Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Ngosi Mwihava. |
Na
Asteria Muhozya, Dar es Salaam
Matokeo ya
utekelezaji wa utoaji wa ruzuku kwa wachimbaji Madini wadogo nchini Awamu ya
Pili yanatarajiwa kufanyiwa tathmini na ufuatiliaji kupitia Mpango wa Matokeo
Makubwa Sasa (BRN).
Hayo yamebainishwa na
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Ngosi Mwihava wakati
akiongea katika Kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa kupitia Televisheni ya
Taifa TBC1 mapema leo, ambapo amefafanua kuhusu taratibu za maombi ya namna ya kupata
ruzuku kwa wachimbaji wadogo wa madini Awamu ya Pili.
Mhandisi Mwihava
ameeleza kuwa, ili kupata matokeo bora ya namna ruzuku hiyo itakavyotumiwa na
wachimbaji wadogo watakaokidhi vigezo vya maombi na kunufaika na ruzuku hiyo,
mpango wa BRN utatumika ipasavyo kuhakikisha kwamba fedha hizo zinatumika kama
ilivyopangwa.
“BRN itatumika
kufuatilia utekelezaji wa ruzuku. Wizarani tuna Sehemu ya Ukaguzi wa Migodi, lakini
pia tuna Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), hawa wote watashirikiana kufanya
tathmini yenye matokeo tunayotarajia,” amesisitiza Mhandisi Mwihava.
Ameongeza kuwa,
kiwango cha ruzuku kwa wachimbaji wadogo Awamu ya Pili kimeongezwa kufikia Dola
za Marekani 100,000/-, ruzuku ambayo inalenga katika kuendeleza uchimbaji mdogo
ili uwe na tija; kuwakwamua wachimbaji wadogo kiuchumi na kuongeza pato la
taifa.
Aidha, ameeleza kuwa malengo
mengine ya ruzuku hiyo kwa wachimbaji wadogo wa Madini kuwa ni kuendeleza
mkakati wa kurasimisha shughuli za uchimbaji mdogo wa madini na kutoa mitaji
ili kusaidia ukuaji wa tasnia ya uchimbaji mdogo wa madini.
Malengo mengine ni
pamoja na uongezaji thamani ya madini wenye Matokeo
Makubwa Sasa.
Ameongeza kuwa,
Serikali imedhamiria kuwasaidia wachimbaji wadogo nchini kuwawezesha kuwa wachimbaji
wa kati, jambo ambalo limefanya Serikali kuzifanyia kazi changamoto zilizojitokeza
katika utoaji ruzuku na mikopo awamu ya kwanza.
“Tunataka kuwasaidia
mitaji, kuwapatia vifaa na kuhakikisha wanapata uelewa wa namna ya kufanikisha
shughuli zao kupitia wataalamu wetu. Tunalenga kuwafanya wakue hadi kuwa
wachimbaji wakubwa”, ameongeza Mwihava.
Aidha, Mhandisi
Mwihava ametumia fursa hiyo kuwataka wachimbaji wadogo kuzitumia ofisi za
madini zilizoko mikoani kwa ajili ya kuchukua fomu za maombi kuanzia tarehe 2
Machi na kuwataka kuzirejesha fomu hizo katika ofisi hizo ifikapo tarehe 27
Machi, 2015, zikiwa na viambatanisho vyake.
Katika hatua
nyingine, Mhandisi Mwihava amesema kuwa, migodi inayoshirikisha watoto wadogo
katika shughuli za uchimbaji madini watanyanga’nywa leseni zao endapo
itabainika kuwa, migodi hiyo inawashirikisha watoto, na hivyo kuwataka
wachimbaji kufuata sheria na taratibu.
“Watoto kushiriki
katika shughuli za uchimbaji ni makosa. Watakaobainika watanyang’anywa leseni
zao. Wizara inapinga si haki kwa watoto kufanya shughuli za uchimbaji madini”, alisisitiza
Mwihava.
Awamu ya pili ya
utoaji ruzuku kwa wachimbaji wadogo nchini, inatekelezwa kupitia Wizara ya
Nishati na Madini, chini ya Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini
(SMMRP), unaopata fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...