Bingwa wa zamani wa dunia wa uzito wa juu, Francois
Botha na rais wa chama cha ngumi cha dunia cha WBF, Howard Goldberg
wanatarajiwa kuwasili nchini kesho Machi 23, tayari kwa kusimamia pambano la Mohamed Matumla Jr
na Wang Xiu Hua wa China.
Botha atawasili nchi kwa mara ya pili kwa mualiko maalumu wa Kampuni
ya Hall Of Fame inayoandaa mapambano ya ngumi ndani na nje ya nchi.
Nguli huyo wa masumbwi anatarajiwa kuwasili saa 12 jioni na ndege ya
Shirika la ndege la Afrika Kusini sambamba na Goldberg wakiwa na
mkanda wa dunia wa WBF wa uzani wa Super Bantam utakaowania na Matumla
Jr na Hua Ijumaa hii kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Hall of Fame, Jay Msangi alisema kuwa,
baada ya kuwasili, Botha atashiriki katika programu mbalimbali za
pambano hilo ambalo kama Matumla Jr akionyesha kiwango atakata tiketi
ya kuzichapa pambano la Utangulizi kwenye lile la dunia kati ya Floyd
Mayweather na Manny Pacquiao la Mei 2 jijini Las Vegas,Marekani.
.jpg)
Wakati huohuo, mpinzani wa Matumla anatarajiwa kuwasili saa saba
mchana wa kesho akitokea China tayari kwa pambano lao la Ijumaa.
Hua atawasili jijini akiwa ameambatana na kocha wake sambamba na
viongozi wengine wa ngumi wa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa Msangi, baada ya kuwasili bondia huyo ataendelea na
mazoezi kabla ya kushiriki zoezi la kupima uzito na afya
litakalofanyika Alhamisi hii.
Katika hatua nyingine, mabondia Ashraf Suleiman, Mada Maugo, Karama
Nyilawila, Japhet Kaseba na Thomas Mashali wako katika maandalizi ya
mwisho kuelekea kwenye mapambano yao ya Ijumaa.
Mabondia hao watapanda ulingoni kuzichapa kabla ya Matumla Jr na Hua
kupanda kuwania ubingwa wa dunia.
Mashali atazichapa na Nyilawila pambano lisilo la ubingwa la uzani wa
super bantam wakati Maugo akizichapa na Kaseba kwenye uzani wa super heavy na Suleiman akionyeshana ubabe na bondia kutoka Marekani pambano la uzani wa juu siku hiyo.
Kwa nyakati tofauti, mabondia hao kila mmoja alijinadi kumkung'uta mwenzake siku hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...