Fainali ya kumsaka Bingwa wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL), inatarajiwa kufanyika kesho kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi kuanzia majira ya saa 10 kamili jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

Awali mchezo huo wa fainali ulikuwa umepangwa kufanyika kesho kwenye dimba la Uwanja wa Taifa, lakini kutokana na sababu zilizopo nje ya uwezo wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TTF imepelekea mchezo huo kuhamishiwa Chamazi.


Mchezo huo wa fainali utaanza saa 10 kamili jioni, na utaonyeshwa moja kwa moja na kituo cha Azam TV ili kuwapa nafasi wapenzi na wadau wa soka waliopo mbali na hasa mikoani kuweza kushuhudia mchezo huo.

Bingwa wa Fainali ya Ligi Daraja la Kwanza atazawadiwa Kombe pamoja na medali, huku mshindi wa pili akipata kikombe na medali pia. Viingilio vya mchezo huo ni tsh.5,000 kwa jukwaa kuu na tsh. 3,000 kwa majukwaa ya mzunguko.

Wakati huo huo, Ligi Kuu ya Vodacom inaendelea leo (Jumamosi)  katika viwanja vitatu tofauti, Mgambo Shooting watakua wenyeji wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Ndanda FC ya Mtwara watawakaribisha Wagosi wa Kaya timu ya Coastal Union kutoka jijini Tanga katika mchezo utakaochezwa kwenye dimba la Ngwanda Sijaona.

Huku wakata miwa wa Kagera Sugar wanaoutimia Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga wakiwakaribisha Maafande wa Jeshi la Polisi kutoka mjini Morogoro timu ya Polisi.

Ligi hiyo ya Vodacom itaendelea tena kesho Jumapili katika viwanja vitatu   tofauti, Uwanja wa Chamazi wenyeji Azam FC wataikaribisha timu ya maafande wa Jeshi la Magereza nchini Tanzania Prisons, mchezo utakaonza majira ya saa 2 kamili usiku.

Mjini Shinyanga wenyeji timu ya Stand United wataikaribisha Simba SC kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, huku wagonga nyundo wa jiji la Mbeya, timu ya Mbeya City wakicheza na timu ya Young Africans kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
  

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA 
MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...