Na Bashir Yakub
Kawaida unapokuwa umeingia katika mkataba au makubaliano katika jambo lolote lile kunakuwa na masharti ambayo unapaswa kuyatimiza au kutimiziwa. Na hapa nazungumzia mikataba yote uwe wa kuuza mbuzi au ule wa kujenga ghorofa mia, yote ni mikataba. Masharti hayo huwa ndio makubaliano yenyewe au twaweza kusema kuwa ndio mkataba wenyewe. Kila upande unawajibika juu ya utekelezaji wa masharti hayo. Yeyote anayefikia hatua ya kukiuka masharti hayo au hata kukiuka sharti moja tu, hana namna ila kukubaliana na hatua na utaratibu wa kisheria kuhusu uvunjwaji au ukiukwaji wa mikataba.
1.KUKIUKA MKATABA AU MAKUBALIANO.
Uvunjaji wa mkataba unaweza kutokea katika njia nyingi. Moja ni ile ya kawaida ambapo mtu huamua kujitoa kwa kusema,kutamka au kuandika kuwa sasa sitafanya hili na lile hata kama lipo katika makubaliano yetu. Pili njia nyingine ya kuvunja mkataba ni pale ambapo mtu hasemi kwa kutamka kwamba sasa sitafanya hili wala lile isipokuwa hatimiza wala hatekelezi kile mlichokubaliana. Ifahamike kuwa mtu anapoingia mkataba na mtu mwingine au kampuni na kampuni au kampuni na mtu sheria inalazimisha kutekeleza kwa usahihi yale yote yaliyokubaliwa katika mkataba huo. Utekelezaji wa baadhi ya masharti na kuacha mengine au kutotekeleza yote kabisa ni uvunjaji au ni kujitoa katilka mkataba kwa mujibu wa sheria. Aidha nasisitiza kuwa ili mtu ajitoe katika mkataba sio lazima aseme kuwa nimejitoa katika mkataba. Kitendo cha kutofuata makubaliano kama yalivyokubaliwa ni kujitoa katika mkataba moja kwa moja.
2.KUMDAI FIDIA ALIYEKIUKA MKATABA AU MAKUBALIANO.
Si vyema mtu akafanya makubaliano na mtu mwingine halafu akapotea bila kutekeleza kile kilichokubaliwa. Ni sababu hii inayonifanya kuwaambia watu kuwadai fidia wale wanaokiuka masharti. Kudai kulipwa fidia baada ya kuvunjwa mkataba ni takwa la kisheria na hivyo si ukorofi kama ambavyo mtu anaweza kufikiri.
3.AINA ZA FIDIA UNAZOWEZA KUDAI UKIVUNJIWA MKATABA.
( a ) Fidia zipo za aina nyingi. Kwanza kuna fidia ambayo utatakiwa kulipa kutokana na makubaliano yenu ya awali wakati mnaingia mkataba. Hii ni aina ya fidia ambayo wahusilka katika mkataba hukubaliana awali kabisa wakati wanaingia katika mkataba ambapo hupanga kiasi cha fidia ambacho watalipana iwapo mmoja kati yao atakiuka au kujitoa katika mkataba. Kwa kuwa fidia hii huwa imeandikwa na ipo ndani ya mkataba basi aliyekiuka au kujitoa katika mkataba hutakiwa kulipa fidia hiyo kulingana na makubaliano yao mara moja.
( b ) Fidia nyingine ni ile ambayo mtu hutakiwa kulipa iwapo wakati wanaingia mkataba hakuna fidia yoyote waliyokuwa wamekubaliana kulipa iwapo mmoja wao atakwenda kinyume. Hii ni aina ya fidia inayotathminiwa na mahakama. Mahakama hutathmini fidia hii kwa kuangalia mambo mawili yaani kiwango cha ukiukwaji wa mkataba na hasara zilizotokana na ukiukwaji huo. Kupitia hayo mahakama huweza kutangaza kiwango cha fidia anachotakiwa kulipwa mtu ambaye amevunjiwa mkataba.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...