Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimraribisha Rais Paul Kagame wa Rwanda kwenye ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Kanda ya Kati (Central Corridor Conference) ulioanza jana na kumalizika leo Machi 26, 2015.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete na wageni wake Rais Paul Kagame wa Rwanda na Rais Pierre Nkurunzinza kwenye ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Kanda ya Kati (Central Corridor Conference) ulioanza jana na kumalizika leo Machi 26, 2015.
Rais Paul Kagame wa Rwanda akipeperusha bendera kuashiria kuzinduliwa kwa safari za treni za mizigo kuelekea Rwanda katika stesheni ya reli ya Dar es salaam akiwa na mwenyeji wake Rais Jakaya Mrisho kikwete leo Machi 26, 2015.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na mgeni
wake, Rais Paul Kagame wa Rwanda, leo, Alhamisi, Machi 26, 2015, wametembelea
Bandari ya Dar es Salaam na baadaye Rais Kagame ameanzisha safari ya treni
maalum za kusafirisha mizigo ya Rwanda kutoka Tanzania.
Rais
Kagame amewasili nchini asubuhi ya leo na kufungua Mkutano wa Wawekezaji katikaUjenzi
wa Miundombinu Ukanda wa Kati (High
Level Investors Forum – Central Corridor Development Acceleration Programme) uliofanyika
kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere mjini Dar es Salaam.
Mara
baada ya hotuba ya ufunguzi na kipindi cha maswali kutoka kwa washiriki na
majibu kutoka kwa viongozi wa nchi tano zinazounda Shirika la Uwezeshaji wa
Usafiri wa Ukanda wa Kati (The Central Corridor Transit Transport
Facilitation Agency (CCTTFA), viongozi hao wawili wamekwenda Bandari ya
Dar es Salaam.
CCTTFA
lilianzishwa Septemba 2, mwaka 2006, na Makubaliano yaliyotiwa saini na nchi
tano ambazo zinanufaika na usafiri wa Ukanda wa Kati – Tanzania, Burundi,
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Rwanda na Uganda.
Katika
Bandari ya Dar es Salaam, Rais Kagame na mwenyeji wake wameanza kwa kutembelea
ofisi mpya za Mpango wa Ukusanyaji Ushuru kwa Pamoja (Single Customs Territory)
miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), mpango
ulioanza kutumika Julai mwaka jana, 2014. Chini ya Mpango huo, kila nchi
inashughulikia mizigo yake yenyewe, ikiwa ni pamoja na kukusanya kodi yake.
Rais
Kagame na mwenyeji wake wametembelea ofisi za Mamlaka ya Kodi ya Rwanda (RRA)
na Mamlaka ya Kodi ya DRC ambako walipewa maelezo kuhusu faida za mpango huo.
Miongoni
mwa mambo mengine, marais hao walielezwa kuwa chini ya Mpango huo, waagizaji wa
mizigo ya Rwanda, kupitia Bandari ya Dar es Salaam, sasa wanajaza fomu moja tu
badala ya tatu na sasa mizigo ya Rwanda inachukua siku mbili tu kutoka Bandari
ya Dar es Salaam hadi Kigali, badala ya siku kati ya tano na 10 kabla ya
kuanzishwa Mpango huo.
Nchi
ambazo tayari zimefungua ofisi zao katika Bandari hiyo kutekeleza Mpango huo ni
Tanzania yenyewe, Burundi, DRC na Rwanda. Uganda inakamilisha maandalizi ya
utekelezaji na Zambia imeonyesha nia ya kujiunga na Mpango huo, kwa sababu
inapitishia mizigo yake katika Bandari ya Dar es Salaam, hata kama siyo
mwanachama wa EAC.
Kutoka
kwa ofisi za Single Customs Territory, viongozi hao wamekwenda kwenye
Bandari ya Dar es Salaam ambako wamepatiwa maelezo kuhusu jinsi utendaji wa
Bandari hiyo ulivyoboreka katika miaka miwili iliyopita.
Aidha,
viongozi hao wameelezwa jinsi gani pia utendaji wa kampuni binafsi ya upakiaji
na upakuaji mizigo ya TICTS inavyofanya kazi na ilivyoboresha utendaji wake
katika sehemu nne za meli kutia nanga (berths) ambako inafanyia kazi yake
katika Bandari hiyo yenye sehemu 11 za kupakia na kupakulia mizigo.
Katika
Bandari hiyo, marais hao wameelezwa kuwa katika miaka mitano iliyopita, kiwango
cha mizigo inayopitia katika Bandari hiyo kimekuwa kinaongezeka kwa wastani wa
asilimia 12.8 kila mwaka.
Wameelezwa
pia kuwa mwaka jana, kiasi cha tani milioni 14.6 ya mizigo kilipitia katika
Bandari hiyo zikiwemo kontena 621,000 na kuwa kati ya mizigo hiyo kiasi cha
asilimia 34, sawa na mizigo tani milioni 5.020 ilikuwa mizigo kwa ajili ya nchi
za jirani.
Aidha,
viongozi hao wameelezwa kuwa muda wa kontena kukaa Bandarini hapo sasa ni siku
tisa tu badala ya siku 21 Februari mwaka 2008, muda wa meli kukaa nje ya
Bandari ikisubiri kuingia Bandarini ili ipakuliwe, sasa ni siku moja unusu
badala ya siku tatu unusu za mwaka 2013.
Marais
Kagame na Kikwete pia wameelezwa kuwa usalama wa mizigo ya waagizaji sasa umeongezeka
mno, kiasi cha kwamba halijakuwepo tukio hata moja la wizi wa mizigo ya wateja
yakiwemo magari na spea zake kwa miaka mitatu mfululizo sasa.
Bandari
ya Dar es Salaam ambayo huhudumia mizigo ya nchi saba – ya Tanzania yenyewe,
Malawi, Zambia, DRC, Burundi, Rwanda na Uganda pia huendesha Bandari kwenye
maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.
Jana,
Jumatano, Machi 25, 2015, Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi pamoja na
wawakilishi wa nchi za DRC na Uganda pia walianzisha safari za treni za namna
hiyo kwenda katika nchi zao.
Rais
Kagame ameondoka nchini kurejea kwao leo baada ya kuanzisha safari hizo na
mkutano wenyewe kuhusu Ukanda wa Kati, ambao pia ulihudhuriwa na Rais Yoweri
Museveni wa Uganda, umemalizika jioni ya leo.
Imetolewa
na;
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam .
26
Machi, 2015
Naona tumejitahidi kuboresha usafiri wa mizigo kwa njia ya reli kwenda nchi jirani. Endelezeni kazi nzuri.
ReplyDelete