Wananchi wa Mkoa wa Njombe wametakiwa kupanda miti kibiashara ili hatimaye kuongeza kipato katika familia zao. Wameagizwa pia kuitunza miti wanayoipanda na kusubiri ifikie umri wa kuvunwa ndipo ikatwe.
Maagizo hayo yametolewa na Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dr. Rehema Nchimbi (pichani) jana tarehe 10 Januari 2015 alipozungumza kama Mgeni Rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Taifa ya Kupanda Miti katika ngazi ya Mkoa.
Katika maadhimisho hayo ambayo mwaka huu yalifanyika wilayani Makete jumla ya miti 3,000 ilipandwa katika kitongoji cha Dombwela kilichoko katika mji wa Makete.
Dr. Rehema Nchimbi aliitumia fursa hiyo kuagiza Halimashauri zote za Mkoa wa Njombe kutenga maeneo maalum ya kupanda miti kwa ajili ya watu wasiojiweza. Miti hiyo itachangia baadaye katika upatikanaji wa fedha za kuwasomesha watoto wa familia hizo.
Vilevile Mkuu wa Mkoa alizitaka Halimashauri zote za Mkoa wa Njombe kustawisha miche ya kutosha na kuwapatia wananchi waipande kwa wingi kwa nia ya kuifanya miti kuwa zao maalum la uwekezaji katika mkoa huo. Aidaha aliwataka wananchi wa Njombe wanaoishi nje ya mkoa kuwekeza pia katika mkoa wao husuan katika upandaji miti ili kukuza uchumi mkoani mwao.
Kwa namna ya pekee Dr. Nchimbi aliwapongeza wananchi wa mkoa mzima wa Njombe kwa kuwa na utamaduni wa kupandamiti. Hata hivyo akawataka kuipalilia inapokuwa midogo, kuitunza kitaalam na kuilinda dhidi ya moto kichaa .
Aina ya miti iliyopandwa katika maadhimisho hayo ni Mizambarao na Miturunga ambayo inafaa kuhifadhi vyanzo vya maji. Mkuu wa Mkoa alichagua kupanda miti ya Miturunga kwa kuwa ni miti imara inayotoa mbao zisizochakaa upesi.
Alipokuwa akipanda mti hiyo Mkuu wa Mkoa alichukua fursa hiyo kuwataka wananchi wa mkoa wa Njombe, pamoja na kupanda miti ya biashara, kuviimarisha vyanzo vyote vya maji katika mkoa wa Njombe kwa kupanda miti inayofaa kuhifadhi maji.
Maadhimisho yaliyofanyika mkoani Njombe ni sehemu ya sherehe za SIKU Ya TAIFA YA KUPANDA MITI ambazo huadhishwa kitaifa tarehe 1 Aprili kila mwaka. Kaulimbiu ya mwaka huu nii:‘Panda Miti Kibiashara’.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...