WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameutaka uongozi wa mkoa wa Iringa uangalie uwezekano wa kuanzisha Halmashauri mpya katika wilaya ya Kilolo kata ya Mahenge na tarafa ya Mahenge kwa sababu ya hali ya kijiografia ya eneo hilo. 
 “Makao makuu ya wilaya hii yako Kilolo kule milimani. Ukitaka kuja huku ni lazima upite kwanza mjini ndipo ufike huku. Hapana! Hatuwezi kuwasaidia wananchi hawa kujiletea maendeleo kwa staili hii,” alisema Waziri Mkuu. 
 Alikuwa akihutubia wakazi wa vijiji vya Nyanzwa na Igunda wilayani Kilolo, jana jioni (Jumamosi, Februari 21, 2015) mara baada ya kukagua mradi wa umwagiliaji wa Nyanzwa ambao ni maarufu kwa kilimo cha vitunguu. Vijiji hivyo viko umbali wa km. 120 kutoka Ipogoro ilipo njia panda ya kwenda Iringa mjini na km. 155 kutoka Kilolo mjini yalipo makao makuu ya wilaya hiyo. 
 Waziri Mkuu alisema kata za tarafa hiyo ni kubwa mno kwa mtendaji kuweza kusukuma maendeleo ya wananchi.
 “Kata hii imeanzia Kitonga hadi huku Nyanzwa. Hivi ni mtendaji gani anayeweza kuja kuhimiza shughuli za maendeleo akitokea huko?” alihoji Waziri Mkuu huku akishangiliwa. 
 Alisema mbali na idadi ya watu, suala la kijiografia huwa linaangaliwa wakati wa kuanzisha maeneo ya utawala. “Hili eneo ni zuri, fursa zipo lakini linakosa usimamizi ndiyo maana hata wilaya hii inaongoza kwa umaskini kuliko wilaya nyingine za mkoa huu. 
"Acheni wilaya ibaki moja, mbunge abaki mmoja lakini Halmashauri ziwe mbili ili muweze kusukuma maendeleo ya eneo hili kwa sababu mtakuwa na madiwani wenu na bajeti yenu,” alisema. Mapema, akisoma taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mtendaji wa Kijiji cha Nyanzwa, Bw. Hekima Masanula Katemo alisema skimu ya umwagiliaji ya Nyanzwa ilijengwa mwaka 1960 wakati huo kwa kutumia banio la miti na magunia ya mchanga. 
Ilikuja kuboreshwa miaka ya 90 kwa ufadhili kutoka Jumuiya ya Ulaya na Serikali ya Sweden. 
 “Hata hivyo, skimu hii ambayo inahudumia wakulima 3,469 wakiwemo wanaume 1,662 na wanawake 1,807; inakabiliwa na uhaba wa maji kwani ni hekta 256 tu ambazo zinamwagiliwa kwa sasa wakati eneo lote la mradi ni hekta 940,” alisema Bw. Masanula. 
 Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake mkoani Iringa kwa kutembelea Manispaa ya Iringa ambako atakagua ujenzi wa maabara kwenye shule ya sekondari Kihesa, kuzindua kituo cha polisi cha Semtema, na kukagua huduma za afya kwenye hospitali ya manispaa ya iringa. 
Pia atakagua mradi wa machinjio ya kisasa ya Ngelewela kabla ya kutubia mkutano wa hadhara kwenye viwanja wa shule ya msingi Ipogolo. 

 IMETOLEWA NA: OFISI YA WAZIRI
 MKUU, JUMAPILI, FEBRUARI 22, 2015.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisalimiana na wauguzi wa hospitali ya Manispaa ya Iringa iliyopo eneo la Frelimo baada ya kuitembelea na kuzungumza na wananchi hospitalini hapo akiwa katika ziara ya mkoa wa Iringa Februari 22, 2015
 Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na Wananchi na watumishi wa  Hospitali ya Manispaa ya Iringa iliyopo Frelimo baada ya kuitembelea akiwa katika ziara ya mkoa wa Iringa Februari 22, 2015.Wapili kulia ni Mkewe Tunu na kulia ni Mbunge wa Iringa, Mchungaji  Peter Msigwa
  Mke wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda akimpongeza, Gaudencia Malangalizi  ambaye amejifungua watoto mapacha wa kiume katika hospitali ya Manispaa ya Iringa iliyopo eneo la Frelimo  Februari 22, 2015. Mama Pinda aliambatana na Waziri Mkuu, Mizengo  Pinda ambaye alitembelea hospitali hiyo.
 Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akifungua Kituo cha Polisi cha SEMTEMA kilichopo Iringa Mjini ambacho kimejengwa na Mbunge wa Viti Maalum, Ritta Kabati (wapili kushoto) Februari 22, 2015. Mheshimiwa Pinda yuko katika ziara ya mkoa wa Iringa. Watatu kushoto ni Mbunge wa Viti Maalum Lediana Mng'ong'o.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiwasalimia walimu wa Shule ya Sekondari ya Kihesa, Iringa mjini  kabla ya kukagua ujenzi wa Maabara na kuhutubia wananchi akiwa katika ziara ya mkoa wa Iringa Februari 22, 2015

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...