Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi.

10/2/2015 Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete amewataka wakazi wa wilaya hiyo kutokubali kuuza maeneo ya ufukwe wa Bahari  ya Hindi kwa kiasi kidogo cha fedha  kwani thamani ya maeneo hayo ni kubwa.

Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alitoa rai hiyo jana wakati akiongea  kwa nyakati tofauti  na viongozi wa Halmashauri kuu ya tawi ya Chama hicho  katika matawi ya Raha leo na Ufukoni yaliyopo katika kata ya Rahaleo wilayani humo.

Alisema hivi sasa kuna wageni wengi ambao wanaenda kwa wananchi na kununua maeneo ya ufukweni kwa bei ya chini lakini kama wamiliki wa maeneo hayo watakuwa na subira watayauza  kwa bei kubwa kwa kipindi cha  miaka michache ijayo. 

“Baada ya miaka michache ijayo mkoa wetu  utakuwa tofauti kimaendeleo,  Serikali inampango wa kujenga mji wa kisasa katika eneo la  Mitwero.

“Nawasihi hata kama mtu anashida kiasi gani atafute njia nyingine ya kupata fedha lakini siyo kuuza eneo la ufukweni kwa bei ndogo,  kama kuna aliyebakiza eneo lake asiuze  kwani kimfaacho mtu ni chake”, alisisitiza Mama Kikwete .

Kuhusu elimu MNEC huyo aliwasihi viongozi hao kusimamia elimu ya watoto wao na kuwahimiza waende shule  kwani wakiwa na elimu wataweza kufanya kazi za kitaalamu katika sekta mbalimbali ikiwemo ya gesi inayopatikana mkoani humo.

Kwa upande wa wanawake aliwahimiza kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi  mkuu ujao na hivyo  kufika katika ngazi ya maamuzi  pia kwa kufanya hivyo hawatapoteza haki yao ya msingi ya kuchaguliwa.

Akiwasalimia viongozi hao Mkuu wa wilaya ya Lindi Dkt. Nassoro Hamidi alisema shule za Sekondari zimefunguliwa lakini  wanafunzi walioripoti shuleni ni wachache  na kuwaomba kupita nyumba hadi nyumba kuwahamasisha wazazi wawapeleke watoto wao shule kwani bila ya elimu hakuna maendeleo.

“Serikali ilitoa agizo  kama watoto hawana ada au nguo za shule waende hivyo hivyo kuanza masomo mambo mengine yatafuata baadaye lakini hadi sasa bado idadi ya wanafunzi walioripoti shuleni ni ndogo”, alisema Dkt. Hamidi.

Kuhusu wananchi kujitolea katika ujenzi wa maabara aliwasihi viongozi kuwahimiza kushiriki  katika ujenzi na maabara hizo ziweze kukamilika kwa wakati  ili watoto wajifunze masomo ya sayansi kwa vitendo.

Mama Kikwete yupo wilayani humo kwa ajili ya kuimarisha kazi za chama hicho ikiwa ni pamoja na kufanya vikao na viongozi na kuangalia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010 . Hadi sasa ameshatembelea matawi 64 kati ya  82 yaliyopo wilayani humo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Mama mwalimu Salma,hili somo ulilotoa ni kubwa tena muhimu sana kwa wananchi wote wa mikoa ya mwambao ya pwani,kwani thamani ya ardhi kila siku inapanda,leo kama mtu akiuza eneo la ufukweni kwa siku za usoni atajutia uamuzi wake na kizazi chake kitakuwa watumwa katika ardhi yao wenyewe,leo hii angalia wenyeji wa asili wa Dar,wamekuwa wageni katika mji wao,na wajanja mafisadi wanatumia vitisho kuwafukuza wenyeji,kuanzia msasani,mbezi beach,kunduchi,Tageta,madale,bunju,boko kote wenyeji wameshauza au kufukuzwa kiujanja kwa vitisho.Kigamboni nako na mradi wa KDA,kuna wajanja wanajaribu kutaka kuwaondoa wenyeji,ARDHI NI MALI

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...