WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali itawasilisha Bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wenye sehemu 14 likiwemo suala la Mahakama ya Kadhi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam, jana jioni (Jumatano, Machi 11, 2015) Waziri Mkuu alisema Serikali inakusudia kuwasilisha muswada huo kwenye mkutano ujao wa Bunge unaotarajiwa kuanza Jumanne ijayo, (Machi 17).
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewasihi Watanzania waondoe hofu iliyoenezwa na tetesi kwamba muswada huo una lengo la kuiingiza mahakama hiyo kwenye Katiba Inayopendekezwa na kuwataka wazipuuze tetesi hizo.
“Hakuna ukweli wowote kwenye jambo hilo kwa sababu Bunge la Katiba lilikwishavunjwa na Bunge lijalo halina mamlaka ya kufanya hivyo. Hili ni Bunge la sasa haliwezi kubadili maamuzi ya awali… Jambo hili halina ujanjaujanja au njama zozote za kuliingiza Kwenye Katiba Inayopendekezwa,” alisema.
“Hizo ni hofu za kweli zilizosambaa na inategemea jinsi mtu alivyoelewa suala zima. Kikubwa ni kutambua kwamba Mahakama ya Kadhi zimekuwa zinafanya kazi hapa nchini tangu mwaka 2012 lakini kwa kuendeshwa na wao wenyewe na siyo Serikali,” alisema.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...