za wadhamini, kwa kuwa klabu zimekuwa zikipokea udhamini wa Sh73 milioni kutoka Vodacom na Sh110 milioni kutoka Azam TV ambazo asilimia tano yake ni Sh9.15 milioni na kwa klabu 14 za ligi hiyo, TFF ingepata Sh128 milioni iwapo klabu zingeridhia.
Hata hivyo, Ndumbaro alikata rufaa kwenye kamati ya rufaa ya nidhamu chini ya Profesa Mgongo Fimbo, na wajumbe wake Hamidu Mbwezeleni ambaye ni Makamu . Wengine ni Titus Bandawe, Twaha Mtengera na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) mstaafu Boniface Mpaze.
TFF imekuwa ikikaririwa mara kwa mara ikisema kuwa tayari ilishawasilisha suala la Ndumbaro kwenye kamati hiyo ya rufaa ya nidhamu lakini kamati hiyo ndio imekuwa ikichelewesha kwa kuikalia rufaa hiyo kwa vile haijapanga muda wa kukutana. Hata hivyo Makamu mwenyektii wa Kamati hiyo ya Rufaa Hammidu Mbwezeleni aliwahi kuimbia Mwananchi kuwa suala hilo bado halijafikishwa kwenye kamati yao.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...